Kufanya Mapinduzi ya Kilimo ni dhamira ya SMZ- Dk. Shein

Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Zanzibar

MAPINDUZI ya kilimo ndio mwelekeo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Saba yenye nia ya kutekeleza kwa vitendo dhamira ya kumkomboa mkulima wa Zanzibar kutoka kilimo duni na kumjengea fursa ya kupata tija na uhakika wa chakula.

Uongozi wa Wizara ya Kilimo na Maliasili iliyasema hayo katika kikao maalum na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein katika muendelezo wa kukutana na Wizara zote za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kuangalia mpango kazi wa Wizara na uhusiano wa Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUZA) na Dira ya 2020.

Ikielezea mikakati iliyojiwekea Wizara hiyo, ikiwemo ile ya robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2011/2012, ukiongozwa na Kaimu wa Waziri, Ramadhani Abdalla Shaaban, uliweka bayana malengo ya Dira ya 2020, mwongozo wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2010- 2015, MKUZA II, na Mipango wa Mageuzi ya Sekta ya Kilimo (ATI).

Uongozi huo ulieleza kuwa katika kipindi cha 2011/12 Wizara itatekeleza dhamira ya Mapinduzi ya Kilimo na kutoa mchango zaidi wa kukuza uchumi wa taifa sambamba na kupunguza umasikini. Miongoni mwa mikakati iliyowekwa ni kuimarisha miundombinu ya umwagiliaji na kuhamasisha uvunaji wa maji ya mvua kwa matumizi fasaha.

Uongozi huo pia ulieleza lengo la kuimarisha miundombinu ya masoko kwenye kilimo, kuongeza thamani ya bidhaa za kilimo na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha vijijini na kuimarisha huduma za wakulima na wafugaji.

Aidha, ulieleza lengo la kutoa huduma za kilimo cha matrekta na huduma za pembejeo kwa wakulima, zikiwemo mbolea, dawa ya magugu, mbegu bora pamoja na huduma za udhibiti magonjwa kwenye mimea na ukaguzi wa mazao. Kwa upande wa kuimarisha zao la karafuu Wizara imepanga kuotesha miche 500,000 ya zao hilo pamoja na kutoa elimu kwa wakulima.

Wizara hiyo ilieleza lengo la kuendeleza misitu ya jamii na kushajiisha matumizi ya gesi ya kupikia, kuzalisha miche ya misitu na kuvuna mazao yake, uendelezaji wa hifadhi pamoja na kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na makaa kwa kutumia nishati mbadala.

Uongozi huo pia, ulieleza mpango wa kuimarisha chuo cha Kilimo kilichopo Kizimbani ili kupata wataalamu wa kilimo na kuwajengea uwezo. Ulisema kuna mchakato wa mradi wa ‘Feed the future’ unaoendelea chini ya Serikali ya Marekani, ambao unahusisha zaidi suala la kilimo cha umwagiliaji maji, kuimarisha mazao na usarifu wa mazao, sera na utafiti.

Wakati huo huo Dk. Shein alifanya mkutano na uongozi wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi ukiongozwa na Waziri wake Mhe.Said Ali Mbarouk ambayo ilieleza Mpango Kazi wake kwa mwaka 2011/2012 ikiwa ni pamoja na kueleza matumaini ya wananchi wa Zanzibar kwa kuanzishwa wka Wizara hiyo mpya ambayo itasaidia sekta ya mifugo na uvuvi.

Wizara ilieleza kuwa katika mwaka wake huu wa fedha imekusudia kuanzisha Baraza la Utafiti wa Mifugo ambapo tayari imeshafanya mazungumzo na taasisi ya COSTECH ambayo imeahidi kutoa mafunzo juu ya kutayarisha mapendekezo ya tafiti.

Aidha, uongozi huo ulieleza kuwa katika kuiimarisha sekta ya uvuvi tayari Wizara imeshafanya mazungumzo na wawekezaji mbali mbali kwa lengo la kuekeza katika sekta ya uvuvi wa bahari kuu.Wizara pia, imeeleza lengo lake la kuimarisha huduma za ugani ili iwafikie walengwa wote katika sekta ya mifugo na uvuvi na kukuza huduma za uzalishaji wa mifugo.

Pia, Wizara ilieleza lengo lake la kufanya mapitio ya sera, sheria, kanuni, mipango na mikakati endelevu ya uvuvi na uzalishaji wa mifugo kwa ajili ya manufaa ya wananchi bila ya kuathiri mazingira.

Sambamba na hayo, Wizara ilieleza azma yake ya kudhibiti uvuvi haramu na kuimarisha ulinzi wa rasilimali kwa kuweka doria ikishirikiana na wananchi ikiwa na lengo pia, la kuongeza uzalishaji wa samaki.

Kwa upande wake Dk. Shein alitoa pongezi kwa watendaji hao wa Wizara waliofanya vikao hivyo kwa nyakati tofauti na kueleza kuwa anamatumaini makubwa ya kupata mafanikio katika uendeshaji Wizara hizo sambamba na kufikia malengo na mikakati hiyo waliyojiwekea.
Aidha, alieleza umuhimu wa kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha sanjari na elimu kwa wananchi juu ya lishe bora pamoja na kueleza azma ya serikali katika kuziendeleza sekta za uvuvi, mifugo, kilimo na maliasi ili ziweze kueleta faida kwa nchi na wananchi wake.