Na Joachim Mushi
TAKRIBANI magari 24 ya watu binafsi jijini Dar es Salaam yameangukiwa na ukuta na kuharibika vibaya pamoja na baadhi yao kujeruhiwa. Tukio hilo limetokea leo asubuhi ndani ya Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani (Ubungo) kwenye eneo la kuegesha magari binafsi ya watu wanaofika Ubungo kwa shughuli anuai ikiwemo kusindikiza ndugu na jamaa zao.
Wakizungumza na mtandao huu baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo walisema magari hayo yameangukiwa na kuta za zege ndani ya eneo lililokuwa likibomolewa, ambalo hutumika kuegesha magari hayo siku zote. Mashuhuda hao walisema takribani watu watatu wamejeruhiwa katika ajali hiyo.
Akizungumzia ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa Maalumu wa Kinondoni, Charles Kenyela alisema wanalichukulia tukio hilo kama ajali zingine hivyo Jeshi la Polisi limeimarisha ulinzi wa mali zilizosalia eneo la ajali huku taratibu nyingine zikiendelea.
Jumla ya magari 24 pamoja na bajaj mbili zimekubwa na ajali hiyo huku magari 19 yakiwa yameharibika vibaya zaidi kutokana na kukandamizwa na kifusi cha kuta za zege zilizoanguka ghafla.
Meneja wa Kituo cha Ubungo hakuwa tayari kuzungumzia chochote kwa vyombo vya habari na juhudi zinafanywa na uongozi wa kituo hicho kuondoa kifusi cha nguzo za zege juu ya magari ili yaweze kuondolewa eneo hilo.
Thehabari.com imeshughudia baadhi ya wamiliki wa magari yaliokubwa na ajali hiyo wakiorodhesha majina yao tayari kwa utaratibu wa kuanza kudai haki zao, kwani walisikika wakisema wameelekezwa kuegesha eneo hilo licha ya uongozi wa kituo kujua kuwa zoezi la ubomoaji linaendelea.
Kuta zilizoangukia magari ni nguzo za zege ambazo zilikuwa zimesalia maada ya zoezi la bomoa bomoa kufanyika. Uchunguzi uliofanywa na mtandao unaonesha baadhi ya nguzo za zege zilizo dondoka zilikuwa zimeanza kugongwa chini kana kwamba zinabomolewa kama ilivyo kwa kuta nyingine za kawaida za jengo hilo.
Hadi mtandao huu unaondoka eneo la tukio wamiliki wa magari hayo walikuwa wakishauriana cha kufanya ilhali hakukuwa na kauli yoyote ya uongozi wa kituo hicho juu ya ajali hiyo.