MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiq ametoa tahadhari kwa wakazi wa jiji hilo kuwa makini kwani ugonjwa wa kipindupindu tayari umevamia baadhi ya maeneo ya jiji. Mkuu huyo wa mkoa alisema tayari watu 24 wamelazwa baada ya kubainika kuwa na ugonjwa huo, huku watu wengine wawili (mwanamke na mwanaume) wameshapoteza maisha kwa ugonjwa huo. Alisema taarifa zinasema ugonjwa huo umebainika kuwepo Wilaya ya Kinondoni kwenye Kata za Kijitonyama, Kimara, Tandale na maeneo mengine jirani na hayo.
Mkuu wa mkoa huyo alisikika akizungumza na vyombo vya habari jana na kuwataka wananchi wa jiji hilo kuzingatia usafi wa mwili na mazingira ikiwa ni pamoja na kuepuka kula hovyo na kunawa mikono kila mara ili kujikinga na ugonjwa huo.
Taarifa kutoka katika vyanzo vingine zinaeleza kuwa idadi ya watu waliopoteza maisha hadi sasa ni watatu huku wengine 30 wakiwa wamelazwa hospitalini kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Tanzania na hasa katika Jiji la Dar es salaam.
Wataalamu wa afya wanasema mlipuko huo unapatikana kwenye maeneo yenye uchafu na watu kutotumia vyoo au kuwa na vyoo vya kisasa hasa katika maeneo yenye msongamano wa makazi Dar es Salaam. Hata hivyo watu waishio katika makazi holela ndio wako katika hatari kubwa zaidi ya kuambukizwa ugonjwa huo wa kipindupindu.
Pamoja na hayo tayari maofisa wa afya wameshachukua hatua ili kuzuia mlipuko zaidi ambapo wamepulizia dawa baadhi ya maeneo ulipolipuka pamoja na kutoa kinga kwa familia za karibu zilizolipukiwa na ugonjwa. Wodi maalumu ya wagonjwa wa ugonjwa huo imeshaandaliwa pia katika Hospitali za wilaya ya Kinondoni eneo ambalo limeathiriwa na ugonjwa huo.
Dar es salaam ni mji wenye idadi kubwa ya watu, na inakadiriwa Mkoa huo unatakribani wakazi zaidi ya milioni tano kwa sasa.