Kinana wa CCM Azungumza na Mabalozi wa Rwanda na DRC

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akizungumza na Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Juma Mpango aliyefika ofini kwa Karibu Mkuu leo, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Dar es Salaam. Kushoto ni Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro.

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana akimkaribisha ofisini kwake, Balozi wa Rwanda, Dk. Ben Rugangizi aliyemtembelea ofisini kwake, leo, Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Dar es Salaam, (Picha zote na Bashir Nkoromo)

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana leo amekutana na mabalozi wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuwa na mazungumzo nao kwa nyakati tofauti, ofisini kwake, katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, jijini Dar es Salaam.

Mabalozi hao wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini ni Athumani Juma Mpango wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo aliyetangulia kuwasili ofisini kwa Katibu Mkuu na baada ya mazungumzo yao alifuatia Balozi, Dk. Ben Rugangizi wa Rwanda. Katika mazungumzo yao, mabalozi hao walimpongeza Kinana kwa kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM, na kueleza kwamba vyama tawala katika nchi zao vimepokea kwa furaha uteuzi huo.

“Chama chetu cha PPRD kinakupongeza sana kwa uteuzi wako, na tunakutakia kila la kheri katika kutekeleza jukumu hili kubwa ulilokabidhiwa”, alisema Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Mpango.

Mabalozi hao walisema wanakishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa namna wanavyosaidia nchi zao. Kwa wake Balozi Mpango alisema, Chama cha PPRD kinapongeza juhudi zinazofanywa na CCM na Serikali yake kwa namna kinavyosaidia jitihada za kuleta amani nchini DRC.

Kwa upande wa Balozi Dk. Rugangizi, alisema RPF ina mengi ya kujifunza kwa upande wa Tanzania na CCM kama chama tawala kwa kuzingatia uzoefu kilichonacho. Walisisitiza kuendeleza uhusiano uliopo hasa kwa viongozi kutembeleana kama wafanyavyo sasa.

Ili kuonyesha mshikamano na ushirikiano, Katibu Mkuu wa CCM, amemwalika Katibu Mkuu wa PPRD kuhudhuria sherehe za miaka 36 ya kuzaliwa kwa CCM zitakazofanyika kitaifa mkoani Kigoma. Hatua hiyo ilitokana na Balozi Mpango kuonyesha wasiwasi wake juu ya kuzorota kwa uhusiano wa CCM na PPRD uliokuwapo hapo nyuma. Hii ni mara ya tano kwa Katibu Mkuu kutembelewa na mabalozi wa nje wanaoziwakilisha nchi zao nchini.