Lema, Zitto, Mnyika, Mdee hawakamatiki

 

Mh. Godbless Lema (kati) kwenye moja ya harakati zake Bungeni

Wabunge vijana kupitia Chama Cha Demokrasia Maendeleo (Chadema), wameibuka washindi wa tuzo ya wabunge bora vijana kwa mwaka 2011.

Tuzo hiyo inayojulikana kama “Mjengwablog Young Leaders Award,” ambayo kuanzia mwakani itakuwa inatolewa kila mwaka.

Shindano la kuwapata wabunge hao liliendeshwa na Blog ya Maggid Mjengwa kwa majuma kadhaa ambapo wadau mbalimbali walipata fursa ya kuwapigia kura wabunge mbalimbali vijana kwa ajili ya kupata washindi.
 
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbess Lema, aliibuka mshindi wa kuwa mbunge bora kijana kwa mwaka 2011 kwa kupata kura 4310 (asilimia 50) kati ya kura 8,576 zilizopigwa.

Lema aliibuka mshindi katika kundi la wanaume, huku kundi la wananwake mshindi wake akiwa ni Halima Mdee (Kawe-Chadema), aliyepata kura 395 kati kura 514 (asilimia 72) ya kura zilizopigwa na washiriki.

Mshindi wa pili katika kundi a wanaume ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, aliyepata kura 3074 (asilimia 35) huku Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, akipata kura 776 (asilimia tisa)

Kwa upande wa kundi la wanawake, Regia Mtema Viti Maalum (Chadema), aliibuka mshindi wa pili kwa kupata kura 32 (asilimia tano) na Esther Bulaya kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) alishika nafasi ya tatu kwa kuibuka na kura 21 (asilimia tatu).

Kwa mujibu wa Blog ya Mjengwa ambayo ilisimamia zoezi hilo, utaratibu wa kukabidhi tuzo na zawadi kwa washindi unaandaliwa.

Tuzo hizo zinatarajia kutolewa kwa washindi katika tarehe itakayopangwa Februari mwakani.

Aidha, utaratibu unaandaliwa kuwezesha tuzo hizo kutolewa sambamba na kufanyika mjadala wa vijana juu ya masuala muhimu ya kitaifa yenye kuvuka mipaka ya vyama.

Mjadala huo utashirikisha washindi, walioshiriki mchakato katika hatua ya fainali, wanaharakati vijana na wanasiasa vijana.

Wengine ni marais wa jumuiya za wanafunzi wa vyuo vikuu, wanahabari, waandishi na wachambuzi wa makala za magazetini na wageni waalikwa.

Katika mjadala huo, kutakuwa na mada fupi zitakazowasilishwa na washindi wa kwanza wa tuzo ambapo wataziwasilisha kwa muda wa dakika 15 kwa kila mshindi wa kwanza toka kwenye kundi lake.

Aidha, washindi wa tuzo watapata fursa ya kujibu maswali kadhaa kutoka kwa washiriki na pia kuruhusu mjadala mpana.

Madhumuni ya tuzo hizo ni kuhamasisha ushiriki wa vijana kwenye masuala ya uongozi wa siasa.

Kupitia tuzo hizo vijana wataweza kuhamasishwa na kuunganishwa katika kushiriki, kujenga na kuimarisha misingi ya kidemokrasia.

Imeelezwa kuwa tuzo hizo zitawahamisisha vijana washiriki kujenga mustakabali wa nchi yao bila kujali tofauti zao za kiitikadi, kidini, kikabila, kimaeneo na hata rangi.

Kuanzia mwakani, tuzo hiyo itashirikisha kundi la wanaharakati, vijana na wanasiasa vijana wanaochipukia.

Baadhi ya wanasiasa vijana waliopigiwa kura katika kinyang’anyiro hicho ni Mbunge wa Bumbuli (CCM), January Makamba; mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) na Mbunge wa Muhambwe (NCCR-Mageuzi) Felix Mkosamali. Wengine ni Mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi na Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohammed Dewji.

CHANZO: NIPASHE