Klabu za Zamalek, Kiyovu Sport zaigomea Yanga na Simba

Baadhi ya wachezaji wa Klabu ya Zamalek

Na Mwandishi Wetu

KLABU za Zamalek ya Misri na Kiyovu Sport zimekataa maombi ya mechi zao za marudiano za Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho dhidi ya Yanga na Simba kusogezwa mbele kwa wiki moja kutoka wikiendi ya Machi 2, 3 na 4 mwaka huu.

Taarifa ambazo mtandao huu umezipata leo kutoka kwa Ofisa Habari wa TFF, Bonifasi Wambura ni kwamba, baada ya mazungumzo na klabu za Simba na Yanga, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilituma maombi Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuomba mechi hizo zisogezwe ili wachezaji wapate fursa ya kutosha kuzitumikia klabu zao na timu ya Taifa (Taifa Stars).

Wambura amefafanua kuwa Februari 29 mwaka huu Taifa Stars itacheza mechi ya mchujo ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa ajili ya fainali za mwakani nchini Afrika Kusini dhidi ya Msumbiji kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Amesema wikiendi ya Machi 2, 3 na 4 mwaka huu Yanga itakuwa inarudiana na Zamalek ugenini wakati Simba itarudiana na Kiyovu Sport jijini Dar es Salaam. CAF ilikuwa tayari kuridhia maombi hayo iwapo Chama cha Mpira wa Miguu cha Misri (EFA) na Shirikisho la Mpira wa Miguu la Rwanda (FERWAFA) wangekubali.

“Lakini EFA na FERWAFA wamekataa ombi hilo kwa vile litavuruga ratiba ya mechi za ligi katika nchi hizo,” amefafanua Ofisa Habari huyo wa TFF.

Wakati huo huo, Wambura amesema pambano la Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Mtibwa Sugar lililochezwa Februari 8 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 49,510,000.

Amesema jumla ya watazamaji 14,604 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo namba 112 kwa kiingilio cha sh. 3,000, sh. 5,000, sh. 10,000 na sh. 15,000 kwa VIP A.

Hata hivyo ameongeza kuwa baada ya kuondoa gharama za awali za mchezo na asilimia 18 ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 7,552,372.88 kila timu ilipata sh. 8,933,048.14, uwanja sh. 2,977,682.71.

Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,191,073.08, TFF sh. 2,977,682.71, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 1,488,841.36, Baraza la Michezo la Taifa (BMT) sh. 297,768.27 na asilimia 10 ya gharama za mechi ni 2,977,682.71.

Alisema mgawanyiko mwingine ni; gharama za awali za mechi zilikuwa nauli ya ndani kwa waamuzi sh. 10,000, nauli ya ndani kwa kamishna wa mchezo sh. 10,000, Posho ya kujikimu kwa kamishna na waamuzi sh. 160,000, mwamuzi wa akiba sh. 30,000, tiketi sh. 4,000,000, maandalizi ya uwanja (pitch) sh. 400,000, umeme sh. 300,000, usafi na ulinzi kwa uwanja sh. 2,350,000 na Wachina (Beijing Construction) sh. 2,000,000.

Gharama nyingine ni Jichangie ambayo ni sh. 200 kwa kila tiketi; kila klabu ilipata sh. 1,022,280 wakati Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) kilipata sh. 876,280.