RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Leodgar Tenga amesema Tanzania itatumia mashindano ya soka kwa wanawake na vijana kama sehemu mojawapo ya kueneza kampeni dhidi ya ugonjwa wa Malaria.
Ametoa kauli hiyo juzi Februari 9, 2013 wakati alipokuwa akichangia mjadala kuhusu juhudi za sekta binafsi katika kupambana na ugonjwa wa malaria uliofanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Sandton, kilichopo jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Mjadala huo uliambatana na hafla ya chakula cha jioni.
Alisema Tanzania imedhamiria kuwa mbia katika kampeni ya kupambana na malaria, kwani inajua umuhimu wa kuwa na makocha na wachezaji wenye afya njema.
“Kampeni hii ni nzuri, tena ya muhimu sababu inalenga kuelimisha jamii juu ya kujikinga na ugonjwa wa Malaria. Ili ufanikiwe katika michezo, ni lazima uwe na wachezaji na makocha wenye afya, ambao si wagonjwa,” alisisitiza.
Naye Mark Fish ambaye zamani aliichezea timu ya soka ya Bafana Bafana ya Afrika Kusini, alisema anatambua adha ya ugonjwa, sababu wakati akicheza soka Zimbabwe aliwahi kuugua Malaria.
“Nina matumaini makubwa ya kushiriki kampeni hii ya kupambana na ugonjwa wa Malaria, alisema Bw. Fish wakati akihojiwa na Bi. Carol Tshabalala, mtangazaji wa kituo cha televisheni cha SuperSport.
Naye Mtendaji Mkuu wa Benki ya Standard Chartered ya Afrika Kusini, Bw. Sim Tshabalala alisema karne hii itakuwa ni karne ya kushangaza kwani wamedhamiria kupambana na ugonjwa huu kwa namna yoyote ile.
Alisema Benki hiyo imeungana na wenzao wa Tanzania katika Programu ya “Malaria Haikubali”. Benki hiyo imeajiri wafanyakazi zaidi ya 25,000 nchini Afrika Kusini.
Akizungumzia kuhusu juhudi za Benki hiyo katika kampeini dhidi ya Malaria, Bw. Tshabalala ambaye alihojiwa na Bi. Carol Tshabalala wa SuperSport katika raundi ya pili ya mjadala mchango wa sekta binafsi kwenye vita dhidi ya malaria, alisema mwaka 2009-2010 Benki hiyo ilitumia dola za Marekani milioni 600 kwa ajili ya matibabu ya wafanyakazi waliougua malaria.
“Tumeeamua kudhamini kampeni hii kwa kugawa vyandarua 11,000 kwa wafanyakazi wetu na vyandarua vingine 50,000 tumevigawa kwa wanajamii. Pia tumetoa elimu kwa watumishi, familia zao na wananchi ili kukuza uelewa wao kuhusu ugonjwa huu,” alisema.
Naye Mjumbe wa Taasisi ya Global Fund, Bw. Brian Brink alisema zinahitajika zaidi ya dola za Marekani bilioni tatu kutoka kwa wafadhili mbalimbali ili kuendeleza kampeni dhidi ugonjwa wa Malaria.
Alisema gharama za Mpango huo kwa bara la Afrika peke yake zimefikia dola za Marekani bilioni 12 kwa mwaka, lakini anafarijika anapoona njia mbadala za kukabili ugonjwa huo zinatumiwa.
“Tanzania ni mfano wa kuigwa katika kampeni, hasa kwa vile imeweka jitihada za kutumia mbadala kama vile upuliziaji wa dawa ukoko (Residual Spraying) na kutengeneza dawa za mseto za gharama nafuu. “Dozi ya ALU haizidi Dola 10 za Marekani, kwa kweli wao ni mfano wa kuigwa,” alisema huku akishangiliwa na idadi kubwa ya wageni walioshiriki kusikiliza mjadala huo.