Libya yashambuliwa kutoka kila kona

UINGEREZA, Marekani na Ufaransa zimeyashambulia majeshi ya kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi kutokea angani, majini na nchi kavu katika tukio la kwanza la utekelezaji amri ya Umoja wa Mataifa (UN) ya kuzuia ndege kuruka.

Maofisa wa Pentagon, wizara ya ulinzi ya Marekani wanasema Marekani na Uingereza zimevurumisha zaidi ya makombora 110 huku ndege za Ufaransa zikiyashambulia majeshi yanayomtii Gaddafi katika mji unaoshikiliwa na waasi wa Benghazi.

Kanali Gaddafi ameapa kulipa kisasi na amesema atafungua maghala ya silaha kuwapatia watu wailinde Libya, katika vita aliyosema haitakuwa na mwisho.

Makombora yalipiga maeneo ya jeshi la anga katika mji mkuu wa nchi hii, Tripoli, na Misrata.

Televisheni ya taifa ya Libya ilisema kwamba watu 48 wameuawa na wengine 150 kujeruhiwa katika mashambulizi hayo.

Hata hivyo, hakukuwa na uthibitisho huru kuhusu vifo hivyo.
Ndege ya Ufaransa ilivurumisha makombora katika maeneo ya serikali ya Libya jioni ya juzi na kuharibu idadi kadhaa ya magari ya kijeshi, kwa mujibu ya msemaji wa jeshi la nchi hiyo.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron alithibitisha kuwa ndege za Uingereza zinashiriki katika operesheni hiyo nchini Libya.

Pamoja na kwamba ni ndege za kivita za Ufaransa zilizoanzisha mashambulizi ya kwanza, ni wazi awamu ya kwanza ya operesheni hiyo imeratibiwa zaidi na Marekani pamoja na uchache wa mashambulizi yake ya makombora kutoka meli na manowari.

Ni jeshi la Marekani lenye uwezo zaidi wa kulibomoa jeshi la anga la Libya ili kutekeleza amri ya kutoruka, lakini yaonyesha Rais Barack Obama ameweka ukomo wa nchi yake kujihusisha katika mgogoro huo.

chanzo:gazeti la Mtanzania