Kutokana na Kukithiri kwa ukatili Mkoa wa Mara waanza mafuzo ya wasaidizi wa kisheria

Na Mwandishi wetu
Musoma,
BAADA ya kuelezwa kuwa Mkoa wa Mara unaongoza kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia kutokana na tafiti ziliozofanywa,Shirika la kutetea haki za Wanawake na Watoto la( ABC Foundation) kwa kushirikiana na Taasisi ya elimu ya watu wazima (TEWW) wameanzisha mafunzo ya wasaidizi wa kisheria (Training in Paralegal Skills) ili kuweza kutoa elimu ya kisheria na madhara ya ukatili.

Akizungumza ofisini kwake,Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Eustuce Nyarugenda alisema kutokana na kulipotiwa mara kwa mara kwa vitendo vya ukatili katika ofisi yake wameamua kuanzisha mafunzo hayo kwa kushirikiana na Taasisi yua elimu ya watu wazima ili kuweza kuwafunza hususani vijana ili kupeleka elimu kwa jamii kwa kufuata vifungu vya sheria.

Alisema mafunzo hayo ya wasaidizi wa kisheria yatafundishwa kwa muda wa mwaka mmoja huku mada tofauti za kisheria ikiwemo ukatili kwa Wanawake,Watoto pamoja na ukatili mwingine wa majumbani ambapo wahitimu wa mafunzo hayo watatunukiwa cheti cha awali cha wasaidizi wa kisheria (Basic Certificate in Paralegal Skills).

Nyalugenda alisema mafunzo hayo yatawasaidia waliofaulu kuweza kutoa elimu kwa Wananchi juu ya athari za mbalimbali za ukatili wa klijinsia na maelekezo juu ya sheria inasema nini pale mtu anapopatikana na makosa ya ukatili wa kijinsia.

Aliongeza kuwa si vyema vitendo vya ukatili vikiendelea kulipotiwa hususani katika Mkoa wa Mara kisha jamii ikaendelea kukaa kimya na kushindwa kutafuta namna ambavyo hali hiyo inaweza kukomeshwa kwa kupitia kutoa elimu mbalimbali na mafunzo yatakayoweza kuzuia na kuondoa hali hiyo.

Aidha Nyalugenda alidai mafunzo hayo yatawahusu vijana waliohitimu kidato cha nne na kuendelea na kueleza kuwa kwa wale wataohitaji kujiunga na mafunzo kwa ajili ya kushiriki na jamii katika kupambana na masuala ya ukatili wa kijinsia wafike katika ofisi za Taasisi ya elimu ya watu wazima Mkoani Mara.

K wa upande wake Mkufunzi mkazi wa Taasisi ya Elimu ya watu wazima Mkoani Mara,Ernesti Yohana alisema watakaofaulu mafunzo hayo watapata vyeti ambavyo vinatambulika Serikalini na kuwasaidia kujiendeleza baadae katika masuala ya Sheria.

Alidai kwa wale watakaofanya vizuri zaidi katika mafunzo hayo wataendelea na mafunzo mengine ya Sheria yanayotolewa na vituo vya Taasisi ya elimu ya watu wazima kwa kushirikiana na Chuo kikuu cha Dar es Salaam na kupata vyeti vya ngazi ya juu katika masuala ya usaidizi wa Sheria.

Tafiti zilizofanywa na watetezi wa Haki za Binadamu hapa Nchini zinaonyesha Mkoa wa Mara unaongoza kwa ukatili wa kijinsia ukiwa na asilimia 72 ukifuatiwa na Mkoa wa Dodoma wenye asilimia 71 huku Mkoa wa Tanga ukiwa wa Mwisho katika masuala ya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia.