Kilichozimwa Bungeni hiki hapa

Mh. Vincent Nyerere

SPIKA wa Bunge, Anna Makinda, mnamo 17 Julai, aliamuru sehemu ya hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kuhusu makadirio ya matumizi ya Wizara ya Mambo ya Ndani isisomwe kwa maelezo kwamba mambo yaliyomo yanaingilia uhuru wa mahakama.

Ifuatayo ni sehemu ya hotuba iliyozimwa. Ilikuwa ikiwasilishwa na Vincent Nyerere

Mheshimiwa Spika;

KATIKA mwaka uliopita wa fedha, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ilihoji matukio mbalimbali ya mauaji ya raia yaliyohusisha askari wa Jeshi la Polisi pamoja na vyombo vingine vya dola.

Tulihoji matukio mengi ya ukiukwaji wa haki za binadamu hasa katika maeneo yenye migodi mikubwa ya dhahabu kama vile Nyamongo na Arusha…

Wakati anatoa hoja ya kuahirisha mkutano wa Bunge la Bajeti mwaka jana, Waziri Mkuu aliahidi kuwa serikali ingefanya uchunguzi wa matukio yote ya mauaji kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (The Inquests Act), Sura ya 24 ya Sheria za Tanzania. Mhe. Waziri Mkuu alisema (namnukuu):

“Vifo… ambavyo vimetokea katika mazingira ya kutatanisha chini ya mikono ya vyombo vya dola, ni lazima vichunguzwe.”

Hadi wakati huu, hakuna Mahakama ya Korona hata moja iliyoitishwa kwa lengo la kuchunguza vifo vilivyotokana na matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaitaka serikali itoe kauli mbele ya Bunge hili kama kauli ya Waziri Mkuu ilitolewa kwa lengo la kuhadaa Watanzania. Pia tunaitaka serikali itamke ni lini itaunda Mahakama za Korona ili kuchunguza matukio yote ya mauaji ya wananchi…
Kwa kuwa serikali haikutimiza ahadi yake ya kuchunguza matukio yale, vitendo vya mauaji na ukiukwaji haki za binadamu vimeendelea nchini.

Kwa mfano, katika taarifa yake kwa mwaka 2011, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinasema, “Mwenendo wa matukio ya ukatili wa polisi na mauaji yanayofanywa kinyume cha sheria na vyombo vya dola umeendelea kuongezeka…
“Kati ya Januari na Desemba 2011 tayari watu 25 wameripotiwa kuuawa wakiwa mikononi mwa polisi na maafisa wengine wa usalama, wakati watu 50 wengine walijeruhiwa.”

Mauaji yenye sura ya kisiasa

Kutokana na serikali kutochukuwa hatua kukabiliana na matukio ya mauaji yanayohusishwa na vyombo vya dola, sasa limezuka wimbi la mauaji na matukio ya majaribio ya mauaji yenye sura ya kisiasa maeneo mbalimbali nchini.

Matukio hayo ni pamoja na mauaji ya kada wa CHADEMA, Mbwana Masudi yaliyotokea wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge jimbo la Igunga, mkoani Tabora na aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Usa River, Msafiri Mbwambo, baada tu ya uchaguzi mdogo wa ubunge Arumeru Mashariki.

Aidha, kumekuwa na majaribio ya mauaji ambapo wabunge wa CHADEMA, Mhe. Highness Kiwia (Ilemela) na Mhe. Salvatory Machemli (Ukerewe), walioshambuliwa kwa mapanga mbele ya maafisa polisi na watu wanaosadikiwa kutumwa na makada wa CCM Mwanza.

Vilevile, Mhe. Mchungaji Peter Msigwa wa Iringa Mjini alivamiwa na wafuasi wa CCM wanaodaiwa kutumwa na Iddi Chonanga, Diwani wa Kata ya Nduli (CCM) katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa.

Matukio ya mauaji au majaribio ya mauaji yenye sura ya kisiasa yamewahusu pia watu… wanaonekana kupinga matakwa ya watawala.

Haya yamemkuta Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka ambaye alitekwa na kuteswa kikatili na watu ambao vyombo vya habari vimewataja kuwa maafisa wa vyombo vya dola.

Kwa mara nyingine, tunaitaka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) iamuru kukamatwa kwa watuhumiwa wote waliotajwa kuhusika na utekaji na jaribio la kumuua Dk. Ulimboka ili kufuta dhana kwamba vyombo vya dola viko juu ya sheria na vinaweza kuua au kutesa wananchi bila mkono mrefu wa sheria kuwaangukia.

Julai 14, 2012, mtu anayesemekana kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM, Kata ya Ndago, jimbo la Iramba Magharibi, Yohana Mpinga, ambaye pia ni mtoto wa Mwenyekiti wa CHADEMA, Kata ya Urughu, alifariki dunia kufuatia vurugu zilizotokea baada ya kumalizika mkutano wa hadhara uliohutubiwa na viongozi wa CHADEMA Kata ya Ndago.

Kwa vile tayari baadhi ya Wabunge na viongozi wa Serikali ndani ya Bunge hili tukufu wanaelekea kuwa wameshapitisha hukumu kwamba CHADEMA inahusika na kifo hicho, tuna haya ya kueleza kuhusiana nalo.

Kwanza, mkutano wetu wa hadhara ulihudhuriwa pia na maafisa polisi waliokuwepo wakati wote wa mkutano. Pili, licha ya kuwepo kwao, kundi la wahuni wanaodaiwa kukodiwa na makada wa CCM wa jimbo, walivuruga mkutano huo mara mbili kwa kupiga mawe watu waliohudhuria lakini mara zote polisi waliokuwepo hawakuchukua hatua zozote.

Baada ya wahuni hao kuvuruga mkutano mara ya pili, viongozi wa CHADEMA walitoa taarifa Kituo cha Polisi Ndago lilipofunguliwa jalada Na. NDG/RB/190/2012.

Tatu, baada tu ya kutoa taarifa Polisi, mkutano uliendelea bila fujo yoyote hadi ulipomalizika na msafara wa viongozi wa CHADEMA uliondoka eneo hilo kwenda Kinampanda kulikokuwa na mkutano mwingine wa hadhara.

Wakati huo, kundi la askari polisi wa Kikosi cha Kuzuia Ghasia (FFU) kutoka Kiomboi walishafika eneo la mkutano na kukuta mkutano umemalizika.

Nne, kwa vile mkutano wa CHADEMA ulimalizika kwa amani licha ya matukio ya kihuni yaliyoripotiwa Polisi, na kwa vile kulikuwa na kikosi cha FFU na askari polisi wengine katika eneo la mkutano, baada ya msafara wa CHADEMA kuondoka, ni wazi watu wanaotakiwa kutoa maelezo ya jinsi marehemu Yohana Mpinga alivyofikwa na mauti ni Jeshi la Polisi lenyewe.

Aidha, ni Jeshi la Polisi pekee linaloweza kuwaeleza Watanzania kwa nini kikundi cha wahuni waliorushia mawe viongozi wa CHADEMA na wananchi waliohudhuria mkutano wa hadhara, hawakuchukuliwa hatua zozote na polisi waliokuwepo au askari wa FFU waliofika baada ya msafara wa CHADEMA kuondoka.

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inasikitishwa sana na mauaji ya kijana huyo na inatuma salamu za pole na rambirambi kwa familia, ndugu na jamaa zake.

Lakini, tunasikitishwa na kushangazwa sana na ushabiki wa kisiasa uliojitokeza humu bungeni na kauli za kutoa hukumu zilizotolewa na baadhi ya wabunge na viongozi wa serikali bila hata kusubiri uchunguzi kamili.

Chanzo: Mwanahalisi