KLABU ya Thai Port Football ya Thailand inatafuta wachezaji nchini Tanzania kwa ajili ya kucheza mpira wa miguu nchini humo na katika nchi nyingine barani Ulaya.
Kupitia kwa wakala wake, klabu hiyo imetuma taarifa kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ikitaka wachezaji wenye umri kuanzia miaka 15 hadi 28 kwa ajili ya kuwafanyia majaribio ambapo watakaofuzu watacheza nchini humo na katika klabu nyingine za Ulaya ambazo wana ushirikiano nazo.
Wachezaji wenye nia ya kufanya majaribio wanatakiwa kutuma taarifa za wasifu wao (CV) kwa klabu hiyo kwa njia ya emaili, wawe na pasi ya kusafiria pamoja na pasi ya mchezaji (player passport).
Wakala atapitia vitu hivyo, na kwa wachezaji atakaowahitaji atawatumia tiketi za ndege na viza kwa ajili ya kwenda kufanya majaribio nchini humo, na watakaofanikiwa kabla ya kusaini nao mikataba watawasiliana na klabu zao nchini (kwa wale wenye klabu).
MTANZANIA APEWA ITC ACHEZE YEMEN
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetoa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) kwa mchezaji Mtanzania Gossage Mtumwa ili aweze kucheza mpira nchini Yemen.
Mtumwa ambaye anatoka katika kituo cha kukuza na kuendeleza vipaji cha Rollingstone cha Arusha aliombewa hati hiyo na Chama cha Mpira wa Miguu cha Yemen (YFA) kwa ajili ya kucheza nchini humo.
TFF inamtakia kila la kheri Mtumwa katika safari yake ya Yemen, na ni matarajio yetu kuwa atakuwa balozi mzuri wa Tanzania nchini humo ili wachezaji wengine wa Tanzania nao wapate fursa ya kucheza mpira wa miguu nchini Yemen.
RWIZA KUHUDHURIA SEMINA YA MAKAMISHNA CAF
Kamishna Alfred Kishongole Rwiza ameteuliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kuhudhuria semina ya makamishna itakayofanyika kuanzia Julai 6-7 mwaka huu katika makao makuu ya shirikisho hilo jijini Cairo, Misri. Semina hiyo inashirikisha baadhi ya makamishna wa CAF walioko kwenye orodha ya makamishna ya shirikisho hilo kwa mwaka 2012-2014.
Rwiza ni mmoja wa makamishna wa CAF kutoka Tanzania, na mechi ya mwisho kusimamia ilikuwa ya Kombe la Shirikisho iliyochezwa Mei mwaka huu nchini Msumbiji. CAF tayari imeshamtumia tiketi Rwiza, na anatarajia kuondoka nchini Julai 4 mwaka huu kwenda Cairo kwa ndege ya EgyptAir.
Imeandaliwa na Boniface Wambura
Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)