KILIO cha muda mrefu cha Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Tanzania Labour Party (TLP), Agustino Lyatonga Mrema kuomba asisahaulike katika ufalme wa Rais Dk John Pombe Magufuli kimesikika na hatimaye amekumbukwa na rais kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu Lyatonga ameteuliwa rasmi na Rais Magufuli kushikilia nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Julai 16, 2016.
Kilio cha Mrema kilianza kusikika baada ya kuona mambo yanakwenda kombo kwa upinzani mkubwa katika nafasi ya ubunge aliogombea, dhidi ya Mbunge wa sasa wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia aliyemshinda katika uchaguzi mkuu uliopita.
Akiwa kwenye kampeni Jimbo la Vunjo Mrema licha ya kuwa na mgombea urais katika chama chake, alimnadi Rais Dk. Magufuli alipopita katika jimbo hilo jambo ambalo lilivuta hisia za wengi, huku akimuomba amkumbuke katika ufalme wake (uongozi).
Hata hivyo Mrema alizungumza kwa masihara huku akimuacha Dk Magufuli akicheka kwa furaha kutokana na kauli hiyo ya Mrema. Mrema alifanya tukio hilo kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu baada ya kusimamisha msafara wa kampeni wa mgombea huyo wa CCM ulipopita katika Jimbo la Vunjo.
Wengine walioteuliwa katika uteuzi wa Rais Dk. Magufuli ni pamoja na Profesa William R. Mahalu ambaye anakuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, na Prof. Angelo Mtitu Mapunda anayekuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kwa kipindi cha miaka mitatu.
Rais Dk Magufuli pia amemteuwa Bi. Sengiro Mulebya kuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bw. Oliva Joseph Mhaiki kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Mwl. Winifrida Gaspar Rutaindurwa kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Dk. Charles Rukiko Majinge kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Hospitali ya Taifa Muhimbili na Dk. Julius David Mwaiselage kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taasisi ya Saratani ya Ocean Road
Wakati huo huo, Rais Magufuli pia amewapandisha vyeo Makamishna Wasaidizi Waandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP) ishirini na tano (25) kuwa Madaibu Kamishna wa Polisi (DCP) na kuwapandisha vyeo maofisa wa Jeshi la Polisi 34 kutoka Ukamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na kuwa Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP).