Na Tiganya Vincent, MAELEZO-Dar es Salaam
MWANASIASA nguli na Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Paul Kimiti amewataka Watanzania kutembelea Maonyesho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara yanayoendelea kwenye Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ili kushuhudia viongozi anuai wazalendo walivyoleta mabadiliko ya kimaendeleo baada ya taifa kujitawala.
Kimiti ambaye pia amewahi kuwa Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Mkuu wa Mkoa ametoa kauli hiyo baada ya kutembelea Banda la Wizara ya Fedha katika Maonesho ya Miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
Alisema Tanzania imepiga hatua kubwa ukilinganisha na wakati nchi hii inachukuliwa kutoka kwa mwingereza mwaka 1961. Kimiti alisema kuwa mtu hawezi kuamini asipotembelea maonyesho na kuona shughuli mbalimbali zinazofanywa na wafanyakazi mbalimbali za umma na sekta binafsi katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata maisha bora.
“Ni wananchi wakatangaziwa ili waje kuona mambo mazuri ambayo Serikali zao zote zimejitahidi kuhakikisha zinawatekelezea ili kuwa na maisha bora…pia waswahili wanasema kuona ni kujifunza ni vema wananchi wakaja wakaona wenyewe kuliko kusikia kutoka kwa watu wengine ambao wanaweza kupotosha ukweli wa mafanikio ambayo tumeyapata tangu mwaka 1961 “alisisitiza Kimiti.
Aidha aliipongeza Wizara ya Fedha kwa hatua yake ya kutoa kitabu na kukigawa kwa wananchi ili waweze kujifunza historia halisi ya Tanzania katika sekta ya fedha na mchango wake katika kusaidia sekta mbalimbali kuleta maendeleo kwa wananchi.
Kimiti alisema kuwa hatua hiyo itawasaidia wananchi watakaosoma kuona kuwa Wizara hiyo inagusa kila sekta katika kuhakikisha kuwa wananchi wapata maendeleo.
Alisema kuwa pamoja na machapisho hayo kugawanywa kwa wananchi ni vema wasisahau kupeleka katika maeneo muhimu kama vile Maktaba za mikoa, Taifa hata mashuleni kwa ajili ya kufikisha elimu kwa wananchi wengi hata baada ya maonyesho.