*Ni baada ya msafara wa Polisi Nigeria kushambuliwa
IDARA ya Polisi nchini Nigeria, imethibitisha kuwa mshukiwa mmoja ambaye anaaminika kuwa kiongozi wa Kundi la Boko Haram, ametoweka, baada ya wapiganaji wa kundi hilo kushambulia msafara wa polisi ambao ulikuwa ukimpeleka kizuizini.
Mshukiwa huyo alikuwa amekamatwa na polisi siku ya Jumamosi na alikuwa akisafirishwa korokoroni ili kuwapa maofisa wa polisi nafasi ya kufanya uchunguzi zaidi.
Baada ya kukamatwa mshukiwa huyo alikabithiwa Kamishna wa Polisi, ambaye aliamrisha mshukiwa huyo apelekwe katika kituo kimoja cha siri cha Abaji. Wakati msafara huo ulipokuwa njiani, wapiganaji wa kundi hilo waliushambulia na kumkomboa kiongozi huyo wa Boko Haram.
Idara ya polisi nchini humo, imesema maofisa wake kadhaa hawakuwajibika wakati wa tukio hilo, hivyo Serikali imemsimamisha kazi kwa muda Kamishna huyo wa polisi.
Ikiwa uchunguzi utabainisha kuwa yeye na maofisa wake walihusika na kutoweka kwa mshukiwa huyo, huenda wakafunguliwa mashtaka ya uhalifu.
Kile ambacho polisi hawajataja ni kwamba mshukiwa huyo, kwa jina Kabir Sokoto, alikamatwa akiwa ameandamana na mwanajeshi katika chumba kimoja cha Gavana wa Jimbo la Bornu kilichoko Abuja wiki iliyopita.
Maofisa wa Serikali wa jimbo hilo mjini Maiduguri walithibitisha kukamatwa kwa mshukiwa huyo. Vyombo vya habari nchini Nigeria vimetangaza kwamba mshukiwa huyo ni afisa wa ngazi ya juu na ndiye anayeaminika kuwa naibu wa kiongozi wa kundi hilo la Boko Haram.
-BBC