Kumekucha Kombe la Kagame, Azam FC Yaanza Vizuri

Baadhi ya wachezaji wa Azam FC

Baadhi ya wachezaji wa Azam FC

MICHUANO ya Kombe la Kagame inayoendelea kutimua vumbi katika viwanja viwili vya Taifa na Karume vilivyopo jijini Dar es salaam, itaendelea kesho kwa michezo miwili itayopigwa katika dimba la Uwanja wa Taifa.

Katika michezo iliyochezwa leo, Malakia ya Sudani Kusini iliibuka na ushindi wa mabao 2- 1 dhidi ya Adama City ya Ethiopia, LLB ya Burundi ikitoka sare ya bila kufungana na Heegan FC ya Somalia mchezo uliochezwa saa uwanja wa Karume, huku Azam FC wakiibuka na ushindi wa bao 1- 0 dhidi ya KCCA ya Uganda.

Vinara wa kundi A timu ya Gor Mahia kutoka nchini Kenya, kesho jumatatu watashuka dimbani kucheza na timu ya KMKM kutoka Visiwani Zanzibar ambayo pia jana iliibuka na ushindi katika mchezo wake wa awali dhidi ya Telecom.

Gor Mahia ambayo ilipata ushindi wa mabao 2- 1 katika mchezo wa kwanza dhidi ya Yanga, itakutana na KMKM ambayo iliibuka na ushindi wa bao 1 – 0 dhidi ya timu ya Telecom ya Djibout, mchezo utakaochezwa saa 10 jioni Uwanja wa Taifa.

Mchezo wa kwanza utazikutanisha timu za Telecom ya Djibout dhidi ya Khartoum-3 kutoka nchini Sudan, ambayo itakua ikicheza mchezo wake wa kwanza. Jumanne kutakua na michezo mitatu ambapo Al Shandy watacheza na LLB katika kundi B saa 8 mchana uwanja wa Taifa, Heegan FC dhidi ya APR uwanja wa Karume saa 10 jioni, Malakia dhidi ya Azam kundi C Uwanja wa Taifa saa 10 jioni.

Jumatano mabingwa mara tano wa michuano ya Cecafa Kagame Cup, timu ya Yanga SC watacheza dhidi ya Telecom ya Djibout saa 10 jioni uwanja wa Taifa, KCCA wakicheza na Adama City saa 10 jioni uwanja wa Karume, na Khartoum wakicheza mchezo wa awali saa 8 mchana uwanja wa Taifa dhidi ya KMKM.
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)