Na Joachim Mushi, Thehabari-Shinyanga
VIKUNDI vya Kijamii Kata ya Songwa vimeeleza changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa Kata ya Songwa iliyopo wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga, ikiwemo Kituo cha Afya Songwa kukatiwa umeme jambo ambalo limeathiri utoaji huduma za afya katika kituo hicho.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo mjini Shinyanga mbele ya waandishi wa habari, wakazi hao wamezitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili wakazi hao ni pamoja na wodi za wagonjwa Kituo cha Afya Songwa kukatiwa huduma za umeme kwa miezi sita sasa huku wagonjwa wakilazimika kuchangia mafuta ya taa ama kwenda na taa ya chemli wanapohitaji huduma.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa kituo hicho kimekatiwa huduma za umeme baada ya Serikali kushindwa kulipa ankra za umeme unaotumiwa na kituo kinachotegemewa na wananchi.
Kituo hicho kimeonekana kukabiliwa pia na changamoto nyingine ikiwemo upungufu wa wahudumu wa afya kama wauguzi, madaktari, ukosefu wa vifaa vya tiba kama dawa, uchakavu wa wodi na nyumba za wafanyakazi, wazee, wajawazito na watoto hutozwa ada za matibabu. Changamoto nyingine ni pamoja na ukosefu wa usafiri wa wagonjwa (ambulance), hakuna chumba mahsusi kwa ajili ya ushauri nasaha na kupima VVU.
Taarifa hiyo imezitaja changamoto zingine ni pamoja na Mimba mashuleni, Ukosefu wa mabweni, Upungufu wa walimu na nyumba zao mashuleni, Ukosefu wa maabara shule ya sekondari, Upungufu wa madawati, Ukosefu wa chakula (njaa) na Wananchi kutembea umbali mrefu kutafuta maji, na yanayopatikana kwa kuuzwa ni bei ghali mpaka shs. 400 kwa lita 20.
“Maji yanayotumiwa na wakazi wa Kata ya Songwa hayatiwi dawa, wakati yale yanayotumiwa na wakazi wa Williamson Diamonds (Mwadui) yanatiwa dawa, wakati yote yanatoka kwenye chanzo kimoja cha mabwawa ya Songwa. Zahanati ya Kijiji cha Maganzo hakina maji, wagonjwa wanateseka sana, hususan akinamama waliojifungua,” inaeleza taarifa hiyo.
Wamezitaja changamoto za Kiuchumi katika Kata ya Songwa ni Ukosefu wa ajira kwa vijana, Wachimbaji wadogo wadogo wa almasi wamenyang’anywa maeneo yao na kupewa wawekezaji, Barabara nyingi za vijijini ni mbovu, Hakuna masoko ya bidhaa za wananchi ndani ya vijiji vyao.
Wanajamii hao wa Songwa wamesema mikutano ya vijiji na vitongoji imekuwa haiitishwi kwa mujibu wa utaratibu huku mapato na matumizi hayawekwi wazi, na hakuna mbao za matangazo. Viongozi hawajali malalamiko ya wananchi likiwemo suala la rushwa kukithiri.
Hata hivyo tayari changamoto zilizotajwa zimewasilishwa kwenye kikao cha ngazi ya Kata cha majumuisho ya zoezi la uraghbishi kilichofanyika Mei 28, 2012 katika Kata ya Songwa, ambapo viongozi mbalimbali akiwemo Diwani Kata ya Songwa, Mtendaji wa Kata ya Songwa, Watendaji wa vijiji kadhaa kushiriki pia.
Viongozi hawa waliahidi kuchukua hatua kadhaa kushughulikia changamoto hizi.
Matokeo ya zoezi hilo la uraghbishi yanawasilishwa kwenye uongozi wa ngazi ya wilaya ya Kishapu, huku wananchi wa Kata ya Songwa wakiwa na matumaini makubwa kwamba changamoto zilizoainishwa hapa zitashughulikiwa haraka iwezekanavyo.
Kuanzia tarehe 21/05/2012 mpaka tarehe 27/05/2012, Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kwa kushirikiana na wanaharakati ngazi ya jamii uliendesha zoezi la uraghbishi katika Kata ya Songwa, wilayani Kishapu.
Huku lengo Kuu la Uraghbishi likiwa ni kuongeza na kuboresha uwezo wa wanaharakati na waraghbishi ngazi ya jamii, wawezeshaji, wasanii na jamii pana, hasa wanawake walioko pembezoni kushiriki kikamilifu katika uchambuzi wa sera, mipango, mifumo mbali mbali na kudai kwa dhati mabadiliko, masuala ya ukombozi wa wanawake kimapinduzi ikiwemo haki ya ajira na maisha endelevu kwa wote.
Hata hivyo mafanikio Yaliyoainishwa Kupatikana ndani ya Kata ya Songwa ni Pamoja na Kupata shule ya sekondari ya Kata Songwa na ya Kijiji cha Maganzo, Kupata maji shule ya sekondari Songwa, Wanafunzi wengi zaidi kufaulu kwenda sekondari ya Kata Songwa, Kupata vyumba vya madarasa pamoja na madawati kiasi shule za sekondari Songwa na Maganzo, Zahanati ya Songwa kupata magodoro, mashuka, vyandarua na vitanda.
Mengine ni pamoja na kupata maji kwenye baadhi ya vitongoji vya Kata ya Songwa kama vile Songwa stesheni, Kuongezeka kwa nguvu ya kiuchumi kwa wanawake kupitia vikundi vya hisa na vikundi vya kijamii kutokana na kuwepo kwa mikopo ya riba nafuu kutoka kwenye vikundi vya hisa; Wanawake kupata ujasiri na kujiamini, hivyo kuwa na sauti na maamuzi ndani ya familia zao.
“Kuanzishwa kwa benki ya wajasiriamali ya BUMWACO iliyoko Maganzo, Kujenga nguvu ya pamoja katika kushughulikia masuala mbali mbali ya kijamii,” imesema taarifa.