MECHI ya kwanza ya nusu fainali ya michuano ya mwaka huu ya Kombe la Chalenji kati ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) na wenyeji Kenya (Harambee Stars) itapigwa Uwanja wa Machakos.
Kwa mujibu wa ofisa wa CECAFA, Amir Hassan mechi hiyo itachezwa Uwanja wa Machakos ulioko takribani kilometa 64 kutoka jijini Nairobi. Mechi hiyo itachezwa Jumanne (Desemba 10 mwaka huu) kuanzia saa 10 kamili jioni na itaoneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha SuperSport kupitia chaneli ya SS9.
Kilimanjaro Stars imetinga hatua hiyo baada ya kuivua ubingwa Uganda (The Cranes) kwa mikwaju 3-2 ya penalti katika mechi ya robo fainali ya michuano hiyo iliyochezwa jana Uwanja wa Aga Khan katika Jiji la Mombasa.
Hadi dakika 90 za kawaida zinamalizika timu hizo zilikuwa zimefungana mabao 2-2. Mabao ya Kilimanjaro Stars yalifungwa na Mrisho Ngasa wakati katika mikwaju ya penalti walofumania nyavu ni Amri Kiemba, Athuman Idd na nahodha Kelvin Yondani.