Kinana Aanza Mabadiliko Ndani ya CCM, Afuta Neno ‘Mheshimiwa’

Kinana, Nape, Khatib wakisalimia wananchi Uwanja wa Ndege wa Rukwa

Na Bashir Nkoromo, Rukwa

KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ameagiza kuanzia sasa wanachama wa CCM kuacha kuitana waheshimiwa badala wake watumie jina ndugu kama alivyoasisi Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere.

Kinana ametoa agizo hilo leo wakati akizungumza na viongozi wa CCM, mjini hapa, akiwa katika siku yake ya pili ya ziara ya siku nne kujitambulisha na kukagua uhai wa Chama katika mkoa huo na mikoa ya Mtwara, Geita na Arusha.

“Mimi katika masiaha yako yote ya kumfahamu Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere, sikupata kumsikia akijiita au akitaka aitwe Mheshimiwa Mwenyekiti, au Mheshimiwa Rais, sasa haya mambo ya sisi kuitama mheshimiwa tunayatoa wapi?”, alihoji Kinana.

Alisema, Mwalimu Nyerere hakujiita Mheshimiwa kwa sababu na maana kubwa sana, kwa hiyo ni lazima Wana-CCM kuendelea utamaduni huo wa kuitaka ndugu kwa sababu unazuia matabaka ya ubwana na utwana.

Mapema kabla ya mkutano huo wa ndani, Kinana alifungua shina la wakereketwa wa CCM Isesa na shina la UWT, Chanji nje kidogo ya mji wa Sumbawanga, ambapo alisema hatua ayake ya kufungua matawi hayo na kushiriki kikao cha shina kinachofunguliwa na mjumbe wa shina husika, ni ishara ya kuwaagiza viongozi wa ngazi zote wa CCM kuhakikisha wanatembelea mashina na matawi.

“Hili siyo langu, ni agizo la Mkutano Mkuu wa CCM uliomaizika mjini Dodoma hivi karibuni, pale tuliazimia kwamba, ili kuimarisha uhai wa Chama lazima viongozi wa ngazi mbalimbali watembelee mashina ma matawi ili kuzijua kero zilizopo huko”, alisema.

Alisema, kulingana na agizo hilo, sasa kila kiongozi wa Chama atapimwa ufanisi wake wa kikazi kwa kuangalia ni namna gani anafanya kazi zake kwa karibu sana na mashina na matawi.

Nape akiwa na kundi la watoto ziarani


Alisema, CCM imesisitiza lifanyike hilo kwa juhudi zaidi kwa sababu ni wazi kwamba wenye chama ni wanachi waliopo kwenye ngazi hizo za mashina na matawi, hivyo kwenda huko ndiko kutaimarisha chama kwa uhakika zaidi.

Katika ziara hiyo, Kinana amefuatana na wajumbe wa NEC, Nape Nnauye (Itikadi na Uenezi), Mohamed Seif Khatib (Oganaizesheni)na waziri wa TAMISEMI, Aggrey Mwanri.
Katika hatua nyingine, Kinana amewahakikishia Watanzania, hususan wanachama wa CCM kwamba yupo tayari kimwili na kiakili kuhakikisha anatekeleza kwa ufanisi mkubwa majukumu makubwa aliyopewa kulitumikia taifa.

Kinana alisema hayo leo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Rukwa akiwa katika siku yake ya pili ya ziara ya siku nne katika mikoa ya Mtwara, Rukwa, Geita na Arusha aliyoianza jana.

“Ni kweli nilikuwa nimetangaza kustaafu siasa kwa kuzingatia kwamaba nimeshashika kwa muda mrefu nyadhifa za kuchaguliwa, nikaona kwamba kama wenzako wameshakuamini mwa muda mrefu ukafanya nao kazi wakikupenda, basi usisubiri mapaka uchokwe ndiyo uondoke”, alisema Kinana na kuongeza;

“Lakini sasa baada ya maamuzi yangu, Mwenyekiti wa Chama Chetu, Rais Jakaya Kikwete akaamua kwa kadiri alivyoona inafaa, akaniteua nikisaidie Chama. Kwa mtu mwenye hekima na uadilifu unapoteuliwa na Mwenyekiti wa Chama chako tena Rais wa Chama kinachotawala, lazima ukubali tena bila kinyongo, nikakubali”.

“Sasa baada ya kuwa mimi ndiye Katibu Mkuu wa Chama hiki, napenda kuwaambia kwa dhadi ya moyo wangu kwamba nipo tayari, kimwili, kiakili kuhakikisha nawatumikia Wana-CCM na watanzania kwa jumla kwa weledi na ufanisi mkubwa”.

Akizungumzia mikakati ya utekelezaji wa kazi zake, Kinana alisema, atajikita zaidi katika kuimarisha uhai wa chama katika ngazi za mashina na matawi waliko wanachama, akifafanua kwamba azma hiyo kimsingi siyo yake ila ya Chama Cha Mapinduzi.

“Nakata niwambieni kwamba kazi muhimu na ya lazima amabayo lazima viongozi wote tuifanye kwa pamoja na kwa uthabiti mkubwa ni hii ya kujenga chama katika ngazi za mashina na matawi na hili si langu bali ni maamuzi ya mkutano mkuu wa CCM uliomalizika Dodoma hivi karibuni”, alisema Kinana.

Alisema, hakuna miujiza itakayokiinua Chama Cha Mapinduzi ambayo ni zaidi ya kuimarisha uhai wa mashina na matawi na kwamba ni kutokana na kujua umuhimu huo ndiyo sababu ameanza kazi yake kwa kufanya ziara za kukabua uhai wa Chama kwenye mashina na matawi na kuwataka viongozi ngazi zote wa CCM kuiga nyayo zake.

Katika ziara hiyo Kinana ambaye anafuatana na Makatibu wa NEC, Nape Nnauye (Itikadi na Uenezi) na Mohamed Seif Khatib (Oganaizesheni), mbali na kukagua uhai wa matawi na mashina, pia amekuwa akifanya mikutano ya hadhara na ya nje, ambayo ameitumia kusikiliza kero mbalimbali za wananchi. Katika kufanaya hivyo, Kinana pia amefuatana na baadhi ya mawaziri akiwemo Naibu Waziri wa TAMISEMI, Aggrey Mwanri

Mkoani Mtwara Kinana ametoa fursa kwa wananchi kueleza akwa kina kuhusu kero kuhusiana na zao la korosho ambapo Mwaziri wa Kilimo na Ushirika Injinia Christopher Chiza ilibidi apande jukwaani kufafanua kwa kina hali ya pembejeo za kilimo cha zao hilo ilivyo, changamoto zake na namna serikali inavyojaribu kuzitatua. Pia Chiza alizungumzia suala la wakulima wa zao hilo kucheleweshewa malipo yao

Mjini Rukwa Kinana alizungyumza kwa kina suala la pembejeo husuasan mbolea ya Minjingu ambayo kama ilivyokuwa mkoani Mtwara, nako waknanchi walilalamika kwamba imekuwa haiwawezeshi kupata mazao ya kutosha na kutaka ibadilishe.