Kulisuka upya Baraza la Mawaziri suluhisho la muda

JK akiwa na kikosi chake cha Mawaziri

Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi imemwelekeza Rais Jakaya Kikwete “kusuka upya” Baraza la Mawaziri, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi. Hayo hayakuwa matazamio ya wengi katika CCM, na jana yake Katibu Mwenezi Nape Nnauye alikuwa ametoa rai kuwa Baraza la Mawaziri lipewe muda kurekebisha matatizo yaliyopo.

Hata Rais Kikwete, akiwa anatokea Malawi kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Dk. Bingu wa Mutharika alitoa rai kama hiyo, kuwa ugomvi uliozuka bungeni ni ‘upepo mbaya’ ambao utapita – lakini makundi tofauti yakawa yanajiandaa kuandamana.

Jambo ambalo Kamati Kuu imezingatia ni kuwa madai ya wabunge kuhusu mawaziri yanaaminiwa na wananchi ‘mia kwa mia,’ na kujaribu kuwatetea mawaziri itagharimu chama kisiasa, hivyo inabidi Baraza la Mawaziri lisukwe upya. Ambacho hakikutolewa hadharani ni mapana na marefu ya kusuka huko, kwani kina hitajika tu la kuita Bunge kwa kikao cha dharura endapo Waziri Mkuu naye atabadilishwa, ili mteule mpya athibitishwe na Bunge ndipo aapishwe.

Kwa mazingira yaliyopo, hilo pia si la kuweka pembeni; hasa kama mabadiliko Baraza la Mawaziri ni ya kina inafaa aingie mtu mwenye mvuto tofauti.

Somo jingine ambalo inabidi lizingatiwe ni mfumo huu wa ubia wa Waziri Mkuu na Rais katika kuunda serikali, kuwa Rais na Waziri Mkuu aliyeapishwa wanakaa pamoja kuunda serikali, wakati ambapo mwajibika halisi wa Baraza la Mawaziri ni Rais.

Hali hiyo pia inamfanya Waziri Mkuu afanane na Rais badala ya msimamizi wa kazi alizoagiza Rais, halafu mawaziri wanajihisi wanalindwa kwani inabidi makubaliano kati ya Rais na Waziri Mkuu kabla waziri hajaguswa. Hapo pia unaweza kuwepo mwanya wa udhaifu kiasi fulani, kuwa mahusiano ya usawa kati ya Rais na Waziri Mkuu ‘yanachuruzika’ na kuwa usawa kati ya Waziri Mkuu na mawaziri, hivyo serikali yote inakuwa ‘haiambiliki.’

Yako maeneo mengine ya mabadiliko ya kanuni za Bunge yanayohitajiwa ili kupunguza vianzio vya mashindano na ‘kuchimbana,’ hata kama tuhuma zinazotajwa ni za kweli. Kwa mfano kama Waziri Ezekiel Maige amenunua nyumba kwa fedha taslimu dola laki saba, hilo kweli linafaa kufanyiwa kazi, lakini si la kulipua bungeni ila lingefikishwa kwanza katika Kamati ya Maadili ya Viongozi, likithibitishwa, Rais angechukua hatua bila kuulizwa swali bungeni.

Hivyo inahitajiwa kanuni za Bunge kurekebishwa kuondoa masuala ya maadili binafsi ya mawaziri, kwani yanatoa mwanya wa kuliyumbisha Bunge na taifa kwa jumla kwa madai ambayo hayajathibitishwa.

Hiyo ni pamoja na madai ya hongo za wawekezaji kwa mawaziri, au hata waziri mdogo kuandaliwa safari na wawekezaji bila kumjulisha waziri – swali ambalo Waziri Omar Nundu angefikisha kwenye vikao husika, na siyo ‘kutupiana madongo’ bungeni kama jinsi ilivyotokea.

Ni wazi kuwa kazi ambayo Rais Kikwete anayo siyo tu kusuka upya Baraza la Mawaziri bali pia kulipa meno; mambo mengi yanaendeshwa kienyeji na mashirika ya umma au mamlaka za kiserikali kwa faida yao, na mambo yakiharibika anayewajibika ni waziri.

Akasema Waziri Nundu kuwa aliambiwa ‘asiingie jikoni’ yeye akawaambia ‘ataingia hadi chooni,’ ambayo kwanza si lugha rasmi ya Bunge, na isitoshe inaonyesha udhaifu wa kanuni, kama Waziri akaishia ‘barazani’ halafu shirika lifanye litakavyo, au ana uwezo halisi wa kusimamia.

Pale waziri anapokuwa hana dhamana kamili, na watendaji wanajinufaisha, msemo wa Waingereza utafuatwa, unaosema ‘ikiwa huwezi kuwashinda, jiunge nao’ hivyo naye anageuka mamluki kama watendaji wake, kwani wote wameteuliwa na Rais.

Na ikiwa serikali itashindwa kabisa kuweka kanuni za uadilifu na zikafuatwa mradi ni mashirika ya umma, irudie sera ya ubinafsishaji, walipe mabilioni katika kodi, na siyo kuendekeza ubadhirifu, kuomba ruzuku na kuifukarisha nchi zaidi.

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI