Kumbe Simu za Mkononi ni Hatari; Husababisha Watoto Kuzaliwa Watukutu

Simu za mkononi

MIONZI ya simu za mkononi inaweza kuathiri maendeleo ya ubongo wa watoto walioko tumboni mwa mama zao, utafiti umeeleza.Utafiti huo umetaja madhara mengine ya mionzi ya simu za mkononi kuwa ni uharibifu wa manii, mimba, kupungua kwa nguvu za kiume, kupoteza kumbukumbu na kuzaa watoto watukutu. Pia umeeleza kuwa matumizi kupita kiasi ya simu hizo, husababisha mtindio wa ubongo na upungufu wa udadisi kwa watoto tangu udogo wao.

Hata hivyo, utafiti huo uliofanywa na Shule ya Tiba na Dawa ya Chuo Kikuu cha Yale, Marekani na kuripotiwa na Gazeti la The Telegraph la Uingereza, umepingwa na watafiti wengine, wakisema haujakidhi baadhi ya vigezo ili kuuthibitisha. Kiongozi wa jopo la utafiti huo, Profesa Hugh Taylor alisema utafiti huo ulioanzia kwa panya, baadaye ulithibitika kwa binadamu.

Profesa Taylor ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Uzazi, Magonjwa ya Wanawake na Sayansi ya Uzazi, alisema: “Tulikuwa na panya wenye mimba katika maboksi na tuliwawekea simu juu ya vichwa vyao. Panya tuliokuwa tumewaweka katika bwawa lile, nusu yao walikuwa wazima na nusu yao walikufa. Panya waliokuwa hai tuliwaacha wajifungue na baada ya kujifungua, tukaanza kutafiti watoto wao.”
“Panya ambao hawakuwa karibu na simu za mikononi walionekana kuwa werevu. Kumbukumbu zao hazikupungua ikilinganishwa na panya walioathiriwa na mionzi ya simu za mikononi ambao katika vipimo vya awali wakiwa tumboni, walionekana kuhangaika.”

“Panya hao wenye mimba waliowekwa kwa siku 17 katika boksi hilo na simu kupigwa mfululizo juu ya vichwa vyao, walizaa watoto watukutu na waliokosa kumbukumbu.”
Aliongeza: “Matokeo hayo yanaweza kutokea kwa binadamu pia. Mjamzito anayetumia simu ya mkononi muda mwingi, anaweza pia kuzaa taahira.”

Utafiti huo umebaini kuwa kati ya asilimia tatu na saba ya watoto wenye umri wa kwenda shule, wana tatizo la utukutu linaloweza pia kuathiri maendeleo yao kitaaluma. Alisema kiwango hicho kimekuwa kikiongezeka kwa asilimia tatu kila mwaka tangu mwaka 1997. Profesa Taylor alisema anaamini kuwa simu za mikononi pia ni sababu ya baadhi ya watoto kukosa adabu na pengine kutokuwa makini katika mambo mbalimbali wanapokuwa watu wazima.

“Huu ni utafiti wa kwanza unaoonyesha ushahidi wa madhara ya mionzi ya simu za mkononi. Tumeonyesha kuwa matatizo ya tabia katika panya yalitokana na mionzi ya simu za mkononi waliyoipata wakiwa tumboni,” alisema Profesa Taylor na kuongeza:

“Kuongezeka kwa utovu wa nidhamu kwa watoto kunaweza kuwa sehemu ya madhara ya mionzi ya simu, ambazo mama zao walikuwa wakizitumia wakati wao wakiwa bado tumboni.”

Profesa Taylor alifanya utafiti huo kwa kuwachukua panya 33 wenye mimba na kuwaweka kwenye boksi lenye nyavu kisha kuweka simu juu yake. Simu hiyo ilikuwa ikiita mfululizo kwa siku 17. Pia aliwaweka panya wengine 33 katika mazingira ya aina hiyo lakini hakuweka simu juu ya boksi hilo.
“Zaidi ya watu 160 waliofanyiwa utafiti wa aina hiyo pia walionekana kuwa na tofauti za kitabia ambayo inaweza kuhusishwa na utafiti huo.

Hata hivyo, Profesa Taylor alisema kuna haja ya kuendelea kufanya utafiti zaidi ili kubaini sababu ya mionzi hiyo ya simu kuathiri watoto walio tumboni mwa mama zao na namna bora ya matumizi ya simu kwa wanawake wajawazito. Mtaalamu huyo anatarajia kuungana na wenzake akiwamo Dk Devra Davis, anayeongoza Shirika lisilo la Kiserikali la Mazingira na Afya la “Environmental Health Trust” kwa ajili ya utafiti zaidi kuhusu madhara ya simu.

Mwaka 2011, Shirika la Kimataifa la Afya Duniani linalojihusisha na uchunguzi wa kansa, lilidai kuwa mionzi ya simu inaweza kusababisha kansa na hivyo jopo hilo la madaktari linaendelea na utafiti zaidi.
Nchi nyingine duniani ikiwamo Ufaransa, ilipiga marufuku kwa kampuni za matangazo ya simu kwa watoto kutokana na hatari mbalimbali zinazoweza kuwatokea. Utafiti huo uliochapishwa katika Jarida la ‘Scientific Reports’ wiki iliyopita

Lengo la utafiti
Ongezeko la matatizo ya magonjwa wa mishipa ya fahamu, matatizo mbalimbali ya ubongo pamoja na magonjwa ya akili, ni mojawapo ya mambo yaliyochagiza kufanyika kwa utafiti huo. Dk Hugh alisema simu za mkononi hazina madhara kwa watu wazima kama inavyodaiwa na wengi, lakini ni vifaa vyenye kuleta athari kubwa kwa watoto walio tumboni.

“Matatizo yanayowapata watoto wa binadamu walio wengi hivi sasa ikiwa ni pamoja na magonjwa ya mtindio wa ubongo, mishipa ya fahamu inasababishwa na matumizi ya simu za mkononi kwa mama wajawazito pamoja na kukaa nazo jirani kwa muda mrefu.”

“Haijalishi mama anaongea na simu au la! Mionzi inapenya na kuleta madhara pia kusababisha kazi ya ukuaji wa mtoto katika ubongo kulegalega, wapo ambao wanalala na simu kitandani zikiwa zimewashwa… hii ni hatari zaidi labda iwe imezimwa,” anasema Dk Hugh.

Watalaamu Dar
Akizungumzia utafiti huo jana, Mkurugenzi wa Teknolojia ya Nyuklia wa Taasisi ya Mionzi Tanzania (Taec), alisema ni vigumu kuukosoa utafiti huo kwa sasa hadi hapo Shirika la Afya Duniani (WHO), litakapotoa tamko sahihi ingawa alisema mionzi ina athari kubwa kwa binadamu.

“Nilipata kusoma utafiti huo katika mitandao siku mbili zilizopita, ni utafiti ambao umewekwa wazi, kwa kweli hata mimi ulinishtua, lakini ni mapema kuzungumzia hilo kwa sasa. Kwani utafiti huo bado unakinzana kwa mambo mengi, licha ya kupingwa pia na baadhi ya wanasayansi.

“Nadhani ni muda mwafaka sasa kufanya uchunguzi kwa binadamu na si kutumia panya kama walivyofanya Chuo Kikuu cha Yale. Hata hivyo, jopo la madaktari pia wanatarajia kufanya kikao chao mapema wiki hii, labda tutapata maoni mapya.”

Alisema kwa kawaida mionzi ina madhara kwa binadamu, lakini bado kuna maswali mengi kwa wanasayansi duniani ambayo bado hayajapatiwa ufumbuzi, hivyo inawawia vigumu Taec kutoa ufafanuzi wowote kuhusu athari hizo.

Meneja wa Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Innocent Mungy alisema utafiti huo unaweza kuwa msaada mkubwa kwa nchi kama Tanzania ambayo hivi sasa ndiyo imechipukia katika matumizi ya simu za mkononi.

CHANZO: www.mwananchi.co.tz