Kuziona Stars na Malawi sh. 5,000, U15 Tanzania Yafanya Kweli AYG

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura.

Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura.

TAIFA Stars na Malawi (Flames) zinapambana kesho (Mei 27 mwaka huu) katika mechi ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni.
 
Malawi tayari ipo jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mechi hiyo wakati Taifa Stars iliyopiga kambi yake Tukuyu mkoani Mbeya inawasili jijini Dar es Salaam kesho (Mei 27 mwaka huu) saa 4 asubuhi kwa ndege ya Air Tanzania.
 
Kiingilio katika mechi hiyo kitakuwa sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya chungwa, bluu na kijani. Kwa upande wa VIP B na C kiingilio kitakuwa sh. 10,000 wakati kwa VIP A itakuwa ni sh. 20,000.
 
Hiyo itakuwa ni mechi ya mwisho ya majaribio kwa Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager kabla ya kwenda jijini Harare kwa ajili ya mechi ya marudiano ya michuano ya Afrika dhidi ya Zimbabwe (Mighty Warriors). Malawi (Flames) inayonolewa na mchezaji wake wa zamani Young Chidmozi nayo itakuwa inacheza mechi ya mwisho ya majaribio kabla ya kwenda N’djamena kuikabili Chad.
 
U15 TANZANIA NG’ARING’ARI AYG
Tanzania imeendelea kung’ang’ara kwenye Michezo ya Afrika kwa Vijana (AYG) kwa upande wa mpira wa miguu kwa vijana wenye umri chini ya miaka 15 baada ya jana (Mei 25 mwaka huu) kuichapa Swaziland mabao 3-0.
 
Mabao ya Tanzania katika mechi hiyo iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Gaborone, Botswana yalifungwa na Amani Ally dakika ya sita, Nasson Chanuka dakika ya 32 wakati Amos Kennedy alikamilisha ushindi huo kwa bao la dakika ya 53.
 
Katika mechi yake ya kwanza, Tanzania ilitoka sare ya bao 1-1 na Mali na baadaye kuwafunga wenyeji Botswana mabao 2-0. Mechi za michuano hiyo zinaoneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha SuperSport cha Afrika Kusini. Tanzania itacheza mechi yake ya nne kesho (Mei 27 mwaka huu) dhidi ya Nigeria wakati mechi ya mwisho itafanyika Mei 29 mwaka huu dhidi ya Afrika Kusini.
 
KOZI ZA UKOCHA LESENI A, B KUFANYIKA JUNI
Kocha a ukocha wa mpira wa miguu kwa ajili ya Leseni A na B zinazotambuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF)  zitafanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Juni 2 mwaka huu.
 
Ada kwa kozi ya Leseni A itakayoanza Julai 21 hadi 26 mwaka huu ni sh. 300,000 wakati ile ya Leseni B itakayofanyika kuanzia Juni 2 hadi 15 mwaka huu ni sh. 200,000. Maombi ya kushiriki kozi hizo yatumwe kwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wakati kwa upande wa Zanzibar yatumwe kwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFA) kabla ya Mei 31 mwaka huu.
 
Washiriki ambao watajitegemea kwa chakula watalipa ada hizo wakati wa usajili utakaofanyika Juni 1 mwaka huu kwa upande wa Leseni B na Leseni A watalipa Julai 20 mwaka huu vilevile wakati wa usajili.
 
TFF itatoa malazi kwa washiriki kwenye hoteli yake iliyopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume wakati wakufunzi wa kozi hizo ni Sunday Kayuni na Salum Madadi ambao wanatambuliwa na CAF. Pia CAF baadaye itatuma Mkufunzi atakayetunga na kusimamia mitihani hiyo.