Kupanda kwa bei tatizo kwa Wananchi-Dk Shein

”]

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

TATIZO kubwa linalosababisha wananchi kushindwa kupata mahitaji yao ya kila siku ni kutokana na kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali hasa zile za chakula mara kwa mara.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini hapa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, katika uzinduzi wa Baraza na Kamati za Uhakika wa Chakula na Lishe katika ngazi ya Taifa, Wilaya na Shehia, hafla iliyofanyika huko katika ukumbi wa Salama katika Hoteli ya Bwawani, mjini Zanzibar

Viongozi mbali mbali walihudhuria wakiwemo Mawaziri, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, Makatibu Wakuu, Wakurugenzi na viongozi wa Kamati hizo. Katika hotuba yake Dk. Shein alieleza kuwa ongezeko hilo linachangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa upatikanaji wa chakula hicho.

Alisema kuwa pamoja na matatizo mbali mbali yanayosababisha kupanda kwa bei ya chakula duniani ikiwemo gharama za usafirishaji, mizozoz katika nchi mbali mbali na sababu nyenginezo. Kutokana na hali hiyo, Dk. Shein alisisitiza kuwa si sahihi kwa baadhi ya wananchi kuona kuwa Zanzibar pekee ndio bei za bidhaa zimekuwa zikipanda mara kwa mara bali tatizo hilo ni la dunia nzima.

Alieleza kuwa katika muda huu ambapo demokrasia inazidi kuenea wananchi mijini na vijijini kila kukicha wanahitaji kufanya mambo mengi zaidi katika kujiletea maendeleo yao. “Masuala haya yote yanajumuishwa kwenye kasha moja, maarufu kwa jina la uhakika wa chakula na lishe,” alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa hizo ni changamoto ambazo viongozi katika taasisi na sekta mbali mbali wana wajibu wa kushirikiana na wananchi pamoja na wataalamu mbali mbali katika kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu na kueleza kuwa uzinduzi huo ni hatua muhimu katika kuzishajiisha taasisi kusimamia na kutoa muongozo juu ya utekelezaji wa masuala ya uhakika wa chakula na lishe.

“Lengo ni kuhakikisha kuwa nchi yetu inajihakikishia usalama wa chakula na lishe na inauwezo wa kukabiliana na hali tete ya upungufu wa chakula na janga la njaa kupitia utekelezaji thabiti wa kisera na kisheria.

Pamoja na hayo Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imejidhatiti katika kuitekeleza Sera hiyo inayoufanya umasikini kuwa agenda muhimu ya maendeleo.

Alisema kuwa Serikali inashughulikia masuala ya uhakika wa chakula na lishe kwa upana wake kwa kuzingatia fungamano la uhakika wa chakula na lishe na juhudi za kupunguza umasiki na kuharakisha maendeleo kama ilivyofafanuliwa katika MKUZA.

Kupitia Sera ya Uhakika wa Chakula na Lishe, Dk. Shein alisema kuwa Serikali itaendeleza juhudi zake katika kuhakikisha wananchi wanashirikishwa katika kuwafikishia huduma muhimu na za msingi ikiwa ni pamoja na kuwapatia haki ya kumiliki ardhi, kuwawezesha kuanzisha biashara ndogo ndogo, maji safi na salama, kuunga mkono miradi inayotegemea nguvu kazi na kuwapatia mikopo midogo midogo.

Dk. Shein alieleza kuwa haki ya chakula ilipitishwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1989 na kuridhiwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwaka 2002 ikiwa ni miongoni mwa nchi zinazotambua haki hiyo.

Alisema kimsingi haki ya chakula inasisitiza kwaamba chakula ni haki ya kila binaadamu hivyo basi makundi yaliyo kwenye hatari ya kupatwa na ukame au ukosefu wa chakula yanahitaji kipaumbele katika kuhakikisha kuwa wana uhakika wa chakula na lishe.

Sambamba na hayo, Dk. Shein alieleza kuwa katika kutekeleza agizo la Umoja wa Mataifa, Baraza la Wawakilishi limetunga Sheria ya Uhakika wa Chakula na Lishe namba 5 ya mwaka 2011, Sheria ambayo ameitia saini tarehe 6 Julai mwaka jana.

Akitoa neno la shukurani Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Idd ambaye pia, ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Uhakika wa Chakula na Lishe alisema kuwa kuna kila sababu ya kutekeleza majukumu kwa ufanisi mkubwa zadi kwa kuzingatia kuwa chakula na lishe ni lazima viende pamoja.

Mapema Waziri wa Kilimo na Maliasili, Suleiman Othman Nyanga alieleza kuwa kila Mzanzibari ana haki ya kupata chakula na lishe ikwia ni haki ya kuishi maisha salama na yenye afya njema. Pia, Waziri Nyanga alisisitiza mashirikiano ndani ya Kamati hizo ili ziweze kutekeleza kwa ufanisi majukumu yao.

Naye Mwakilishi Mkaazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Chakula Duniani Tanzania Bi Dianna Allen Tempelman, alieleza kuwa Shirika hilo litaendelea kuuunga mkono juhudi hizo za Zanzibar na kueleza kuwa hatua hiyo ni ukombozi katika suala zima la chakula na lishe nchini.