Leo ni kumbukumbu ya Edward Moringe Sokoine

Edward Moringe Sokoine

Na Mwandishi Wetu,

LEO ni kumbukumbu ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania, hayati Edward Moringe Sokoine. Maadhimisho ya kumbukumbu hizo yanafanyika eneo ambalo alipata ajali kiongozi huyo njiani akitokea Dodoma kuja Dar es Salaam ikiwa ni miaka 28 tangu kifo chake.

Taarifa zinasema Waziri Mkuu wa sasa Mizengo Pinda ndiye atakayekuwa mgeni rasmi akiiwakilisha Serikali katika maadhimisho hayo yatakayoanza kwa kufanya ibada eneo ulipojengwa mnara wa kumbukumbu yake.

Hayati Sokoine aliyekuwa kipenzi kikubwa cha Watanzania kutokana na uongozi wake uliotukuka alikuwa Waziri Mkuu mara mbili, tangu Februari 13, 1977 hadi Novemba 7, 1980 na pia kushika nafasi hiyo tena Februari 24, 1983 hadi kifo chake.

Uongozi wa Sokoine enzi zake ulionekana kuwa wa mfano kwa jinsi alivyokuwa na uadilifu na kufuatilia utendaji kazi huku akikemea ulaji rushwa na ubadhirifu wa mali za umma. Sokoine alifariki kwa ajali ya gari Aprili 12, 1984, wakati akitoka kwenye kikao cha Bunge Mjini Dodoma kwenda Dar es Salaam.

Kifo chake kilileta majonzi makubwa kwa Watanzania wa kawaida ambao walikuwa wanamtarajia kuwatetea wanyonge na kuinua hali ya maisha yao. Mwili wa Edward Moringe Sokoine ulizikwa nyumbani kwao Monduli, mkoani Arusha. Chuo cha Kilimo na Mifugo Morogoro kilipewa jina la “Chuo cha Kilimo cha Sokoine” ambacho kwa sasa ni Chuo Kikuu cha Sokoine kulinda heshima na kumbukumbu ya kiongozi huyo.