Kiongozi CCM Aanguka Kikaoni Afariki Dunia

Salmin Awadh Salmin

Salmin Awadh Salmin


SALMIN Awadhi Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) amefariki dunia baada ya kuanguka akiwa katika kikao cha CCM Ofisi Kuu ya chama hicho Kisiwandui.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Idara ya Utawala Baraza la Wawakilishi (BWZ), Amour M. Amour ilisibitisha kutokea kwa kifo hicho na ikaendelea kueleza kuwa Awadhi anatarajiwa kuzikwa kesho Makunduchi. Alisema shughuli za kuuaga mwili wa marehemu zitafanyika katika saa tano kwenye Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi mjini Zanzibar, kesho.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amempelekea Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, salamu za rambirambi kuomboleza kifo cha Salmin Awadh Salmin, Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni katika Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Baraza hilo.

Salmin ambaye alikuwa pia Katibu wa Kamati ya Wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika Baraza la Wawakilishi, amefariki dunia ghafla mchana wa leo, Februari 19, 2015, wakati akihudhuria kikao cha CCM kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya Kisiwandui, mjini Zanzibar.

Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Rais Shein, “Nimepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Salmin Awadh Salmin, Mwakilishi wa Jimbo la Magomeni katika Baraza la Wawakilishi na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya Baraza hilo ambaye nimejulishwa ameanguka ghafla wakati akihudhuria kikao mjini Zanzibar.”

“Nimemjua Mheshimiwa Salmin kwa muda mrefu na hakuna shaka kuwa katika miaka 10 iliyopita tokea mwaka 2005 alipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuingia Baraza la Wawakilishi ameliwakilisha vizuri Jimbo lake la Magomeni na watu wake, na ameonyesha uongozi katika Baraza la Wawakilishi na kutoa mchango mkubwa katika Chama chetu cha CCM. Tutaendelea kukosa mchango wake na busara zake za uongozi”, amesema Rais Kikwete na kuongeza:

“Nakutumia Mheshimiwa Rais salamu za rambirambi za dhati ya moyo wangu kuomboleza kifo hiki kikubwa. Aidha kupitia kwako, nawatumia salamu za rambirambi wananchi wa Magomeni ambao wamepoteza Mwakilishi wao na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi waliopoteza mwenzao na kiongozi wao.”

Ameongeza Rais Kikwete: “Kupitia kwako, vile vile, natuma pole nyingi sana kwa familia, ndugu na jamaa wa Mheshimiwa Salmin kwa kuondokewa na mhimili mkuu wa familia na mlezi. Wajulishe niko nao katika msiba huu mkubwa na kuwa msiba wao ni msiba wangu pia. Napenda pia uwajulishe kuwa naungana nao katika kumwomba Mwenyeji Mungu aiweke pema roho ya marehemu. Amen.”