KUKAMATWA MBOWE; UPINZANI WATOA KAULI NZITO

 

Kiongozi Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

AMRI YA KUMKAMATA KIONGOZI WA KAMBI RASMI YA UPINZANI YAINGILIA UHURUWA BUNGE, YAHATARISHA DEMOKRASIA!!!

 Dar es Salaam, Juni 3, 2011:

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imepokea kwa mshtuko, masikitiko na mshangao mkubwa taarifa za Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha kutoa amri ya kumkamata Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe.

 Mheshimiwa Mbowe pamoja na Wabunge, viongozi na wanachama kadhaa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wanakabiliwa na mashtaka kadhaa yanayotokana na maandamano tarehe 5 Januari 2011 katika Jiji la Arusha yaliyopelekea Jeshi la Polisi kuua wananchi watatu na kujeruhi wengine wengi. Taarifa zinaonyesha kwamba amri hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, Mheshimiwa Charles Magessa, siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Mei 2011 na kurudiwa tena jana, yaani tarehe 2 Juni 2011.

 Mheshimiwa Mbowe hakuhudhuria mahakamani katika tarehe zote mbili kwa vile amekuwa akihudhuria vikao vya Kamati mbali mbali za Bunge vilivyoanza tarehe 23 Mei 2011 na ambavyo vinaendelea hadi hivi sasa kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano wa Nne wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaotazamiwa kuanza tarehe 7 Juni hadi tarehe 7 Septemba 2011. Kama Mbunge na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Mbowe ni mjumbe wa Kamati mbali mbali za Bungekama vile Kamati ya Uongozi, Kamati ya Kanuni za Bunge na Kamati ya Fedha na Uchumi. Aidha, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ni mjumbe katika Tume ya Utumishi wa Bunge na ndiye msemaji mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

 Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshtushwa na amri ya kumkamata Mheshimiwa Mbowe kwa vile inakiuka moja kwa moja sheria, mila nadesturi za miaka mingi zinazohusu kinga, haki na mamlaka ya Bunge na ambazo ndio msingi mkuu wa demokrasia yetu ya kibunge. Ibara ya 100 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inatambua na kulinda “uhuru wa mawazo, majadiliano na utaratibu katika Bunge na uhuru huo hautavunjwa wala kuhojiwa na chombo chochote katika Jamhuri ya Muungano, au katika Mahakama au mahali penginepo nje ya Bunge.”Uhuru huu wa kikatiba umetiliwa mkazo katika vifungu vya 5, 6 na 11 vya Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge ya mwaka 1988 vinavyokataza Mbunge kukamatwa au kupewa amri ya kuhudhuria mahakamani wakati akiwa ndani ya eneo la Bunge au wakati Bunge limekutana bila kuwepo kwa kibali cha Spika.

 Maneno ‘eneo la Bunge’ limetafsiriwa na kifungu cha 2 cha Sheria hiyo kumaanisha “ukumbi ambao hutumiwa kwa vikao vya Bunge, pamoja na ofisi, vyumba, vibambaza (lobbies), maeneo ya wageni (galleries), courtyards, bustani na maeneo mengine yaliyowekwa kwa ajili ya matumizi au malazi ya wajumbe, maafisa au wageni wa Bunge pamoja na njia zinazounganisha maeneo hayo na maeneo mengine yanayoweza kutangazwa na Spika kuwa ndani ya maeneo ya Bunge.” Kwa maana hiyo, Mbunge anapokuwa anahudhuria vikao vya Bunge au Kamati zake au anapokuwa mahali pengine popote kwa kuitikia wito wa kuhudhuria vikao hivyo vya Bunge hawezi akakamatwa ili kutekeleza amri ya Mahakama au ya chombo kingine chochote nje ya Bunge.

Kufuatana na mila na desturi za kibunge za Jumuia ya Madola ambazo nchi yetu imezikubali na inatakiwa kuzifuata, kinga ya Wabunge dhidi ya kukamatwa inakuwa na nguvu wakati wa mkutano wa Bunge pamoja na muda muafaka na wa kutosha’ kabla na baada ya mkutano wa Bunge. Kwa mujibu wa Erskine May, mwandishi maarufu wa mila na desturi za mabunge ya Jumuia ya Madola, “muda muafaka na wa kutosha umechukuliwa kwa ujumla kuwa ni siku arobaini kabla na baada ya mkutano wa Bunge.”

Kwa mantiki hiyo, wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Arusha inatoa amri dhidi yake, Mheshimiwa Mbowe alikuwa analindwa na kinga ya Bunge.Aidha, Mheshimiwa Mbowe ataendelea kulindwa na kinga hiyo kwa kipindi chote cha Mkutano wa Nne wa Bunge la Jamhuri ya Muungano pamoja na ‘muda muafaka na wa kutosha’ – kama unavyotambuliwa katika mila na desturi za Mabunge ya Jumuia ya Madola – utakapokwisha baada ya Mkutano huo!

Kwa upande mwingine, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeshangazwa na unafiki na ubaguzi wa wazi unaoonyeshwa na Jeshi la Polisi juu ya Wabunge wa vyama vya upinzani. Hii ni kwa sababu wakati Jeshi la Polisi limekuwa likiwakamata Wabunge wa Upinzani bila kuomba kibali chochote cha Spika kama inavyotakiwa na Sheria ya Kinga, Mamlaka na Haki za Bunge – kama ilivyotokea kwa Wabunge wa CHADEMA Waheshimiwa Mbowe, Godbless Lema (Arusha Mjini), Phillemon Ndesamburo (MoshiMjini), Joseph Selasini (Rombo), Meshack Opulukwa (Meatu), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Esther Matiko (Viti Maalum, CHADEMA) na Magdalena Sakaya (Viti Maalum, CUF), wabunge wa CCM – na ambao wanakabiliwa na tuhuma za makosa makubwa zaidi – wamekuwa wanaombewa kibali cha Spika kabla ya kukamatwa.

Kwa hili, tuna ushahidi wa barua ya Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Mwanza SP B.M. Wakulyamba kwa Katibu wa Bunge ya kumwomba Mheshimiwa Titus Mlengeya Kamani (Busega, CCM) ili akahojiwe na Jeshi la Polisi kuhusu kuhusika kwake na njama za kutaka kumwuua aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Busega Dk. Raphael Masunga Chegeni. Barua hiyo ya tarehe 31 Mei 2011 ilinakiliwa kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mwanza na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai, Makao Makuu ya Polisi DCI Robert Manumba. Hakuna Mbunge hata mmoja wa CHADEMA au chama kingine cha upinzani ambaye – kwa taarifa zetu – amewahi kuombewa kibali cha kukamatwa na Polisi kama inavyoonekana kwa Wabunge wa CCM. Hii inadhirihisha upendeleo wa wazi wa Jeshi la Polisi kwa Wabunge wa CCM

Kwa sababu hizo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni haitarajii, naitapinga kwa nguvu zake zote, kitendo chochote cha kumtishia au kumkamata Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Aikaeli Mbowe kwa kipindi chote ambacho ana kinga ya Bunge kama inavyotambuliwa na Katiba na sheria zetu pamoja na mila na desturi za kibunge ambazo tumechagua kuzifuata kwa hiari yetu wenyewe.

 Aidha, tunatarajia Mahakama pamoja na vyombo vingine vyote vilivyoanzishwa na vinavyofanya kazi zake kwa mujibu wa sheria za nchi yetu vitatumia busara ili kuiepusha nchi yetu na fedheha ya kuonekana inakamata Wabunge wake wakati wakiwa wanatekeleza wajibu wao wa kibunge!

 ————————————

Tundu A. M. Lissu (MB.)

Mnadhimu Mkuu

KAMBI RASMI YA UPINZANI BUNGENI