Kuondoka kwa Kalala Jr hakuiyumbishi Mapacha 3- Josee Mara

Pichani kati ni Mwanamuziki mahiri Josee Mara akifafanua kuhusiana na mikakati yao waliyonayo kwa sasa mara baada ya mwanamuziki mwenzao mmoja, Kalala Jr kutimka na kuwaacha wakiwa wawili badala ya watatu. Josee Mara amesema wao wako fiti na hakuna kilichoharibika, kwani kuna wanamuziki wengine kadhaa ambao ni wazuri na watafanya nao kazi kama ilivyokuwa kwa Kalala Jr. “Na sasa hivi nakuhakikishia Da’Suzzy tutapiga kazi ile mbaya, kwa sababu hao vijana tunaowaongeza ni wanamuziki wazuri na tunawafahamu toka kitambo, kwa hivyo naamini mambo yatakuwa sawa na washabiki wetu wasivunjike moyo, waendelee kutuunga mkono tu, sisi ni wapambanaji kwa hiyo ni lazima tupambane” amesema Josee Mara. Aidha Khalid Chokoraa ameongeza kuwa katika kuonesha bado wako fiti wamekwisharekodi singo   yao moja iitwayo ONA NAONEWA, ambayo wataitambulisha hivi karibuni kwa mashabiki wa muziki wa dansi.
Mmoja wa watangazaji wa Clouds FM, kupitia kipindi cha Wikend Bonanza, Da’ Suzzy akizungumza na wanamuziki mahiri wa dansi hapa nchini waliokuwa wakijiita Mapacha 3, ambapo kwa sasa mmoja wao Kalala Jr ameamua kuachia ngazi na kuwaacaha wenzake Khalid Chokoraa na Josee Mara kama uwaonavyo pichani wakiwa na Meneja wao Hamis Dacota pichani kulia. Da’Suzzy alikuwa akitaka kujua kwanini msanii mwenzao Kalala Jr ameamua kutimka kwenye bendi yao na kwamba wana mikakati gani ya kuliziba pengo la mwanamuziki huyo aliyetimka. Kwa mujibu wa Meneja wa bendi hiyo ya Mapacha 3, Hamis Dacota amebainisha kuwa Kalala Jr aliamua kuondoka mwenyewe bila kuwepo na ugomvi wowote baina yao, “hivyo kama mwanamuziki mwenzetu, kijana mwenzetu tunamtakia kila kheri huko aendako, lakini kama akitaka kurudi pia milango iko wazi anakaribishwa sana, kwa sababu yeye ni mmoja wa waasisi wa Bendi ya Mapacha 3”, alisema Dacota.