KIPANDE cha barabara ambacho ujenzi wake unaendelea kwa kiwango cha lami kati ya Ndundu mkoani Pwani na Somanga mkoani Lindi chenye urefu wa kilometa 60 sasa umepangwa kukamilika kabla ya mwezi Juni 2013. Taarifa hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi Eng. Gerson Lwenge wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Mrisho Kikwete alipotembelea mradi huo akitokea mkoani Lindi.
Lwenge alimjulisha Rais Kikwete kuwa, baada ya mkandarasi huyo kushindwa kuikamilisha kazi hiyo mwezi Januari 2011 kwa mujibu wa mkataba, taratibu kadhaa zilifuatwa ili kuhakikisha kuwa mkandarasi huyo anachukuliwa hatua stahiki kwa lengo la kuhakikisha anaikamilisha kilometa 28 zilizobaki kama ilivyokusudiwa.
“Hatua kadhaa zimekwishachukuliwa ambapo kwa sasa mkandarasi ameweza kuongeza uwezo kwa kuzalisha kilometa 5 za lami kwa mwezi na hivyo kurudisha matumaini kuwa ndani ya miezi sita kazi hiyo inaweza kuwa imekamilika” alisema Naibu Waziri Injinia Lwenge..
Rais aliitaka Wizara ya Ujenzi kupitia Tanroads kuhakikisha kuwa inausimamia mradi huo kwa karibu zaidi ili kuondoa visingizio vingine vyoyote vinayvyoweza kusababisha mradi huo kuchelewa zaidi.
Ujenzi wa sehemu hiyo ya barabara ambayo ndiyo pekee iliyobaki katika barabara kuu inayounganisha mikoa ya Kusini na Jiji la Dar es Salaam, ulianza mwaka 2008 ukiwa umepangwa kukamilika ndani ya miaka mitatu. Mkadarasi aliyeshinda zabuni hiyo ni Kampuni ya M/S M.A. Kharafi & Sons kutoka Kuwait kwa gharama ya Shs. 58.8 bilioni. Fedha hizo zimetolewa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na mifuko ya maendeleo ya KUWAIT na OPEC.Baada ya ziara hiyo Mheshimiwa Rais alirejea Dar es Salaam