Kilimanjaro watakiwa kutumia fursa kujiletea maendeleo

Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia alikuwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Cleopa David Msuya akiongea na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu Mkoa wa Kilimanjaro na uendelezaji wa fursa zilizopo kwa maendeleo ya mkoa huo na taifa leo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Arnold Kilewo. (Picha na Aron Msigwa-MAELEZO)

Na Aron Msigwa – MAELEZO

WANANCHI wa Mkoa Kilimanjaro wametakiwa kutumia fursa zilizopo katika mkoa huo ukiwemo Mlima Kilimanjaro, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro kujiletea maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya Mkoa wa Kilimanjaro ambaye pia alikuwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Cleopa Msuya amesema wananchi wana jukumu la kushirikiana na Serikali katika kutumia fursa zilizopo kujiletea maendeleo.

Amesema kwa sasa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wanakabiliwa na changamoto anuai za kimaendeleo licha ya kuwepo fursa nyingi za maendeleo, huku akisisitiza kuwa iwapo fursa hizo zitatumika ipasavyo wananchi watanufaika na umasikini utapungua.

Amefafanua kuwa maendeleo ya mkoa huo yapo wazi kutokana na mkoa huo kuwa na maeneo mazuri ya uwekezaji katika shughuli za kilimo, nguvu kazi na miundombinu mizuri ya kurahisisha ufanyaji kazi.

“Ni dhahiri mkoa wa Kilimanjaro ni moja ya mikoa yenye shule nyingi katika Tanzania, hivyo tuna nafasi nzuri ya kupata maendeleo pamoja na mlima Kilimanjaro tulionao ambao ni kivutio kizuri ndani na nje ya nchi yetu,” amesema.

Ameongeza kuwa kwa sasa Mlima Kilimanjaro bado haujatumika ipasavyo katika kukuongeza pato la Taifa licha ya mlima huo kuwa na fursa nyingi za kuwainua kiuchumi wananchi hasa katika sekta ya utalii.

Hata hivyo ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo wanaoishi maeneo ya Mlima Kilimanjaro kuendelea kutunza mazingira ya mlima huo ili uendelelee kuwa kivutio cha watalii na kuongeza pato la taifa.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Arnold Kilewo amefafanua kuwa kwa sasa jukwaa hilo linaandaa utaratibu wa kuwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo wa mkoa wa Kilimanjaro ili kutathmini na kujadili changamoto mbalimbali za kimaendeleo za mkoa huo na namna ya kuendelea kutumia fursa zilizopo ili kujiletea maendeleo ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mizengo Pinda.