WANANCHI wa mkoa wa kaskazini Unguja wamesema ni muhimu uongozi wa wilaya ya Kaskazini B, Unguja kuteua Masheha wanawake ili kudhibiti vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake na watoto (GBV) ambavyo vimeshamiri katika wilaya hiyo.
Utafiti wa kihabari uliofanywa na wanahabari huko Zanzibar unaoyesha kuwa Wilaya ya Kaskazini B, Unguja Shehia zote 29 za wilaya hiyo zinaongozwa na wanaume huku vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto vikiwa ni vingi zaidi.
Mwanaharakati wa mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto katika wilaya ya Kaskazini B, Rukia Khaidar Gulam wa Bubwini, amesema matukio 108 ya ukatili wa kijinsia ukiwepo ubakaji yaliyoripotiwa katika wilaya hiyo mwaka 2011.
Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa ripoti utafiti huo hivi karibuni Rukia alisema baadhi ya matukio hayo yangeweza kuzuilika endapo Shehia zingekuwa zinaongozwa na wanawake wenye uelewa kuhusu athari za ukatili na jinsi ya kuepusha vitendo hivyo.
Alisema zaidi ya kesi 61 zinazohusu ukatili dhidi ya wanawake na watoto zimeripotiwa mwaka huu 2012 katika wilaya ya Kaskazini B na kwamba hakuna jitihada madhubuti zinazofanywa na Masheha kudhibiti uovu huo.
Mama huyo amesema kuwa viongozi Wanawake wenye mwamko na upeo kuhusu masuala ya jinsia wangeweza kutoa kipaumbele kushughulikia kesi za udhalilishaji ambazo zimekuwa zikiathiri wakaazi wa wilaya hiyo hasa wanawake na watoto.
Bwana Shaabani Juma wa Kaskazini A alisema kwa kauli kuwa wanawake hawawezi kufanya vizuri wanapopewa nafasi za uongozi zinatolewa na watu wasiothamini nafasi ya wanawake na ambao wana lengo la kuzorotesha maendeleo ya kundi hilo muhimu katika nchi.
Alitoa mfano wa Sheha wa Shehia ya Pitanazako, Acheni Machano Juma katika wilaya ya kaskazini A ambaye amesema anafanyakazi nzuri hasa ya kufuatilia matukio ya ukatili dhidi ya wanawake na watoto na kuhakikisha kuwa sheria inachukua mkondo wake.
Utafiti huo umebainisha kuwa wakati wilaya hiyo ya Kaskazini B, katika mkoa wa kaskazini Unguja ikiwa haina kabisa Sheha mwanamke, wilaya tisa za wilaya hiyo zilizobakia Masheha wanawake ni asilimia kati ya 3 hadi 19.
Mikataba ya kimataifa kuhusu haki za wanawake na watoto ambayo Tanzania imeridhia inaelekeza nchi kuhakikisha kuwa idadi sawa ya viongozi kati ya wanawake na wanaume.