Kilimanjaro walilia sukari, yaadimika kilo sasa 2,500/-

Wadau wa Sukari wakiwa Kiwanda cha Kagera

Na Joyce Anael, Moshi

WANANCHI mkoani Kilimanjaro wameiomba Serikali kuingilia kati tatizo la mfumuko wa bei ya sukari kutokana bei kupanda ghafla kutoka sh. 1,800 kwa kilo hadi kufikia sh. 2,500 kwa kilo licha ya sukari kuzalishwa kwa wingi katika kiwanda cha sukari cha TPC wilayani Moshi mkoani humo.

Wananchi hao wamesema wanashagazwa na ongezeko la bei la ghafla huku wakati mwingine sukari ikiwa haipatikani hali ambayo imesababisha wananchi wengi kuteseka licha ya Serikali kupiga marufuku kupanda kwa gaharama za bidhaa hiyo.

Walisema ni vema Serikali ikadhibiti tatizo hilo kutokana na kwamba wananchi wengi hususani wa kipato cha chini wanapata shida wakiwemo wa maeneo ya vijijini ambako sukari inauzwa kati ya sh. 2,600 hadi 3,000 kwa kilo moja.

“Suala la kupanda kwa bei ya sukari Serikali inapaswa kuliangalia na kulidhibiti kwani wanaoumia ni wananchi wasio na uwezo wa kununua sukari hiyo huku wafanyabiashara wakiendelea kuneemeka,” walisema wananchi hao.

Akizungumzia kupanda kwa bei ya sukari Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha sukari TPC kilichopo wilayani Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Baissac, amesema ongezeko bei ya sukari linachangiwa na sababu anuai ikiwemo kupungua kwa uzalishaji katika kiwanda cha sukari cha Mtibwa na kilombero hali ambayo inasababisha kiwanda hicho kuelemewa na wateja.

Alisema kupungua kwa uzalishji katika viwanda hivyo kumesababisha wateja wengi wa sukari kukimbilia mkoani Kilimanjaro na kununua sukari hali ambayo inafanya sukari kupungua na hivyo kuuzwa kwa bei kubwa.

Aidha aliongeza kuwa sababu nyingine inayosababisha kupanda kwa bei ya sukari ni baadhi ya wafanyabiashara kusafirisha sukari kwenda nchi jirani ya Kenya ambapo sukari katika nchi hiyo inauzwa kwa gharama kubwa na haipatikani. Alisema Kiwanda cha sukari cha TPC kinauwezo wa kuzalisha sukari

Tani 350 hadi 400 kwa siku lakini kwa sasa tani zaidi ya 600 zinahitajika kwa siku uhitaji ambao ni mkubwa ikilinganishwa na uzalishaji. Alisema hali hiyo inachangiwa na wateja wa sukari kuwa wengi hivyo kusababisha hata wafanyabiashara kupandisha bei kutokana na kuona

wateja ni wengi na sukari imepungua. Baissac alisema suala la kupanda kwa bei ya sukari ni la kidunia na ni kutokana na sababu nyingi ambapo ni pamoja na kupanda kwa gharama za uzalishaji ikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta.

Imebainika kuwa sukari katika kiwanda hicho inauzwa Sh. 75,050 kwa mfuko wa kilo 50 wakati wafanyabiashara hao wanauza mfuko huo kwa sh. 105,000 hali ambayo imesababisha sukari hiyo kupanda kwa ghafla na kuwakandamiza wananchi wengi.