Laurent Gbagbo afikishwa mahakamani

Aliyekuwa Rais wa Ivory Coast, Laurent Gbagbo akiwa chini ya ulinzi.

RAIS aliyeondolewa madarakani nchini Ivory Coast, Laurent Gbagbo amefikishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC).

Laurent Gbagbo anakuwa ni rais wa kwanza kukabiliwa na mashtaka katika mahakama hiyo, huku akiwa ameshtakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu kwa kuhusishwa na umwagikaji damu uliotokea baada ya uchaguzi wenye utata mwaka jana. Gbagbo alipelekewa nchini Uholanzi wiki iliyopita.

Kiongozi huyo atasomewa makosa yake chini ya sheria za mkataba wa Roma uliounda mahakama hiyo. Baada ya kusomewa mashtaka yake itakuwa jukumu la majaji waandamizi kuamua siku ya kusikiliwa kwa kesi dhidi ya Laurent Gbagbo.

Wafuasi wa Gbagbo nchini Ivory Coast wamesema hatua ya kumkamata mwanasiasa huyo ni kama utekaji nyara wa kisiasa na kuonya hatua ya kumfungulia mashtaka inahujumu mpango wa maridhiano ya kitaifa.

Hata hivyo mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya ICC anayeondoka Luis Moreno- Ocampo amekanusha kauli hiyo na kusema kuna ushahidi tosha kumfungulia kiongozi huyo mashkata ya uhalifu wa kivita na siyo shinikizo za kisiasa. Mahakama ya ICC ilianzishwa mwaka 2002. Hii ndiyo kesi ya kwanza kubwa kusikilizwa katika mahakama hiyo.

Baadhi ya wadadisi wameona kama ushindi kwa mahakama hiyo huku baadhi nao wakiendelea kulalalamikia utaratibu wake hususan katika utekelezwaji wa kesi. Kuna wengine ambao wamelalamikia mahakama hiyo kwa kuwalenga viongozi na wanasiasa wa bara la Afrika pekee na kufungia macho mataifa mengine hasa ya magharibi.

-BBC