Lindi Yajivunia Upatikanaji Huduma ya dawa za Maambukizi ya VVU

Lindi

Na Anna Nkinda – Maelezo, Lindi
Kuimarika kwa upatikanaji wa huduma ya kupewa dawa za kuzuia maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kwa wamama wajawazito ili kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto zimesababisha watoto wengi kuzaliwa wakiwa salama.

Hayo yamesema na Dkt. Zulfa Msami wakati akisoma taarifa ya kituo cha Afya cha Manispaa ya Lindi kwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi mjini Mama Salma Kikwete alipotembelea kituo hicho.

Dkt Msami alisema kwa mwaka 2014 wamama wajawazito 241 kati ya 280 walipima VVU katika kituo hicho kati yao 30 sawa na asilimia 12 walikutwa na maambukizi na kwa upande wa watoto ambao mama zao walikuwa na maambukizi 35 walipimwa na mtoto mmoja aligundulika kuwa na maambukizi.

“Kituo kilianza kutoa huduma endelevu ya VVU/UKIMWI mwaka 2008, mpaka Disemba mwaka 2014 kuna wateja 997 wanaopatiwa huduma kati ya hao 579 sawa na asilimia58 wanatumia  dawa za kupunguza makali ya VVU. Tunahudumia wateja wote bila malipo yeyote na dawa zimekuwepo kwa kipindi chote cha mwaka hadi sasa”, alisema Dkt. Msami.

Kwa upande wa huduma ya kujifungua alisema huduma hiyo ilianza kutolewa mwaka 2008 kituo kina  vitanda 10 ya kulaza wagonjwa kwa mwaka jana kina mama wajawazito 288 walijifungua kituoni sawa na asilimia 100 ya matarajio ya kinamama kujifungua katika kituo hicho.

Huduma zingine zinazotolewa katika kituo hicho ni huduma za wagonjwa wan je (OPD), afya ya uzazi na mtoto (RCH), maabara, uzazi wa mpango, elimu ya afya, upimaji virusi kwa hiari na ushawishi(VCT), kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT), huduma endelevu kwa waishio na VVU/UKIMWI (CTC) na huduma za majumbani (HBC), huduma kwa wamama wajawazito na za chanjo.

Naye Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliwataka watu wanaoishi na VV U kutokujinyanyapaa wenyewe na ugonjwa huo kwani hivi sasa kuna dawa za kupunguza makali ya ugonjwa na mgonjwa akitumia dawa hizo ananenepa na kuwa na afya njema kama watu wengine na pia wagonjwa wengi wanajitokeza hadharani na kusema hali yao.

Mama Kikwete alisema, “Maambukizi ya VVU katika mkoa wa Lindi yamepungua kutoka  asilimia 4.2 kwa mwaka 2013 hadi  asilimia 3.8 kwa mwaka 2014 jitahidini kutoa elimu kwa jamii ili yasiongezeke kwani Tanzania bila Ukimwi inawezekana”.

Mama Kikwete pia aliwahimiza viongozi wa CCM na watumishi wa Afya wawaelimishe wananchi ili wajiunge na mfuko wa afya ya jamii (CHF) na mfuko wa Taifa wa bima ya afya (NHIF)  kujiunga kwao na huduma hizo kutawawezesha kupata huduma ya matibabu  wakati wowote pindi watakapoumwa hata kama hawana  fedha.

Kituo hicho ni kituo pekee cha Afya kilichopo katika Manispaa ya Lindi kilianza kazi kama zahanati mwaka 1962 kutokana na ongezeko la idadi ya watu wanaohudumiwa pamoja na huduma mbalimbali za afya  zinazotolewa kituo kilipandishwa hadhi na kuwa kituo cha Afya mwaka 2002 na kinahudumia wakazi 6637.
Mwisho.