Kocha Mkuu Stars Kutimuliwa, Apewa Mtihani wa Mwisho…!

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Mart Nooij

Kocha Mkuu wa timu ya Taifa, Mart Nooij


KAMATI ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) imesikitishwa na mwenendo mbovu wa Taifa Stars, hivyo kumpa mtihani wa mwisho kocha mkuu wa timu ya Taifa, Mart Nooij na endapo atashindwa atafukuzwa kazi.

Kwa mujibu wa taarifa ya kamati hiyo mtihani aliopewa kocha Mart Nooij ni kuhakikisha anafuzu kwa fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) na asipofanikisha jambo hilo mkataba wake wa kazi kuifundisha timu hiyo utasitishwa mara moja.

“…Baada ya majadiliano ya kina, ilikubaliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya Taifa, Mart Nooij apewe changamoto maalumu ya kufuzu kwa fainali za Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN na asipofanikisha jambo hilo mkataba wake utasitishwa mara moja,” ilisema taarifa ya TFF.

Maamuzi haya yamezingatia hali halisi ya timu ya Taifa ambayo inakabiliwa na michuano mbalimbali ya kimataifa ndani ya kipindi kifupi. Aidha katika kuliimarisha benchi la ufundi la timu ya Taifa, Leopald Tasso Mkebezi ameteuliwa kuwa meneja mpya wa timu ya Taifa. Mkebezi amewahi kuwa meneja wa timu ya Taifa katika kipindi cha mwaka 2006 – 2012.

Wakati huo huo; Rais wa TFF, Jamal Malinzi kwa niaba ya kamati ya utendaji amewaomba radhi wapenzi wa mpira kwa matokeo mabaya ya Taifa Stars kwenye michuano ya Cosafa. Kikao cha kamati ya utendaji pia kilipokea taarifa juu ya mwenendo wa timu ya Taifa.

IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)