KUZALIWA SUDAN KUSINI: Ni furaha, kilio kwa Afrika?

Marais Salva Kiir wa Sudan Kusini na mwenzie wa Sudan ya Kaskazini, Omar Al-Bashir wakipungia wananchi katika sherehe za uzinduzi wa Taifa Jipya la Sudan Kusini

 

*Taifa moja lagawanyika katikati ya ndoto za Afrika Moja
*Kuendekeza udini, ukabila vyachochea mgawanyiko wake
*Kuwa mwanachama mpya Jumuiya ya Afrika Mashariki

JUBA, Sudan Kusini

MAELFU ya raia wa Sudan Kusini jana walitokwa na machozi waliposhuhudia kupandishwa kwa bendera ya taifa lao jipya katika sherehe za uhuru zilizofanyika katika Jiji la Juba, katika tukio ambalo wachunguzi wa mambo wanasema linaiachia Afrika swali muhimu.
Rais Salva Kiir alisaini katiba ya taifa hilo la 193 kutambuliwa na Umoja wa Mataifa likiwa pia la 56 kwa Afrika, huku akila kiapo cha urais mbele ya umati uliohusisha viongozi wengine kadhaa wa duniani.
Waliokuwapo ni pamoja na Rais wa Sudan, Omar al-Bashir, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ametajwa kuwa huko kushuhudia tukio hilo.
Kuzaliwa kwa Sudan Kusini kunatajwa kuhitimisha uhasama wa muda mrefu baina ya pande za Kusini na Kusini za iliyokwa Sudan moja iliyopata uhuru mwaka 1956 kutoka Uingereza.
‘Bahari’ ya watu iliujaza Uwanja wa Uhuru jijini Juba, karibu na makumbusho ya marehemu John Garang, kiongozi wa waasi aliowaongoza Wasudan Kusini katika vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Kundi la viongozi wa dunia lilitoa hutoba kwenye jukwaa kuu lakini sherehe za kina zilikuwa kwenye umati wa watu waliopagawa kwa kucheza ngoma.
Rais Kiir baada ya kupandishwa bendera ya Sudan Kusini, alikataa kuikabidhi ile ya Jamhuri ya Sudan, katika kilichosemwa itatunzwa makumbusho kwa ajili ya kuweka historia sawa.
Rais wa Sudan, Al-Bashir, katika hotuba yake aliwapongeza ndugu zao hao kwa kufanikiwa kuunda taifa jipya.

SWALI KWA AFRIKA
Wachunguzi wa mambo wanasema licha ya tukio hilo kubeba picha ya furaha, lakini ni pigo kwa ndoto waliyokuwa nayo baadhi ya viongozi magwiji wa Afrika kama Kwame Nkurumah na Julius Nyerere ya kutaka siku moja Afrika iwe taifa moja lenye nguvu.
Wakati Umoja wa Afrika ukiwa bado unahangaikia kuleta umoja huo, mmoja wa wanachama wake Jamhuri ya Sudan imefika hatua sasa imegawanyika.
Hivyo wachunguzi wa mambo wanauliza, Afrika ifurahie, au ilie kwa Sudan kugawanyika?

SABABU ZA MGAWANYIKO
Matatizo mengi yaliyokuza uhasama wa pande hizo za Sudan hadi kuzusha vita ya wenyewe kwa wenyewe inayotajwa kuua watu karibuni milioni 1.5, yanaonekana pia kuzikabili hata nyingine nyingi za Afrika.
Mathalani Tanzania iliyozaliwa baada ya muunganiko baina ya Tanganyika na Zanzibar, kwa miaka kadhaa sasa muungano wake umekuwa ukitikiswa kwa hoja zinazoibua maswali mengi kuliko majibu.

Tofauti za Uchumi
Wasudan wamegawanyika kwa matatizo ya tofauti za kiuchumi na mgawanyo wa rasilimali hasa mafuta. Na katika tofauti ya suala hilo, hadi Sudan Kusini inatawazwa kuwa huru jana, bado iko katika mgogoro na Kaskazini katika suala la mpaka, kwani pande hizo zinagombea jimbo la Abyei, moja ya maeneo yenye utajiri mkubwa wa mafuta.
Suala la kutopatikana mwafaka sahihi kuhusiana na mpaka mpya baina ya Kusini na Kaskazini, bado linaacha wasiwasi wa mzozo mwingine.
Waziri wa Masuala ya Rais wa Jamhuri ya Sudan, Bakri Hassan Saleh, ametangaza kuwa wanaitambua Sudan Kusini kuwa ni taifa huru kwa mipaka iliyowekwa tangu Januari Mosi, 1956 wakati Sudan ilipopata Uhuru kutoka Uingereza.
Suala la mipaka hivi karibuni lilizua mapigano katika maeneo mawili ya mpakani, Abyei na Kordofan Kusini, ambako watu 170,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Matatizo ya Umasikini
Sudan Kusini pamoja na utajiri mkubwa wa mafuta ilionao, lakini pia ni miongoni kwa mataifa masikini katika kundi la nchi zinazoendelea.
Inakadiriwa mtoto mmoja kati ya saba hufariki kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano.
Pia watoto wengi walio chini ya umri wa miaka 13 bado hawajaandikishwa shule na inasemwa asilimia 84 ya wanawake wake hawana elimu kabisa.

Matatizo ya udini
Wakati sehemu kubwa ya watu wa Sudan Kaskazini wakiwa wafuasi wa imani ya Kiislamu, taifa jipya la Sudan Kusini lenye watu kati ya milioni 7.5 hadi milioni 9.7, linaundwa na wakristo zaidi huku kukiwapo na wachache wanaoshiriki dini za jadi.
Tofauti zao za dini kwa namna moja ama nyingine zilichangia uhasama wao na Kaskazini.

Changamoto za Sudan Kusini
Kwanza inakabiliwa na changamoto kubwa ya kugawana madeni na mfumo wa biashara ya mafuta na Kaskazini, jambo ambalo inaelezwa linaweza kuziingiza pande hizo katika uhasama mpya.
Pia Sudan Kusini inakabiliwa na changamoto ya usalama wa ndani. Inatajwa kuwa na makundi yasiyopungua saba ya uasi ambayo huenda yakaisumbua serikali ya Kiir.

Ushirikiano na Kaskazini
Wakati jana Sudan Kusini kulikuwa hakukaliki kwa furaha, mjini Khartoum, makao makuu ya Kaskazini kwa watu wengi ilikuwa siku ya kawaida wakiendelea na shughuli zao, ingawa kuna baadhi walikusanyika wakibeba bendera za Sudan na kupiga kelele: “Allahu Akbar (Mungu ni Mkubwa).

Mwanachama mpya Jumuiya ya Afrika Mashariki
Kwa uwepo wake wa kijiografia, Sudan Kusini, inapewa nafasi kubwa ya kuwa mwanachama wa sita wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, itakapoungana na Tanzania, Kenya, Uganda (waasisi wa jumuiya hiyo) pamoja na nchi za Rwanda na Burundi zilizojiunga baadaye.

Source: Mtanzania