LIREFA Yampongeza Mama Salma Kikwete Kuinua Soka

MKE wa Rais Mama Salma Kikwete

Na Anna Nkinda – Maelezo

MKE wa Rais Mama Salma Kikwete amepongezwa kwa jitihada zake za kuinua sekta ya michezo nchini jambo ambalo limewafanya vijana wengi kujipata ajira katika fani hiyo.

Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu cha Mkoa wa Lindi (LIREFA), Francis Ndulane wakati wachezaji wa timu ya Kariakoo ya mkoa huo walipotembelea Ofisi za Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) zilizopo Ikulu jijini Dar es Salaam.

Ndulane alisema kuwa mchango unaotolewa na Mama Kikwete umewapa hari na kuwatia moyo vijana wengi na hivyo kuweza kuendeleza sekta ya michezo mkoani humo.

Alisema kuwa hapa nchini vijana wengi wana vipaji mbalimbali, lakini hawana watu wa kuwaendeleza, hivyo alimshukuru kwa jitihada zake za kuwaendeleza katika sekta hiyo na hivi sasa wanaamini kuwa wataweza kujiajiri na kuweza kuzisaidia familia zao.

Kwa upande wake Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA aliwapongeza wachezaji hao kwa juhudi kubwa wanayoifanya katika soka hadi kufikia hatua ya kushiriki ligi ya taifa ya mabingwa wa mkoa ngazi ya taifa na kufikia hatua ya nane bora.

Naye Mwenyekiti wa timu hiyo Abdalah Livemba aliwashukuru Mama Kikwete na Waziri wa Mambo ya Nje Bernard Membe kwa moyo walionao wa kuisaidia timu hiyo hadi kufikia hapo ilipo. Alimuomba kuwatafutia mdhamini ili awezkuwasaidia kubeba mzigo mkubwa wa kuitunza timu hiyo ambao unaelekea kuwalemea.

Mama Kikwete aliikabidhi timu hiyo zawadi za viatu jozi 29, jezi seti mbili zikiwa na idadi ya jezi 32 kila seti, mipira mitatu, pampu moja na soksi jozi 16.

Timu ya Kariakoo inashiriki mashindano ya ligi ya mabingwa mkoa ngazi ya Taifa ambayo yalianza Juni 12, 2013 kwa kuzishirikisha timu 28 kutoka nchi nzima wao wamebaki kati ya timu nane na leo wanapambana na Friends Rangers ya mkoa wa Dar es Salaam mchezo utakaofanyika katika uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi jijini Dar es Salaam.