LIGI Kuu ya Vodacom inatarajiwa kuendelea mwishoni mwa wiki kwa viwanja sita kutimua vumbi, michezo mitatu ikifanyika siku ya Jumamosi na michezo mingine mitatu kufanyika siku ya Jumapili.
Katika Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, wenyeji timu ya Polisi Morogoro watawakaribisha maafande wa Ruvu Shooting kutoka Mlandizi, Coastal Union watakua wenyeji wa Kagera Sugar kwenye dimba la Mkwakwani, huku JKT Ruvu wakiwakaribisha Azam FC katika uwanja wa Azam Complex Chamazi.
Jumapili Mgambo JKT watakua wenyeji wa timu ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, huku Mtibwa Sugar wakiwa wenyeji wa wagonga nyundo timu ya Mbeya City katika Uwanja wa Manungu Turiani. Katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam watani wa jadi Simba SC watakuwa wenyeji wa Young Africans, mchezo unaotarajiwa kuanzakutimua vumbi majira ya saa 10 kamili jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
KUZIONA SIMBA, YANGA SH.7,000
Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetangaza viingilio vya mchezo wa siku ya jumapili kati ya Simba SC na Young African utakaofanyika kwenye dimba la Uwanja wa Taifa kuanzia majira ya saa 10 kamili za jioni.
Mchezo huo utachezeshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro, akisaidiwa na Soud Lila (DSM) mshika kibendera wa kwanza, Florentina Zabron (Dodoma) mshika kibendera wa pili, Mwamuzi wa akiba Israel Mjuni (DSM), na kamisaa wa mchezo ni Ame Santimeya (DSM).
Viingilio vya mchezo huo, VIP A sh. 40,000, VIP B sh. 30,000, VIP C sh. 20,000, Rangi ya Machungwa (Orange) sh. 10,000, huku Rangi ya Bluu na Kijani ikiwa ni sh. 7,000.
Tiketi zitaanza kuuzwa keso (jumamosi) saa 2 kamili asubuhi katika vituo vya, Karume (Ofisi za TFF), Mgahawa wa Steers (Posta Mpya), Oilcom (Buguruni), BigBon (Kariakoo), Olicom (Ubungo), Dar Live (Mbagala), Uwanja wa Uhuru, Kivukoni (Ferry) na Makumbusho (kituo cha mabasi).
Magari yenye vibali maalum ndiyo yatakayoruhusiwa kuingia ndani ya uwanja siku ya jumapili kwa kupitia barabara ya Mandela na Uwanja wa Uhuru, barabara ya Chang’ombe itafungwa kuanzia saa 12 kamili asubuhi.
TFF inawaomba, wapenzi, washabiki na wadau wa mchezo kununua tiketi katika vituo vilivyotajwa ili kuepuka kuuziwa tiketi bandia, ili kuimarisha ulinzi na usalama wa mchezo, mashabiki wenye mabegi, silaha, vilevi na chupa za maji hawataruhusiwa kuingia navyo uwanjani.
Aidha katika mchezo huo TFF itatoa ujumbe maalum kupitia kwa wachezaji kuhamasisha juhudi za Taifa za kuzuia mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino).