NA MWANDISHI WETU
KATIBU MKUU wa Chama Cha Mapinduzi, Abdulrahaman Kinana, wiki ijayo ataanza ziara ya kikazi katika mikoa ya Shinyanga, Mara na Simiyu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu wa NEC, Itikadi Nape Nnauye, alisema, ziara hiyo ambayo naye atakuwemo, itaanzia katika mkoa wa Shinyanga Septemba 10 hadi 13 mwaka huu, kwa kutembelea wilaya zote nne za mkoa huo na kufuatiwa na mkoa mpya wa Simiyu kuanzia Septemba 14 hadi 19, pia kwa kutembelea wilaya zote tano.
Nape alisema, Kinana atahitimisha ziara hiyo katika mkoa wa Mara ambako atatembelea katika wilaya sita za mkoa huo kuanzia Septemba 20 hadi 25, mwaka huu.
Alisema pamoja na kuwa ziara hiyo ya kikazi ni ya kawaida, lakini lengo kuu ni kukagua utekelezaji wa Ilani ya Chama, kukagua na kuimarisha uhai wa chama na kuhamasisha wananchi wa maeneo hayo ambayo kwa kiasi kikubwa ni ya wafugaji, kujituma katika shughuli za uzalishaji ili Kuleta tija katika maisha yao na ya taifa kwa ujumla.
“Katika ziara hiyo Katibu Mkuu, takagua maendeleo ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010/2015 hasa katika miradi ya kimaendeleo Kama vile Ujenzi wa majosho kwa ajili ya wafugaji, maendeleo ya maboresho ya kilimo cha Pamba, uvuvi wenye tija pamoja na maboresho ya sekta za Afya, elimu na miundombinu zikiwemo Barabara”, alisema Nape.
Alisema, pia katika ziara hiyo Katibu Mkuu atapata fursa ya kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kwa kushauriana na serikali kutafuta namna ya kuzitafutia ufumbuzi.Katibu mkuu pia atafanya mikutano ya ndani, na ya hadhara katika kila wilaya za mikoa hiyo.