MKUU wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Helen Clark, atafanya ziara nchini Tanzania kuanzia Mei 10 hadi 13, 2014. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa UNIC Tanzania, Stella Vuzo kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, katika ziara ya Helen Clark anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika chakula cha jioni cha kufunga mkutano kuhusu ujangili wa meno ya tembo na hifadhi ya wanyamapori hapo Mei 10, 2014, katika Hoteli ya Hyatt Regency Kilimanjaro.
Taarifa imeeleza kuwa ujangili wa meno ya tembo na biashara haramu ya pembe za ndovu ni masuala yanayotia wasiwasi mkubwa barani Afrika na kwingineko, pamoja na kukua kwa masuala ya kiusalama, kiuchumi, kisiasa na kimazingira bado uhalifu huu unaongezeka kwa kasi. Katika Afrika Mashariki, makundi ya uhalifu yanatumia mbinu za kisasa kuua tembo na kutumia fursa ya rushwa kuvusha pembe nje ya mipaka ya Afrika. Tanzania ni nchi yenye idadi kubwa zaidi ya Tembo katika Afrika na ndio hasa iliyoathirika kwa namna ya pekee na ukuaji wa tatizo hili.
Alisema UNDP imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na serikali ya Tanzania na wadau wengine katika hifadhi ya wanyamapori kushughulikia changamoto hizi. Akiwa nchini, mkuu huyu wa UNDP atashiriki katika kufunga mkutano wa Dar es Salaam juu ya hatua za kukomesha ujangili wakati ambapo wadau wa kitaifa watajadili na kukubaliana juu ya hatua za utekelezaji wa kukomesha ujangili wa meno ya tembo na biashara haramu katika bidhaa za wanyamapori.
Mkutano huo utakuwa wa kwanza kitaifa kufuatia mikutano ya kimataifa iliyofanyika Botswana, Paris na London. Helen Clark pia atatembelea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kushuhudia matokeo ya mapambano dhidi ya jitihada za kupambana na ujangili zinazofanywa na UNDP na Mfuko wa Dunia wa Mazingira zinazolenga uhifadhi wa wanyamapori na kutunza mazingira hususan katika maeneo ya Kusini ya Tanzania, ikiwa ni pamoja na maeneo ya hifadhi ya Ruaha, Kitulo, Mpanga Kipengere na Mlima Rungwe.
Mkuu huyo wa UNDP ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani wa New Zealand, Helen Clark atamtembelea Spika wa Bunge, Anne Makinda (Mbunge) na kufanya mazungumzo na Wabunge Wanawake mjini Dodoma Mei 12, 2014, ambapo atazungumzia masuala ya jinsia na maendeleo ya wanawake katika uongozi na siasa. Tarehe 13 Mei, atakuwa Jijini Dar es Salaam na atatoa hotuba ya ufunguzi kwenye mkutano wa Kamati ya UNDP ya Mradi wa Uwezeshaji wa Kidemokrasia (wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 26), hususan suala la kura ya maoni kuhusu katiba mpya na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kwa ujumla.
Kamati hiyo inaongozwa na wenyeviti wawili wa tume za uchaguzi Tanzania (NEC na ZEC) na inajumuisha vyama vya kiraia, serikali, na wawakilishi wa wafadhili. Akiwa Tanzania, Helen Clark pia atakutana na viongozi waandamizi wa serikali na vyama vya kiraia kujadili masuala ya ukuaji wa uchumi. Vilevile kutakuwa na press conference Jumamosi tarehe10 May, 2014 kuanzia saa kumi na mbili jioni.