CALIFORNIA, Marekani
MWISHO wa dunia umefika na huenda tusiione tena Jumapili ya kesho kwani dunia inafikia mwisho wake leo Jumamosi, kwa mujibu wa Mchungaji wa Kanisa moja la California.
Mchungaji Harold Camping wa California, ametabiri kuwa mwisho wa dunia ni leo
Mei 21 mwaka huu saa moja kamili usiku.
Mchungaji Camping kwa kutumia mahesabu ya tarehe na mafunzo ya Biblia, ametabiri kuwa kiama kitakuwa leo.
Amesema miezi mitano baadaye Oktoba 21 mwaka huu, Mungu ataiteketeza dunia na Wakristo waliozingatia neno la Mungu watapaishwa mbinguni kukutana na Yesu.
Mchungaji Camping anamiliki radio ya dini ya Christian Family Radio Network yenye mtandao mkubwa Marekani na sehemu nyingine dunia.
Radio yake inarusha matangazo kwa lugha 48 Marekani na nchi nyinginezo ikiwemo Afrika Kusini.
Mchungaji Camping (89), ana wafuasi wengi duniani na amekuwa akipiga kampeni za kuwajulisha watu mwisho wa dunia ni Mei 21.
Magari yenye mabango yenye ujumbe wa mwisho wa dunia Mei 21 yamekuwa yakionekana sehemu mbalimbali za Marekani.
Anasema kuwa mwisho wa dunia ni Mei 21 kwa sababu itakuwa ni siku ya 722,500 tangu Yesu aliposulubiwa msalabani Aprili Mosi AD33 kwa mujibu wa hesabu za Mchungaji Camping.
Mchungaji Camping anasema namba 722,500 ni muhimu sana kwa Wakristo duniani kwani inapatikana kwa kuzizidisha namba tatu tukufu (5, 10, 17) mara mbili (5X10X17X5X10X17).
Hii si mara ya kwanza kwa Mchungaji
Camping kutabiri matukio makubwa duniani.
Septemba 6, 1994, Mchungaji Camping na wafuasi wake wengi walikusanyika mbele ya ukumbi wa Alameda wakisubiri kurudi kwa Yesu Kristo ambaye hakutokea.
Tangu wakati huo, Mchungaji Camping alisema kuwa wamefanya utafiti mkubwa na hivyo wana uhakika safari hii utabiri wao utakuwa sahihi.
Ciao…