HOTUBA YA DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWENYE SHEREHE YA KILELE CHA MBIO ZA MWENGE WA UHURU, KUMBUKUMBU YA BABA WA TAIFA MWALIMU JULIUS KAMBARAGE NYERERE NA WIKI YA VIJANA KITAIFA, TAREHE 14/10/2015 – MKOANI DODOMA
Mheshimiwa Dkt. Fenella Mukangara, Waziri wa Habari,
Vijana, Michezo, Utamaduni na Michezo;
Mheshimiwa Zainabu Omar Mohamedi, Waziri wa Uwezeshaji, Ustawi wa Jamii, Vijana Wanawake na Watoto – Zanzibar;
Mheshimiwa Chiku Gallawa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri;
Waheshimiwa Wabunge na Wajumbe wa
Baraza la Wawakilishi;
Ndugu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma;
Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa Kutoka Tanzania
Bara na Zanzibar;
Makatibu Wakuu Kutoka Wizara Mbalimbli Tanzania
Bara na Zanzibar;
Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika
ya Kimataifa;
Waheshimiwa Viongozi wa Vyama Mbalimbali vya Siasa;
Viongozi Wetu wa Kiroho Kutoka Katika Madhehebu
Mbalimbali;
Vijana Wetu;
Ndugu Wananchi;
Mabibi na Mabwana;
Nawashukuru Mawaziri wetu Mheshimiwa Fenella Mukangara wa Serikali ya Muungano na Mheshimiwa Zainabu Omari Mohamed wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kunialika kuja kushiriki katika sherehe za mwaka huu za kilele cha Mbio za Mwenge wa Uhuru. Napenda pia kutumia nafasi hii kumpongeza na kumshukuru Mheshimiwa Chiku Galawa, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na viongozi wenzake na wananchi wote wa Dodoma kwa kukubali kuwa mwenyeji wa sherehe hizi na kwa maandalizi mazuri. Tunawashukuru kwa mapokezi mazuri na kwa ukarimu wenu mkubwa.
Pongezi kwa Wizara na Wananchi
Pia, nawapongeza Mawaziri, Makatibu Wakuu, viongozi waandamizi na maafisa wa ngazi mbalimbali wa Wizara zetu hizi mbili husika kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya ya kuandaa na kusimamia utekelezaji wa programu ya Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2015. Kwa namna ya kipekee pia napenda kuwatambua, kuwashukuru na kuwapongeza Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi, Watendaji wa Halmashauri na viongozi wa Majimbo, Kata, Shehiya, Vijiji na Mitaa kote nchini kwa kuziwezesha Mbio za Mwenge mwaka huu kufanyika kwa usalama katika maeneo yao.
Nawapongeza na kuwashukuru wananchi wote kwa jinsi walivyoupokea na kuukimbiza Mwenge katika maeneo yao. Nafarijika kuona hamasa ya wananchi juu ya Mwenge iko juu sana na kuwanyima wale wote wenye fikra hasi kuhusu Mwenge. Mwaka huu, Mwenge umekagua, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwa miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 463.5. Haya ni baadhi tu ya manufaa ya Mwenge wa Uhuru.
Pongezi kwa Wakimbiza Mwenge
Ndugu wananchi;
Nawapongeza kwa namna ya pekee vijana wetu waliokimbiza Mwenge wa Uhuru kitaifa chini ya uongozi mahiri na makini wa Ndugu Juma Khatibu Chum. Nawapongeza kwa kazi kubwa na nzuri ya kukimbiza Mwenge kwa siku 168 kupitia Mikoa yote, Wilaya zote, Vijiji vingi na mitaa mingi kote nchini. Jukumu hili ni zito na lina changamoto nyingi. Linahitaji watu wenye moyo wa uvumilivu, ustahamilivu na kuwa tayari kujitoa na kulitumikia taifa. Kwa uzalendo wenu na mapenzi kwa nchi yenu hamkukata tamaa na kuweza kumaliza mbio hizi na kuufikisha Mwenge mikononi mwangu salama salmini. Napenda kuwahakikishia kuwa tumeona uongozi ndani yenu na uzalendo mkubwa. Majina yenu yatabaki katika historia ya nchi yetu.
Nawashukuru pia, kwa Risala yenu na kwa kunikabidhi Kitabu kikubwa chenye Risala za Utii za wananchi wa Tanzania. Tutazisoma zote na tutayafanyia kazi yale yenye kuhitaji hatua za kuchukua.
Umuhimu wa Mwenge katika Taifa letu
Ndugu Wananchi;
Umuhimu wa Mwenge wa Uhuru katika Taifa letu ni jambo linalolopaswa kurudiwa kuelezwa mara kwa mara bila kuchoka. Hatupaswi kubweteka maana kazi ya ujenzi wa moyo wa uzalendo na mapenzi ya raia kwa taifa lao haina ukomo. Kama nchi kubwa ambazo zimejitawala kwa zaidi ya karne moja zinaendelea na kazi hiyo seuze sisi nchi yenye umri wa nusu karne?
Ndugu wananchi;
Mwenge wa Uhuru uliwashwa kwa mara ya kwanza tarehe 9 Desemba, 1961 kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro kutimiza ahadi ya Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wakati wa kudai uhuru wa Tanganyika kwamba: “Sisi tunataka kuwasha Mwenge na kuuweka juu ya mlima Kilimanjaro, umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki na heshima palipojaa dharau”.
Baada ya Uhuru ndipo utaratibu wa Mbio za Mwenge wa Uhuru ulipoanzishwa na kuendelea hadi sasa. Kimsingi mbio hizo zimeendelea kueneza ujumbe wa amani, umoja, mshikamano, utu na moyo wa uzalendo na kujitolea miongoni mwa Watanzania. Mambo hayo yamekuwa Tunu zinazolitambulisha nchi Tanzania na watu wake.
Ni mambo yasiyokuwa na chama wala itikadi. Sote yanatuhusu, kutugusa na kutunufaisha. Pamoja na kusema tunu hizo kila mwaka kumekuwepo na ujumbe maalum unaoakisiwa katika kauli mbiu. Mwaka huu kwa mfano kauli mbiu ni “tumia haki yako ya kidemokrasia na kupiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu 2015”. Mtakubaliana nami kuwa ni ujumbe muafaka. Aidha katika Mbio za mwaka huu pia Mwenge hueneza ujumbe kuhusu mapambano dhidi ya UKIMWI, malaria, dawa za kulevya na rushwa. Masuala hayo yamekuwa yanazungumzwa kwa miaka kadhaa sasa kwa sababu ya umuhimu wake, bado yapo na kwamba mapambano yanastahili kuendelea dhidi ya changamoto hizo. Haya ni masuala ya kutafakari tunaposherehekea Mwenge wa Uhuru, kutafakari maisha na wosia wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na kuamua juu ya mwelekeo na hatma ya nchi yetu kupitia sanduku la kura katika uchaguzi mkuu ujao.
Kumbukumbu ya Baba wa Taifa
Ndugu Wananchi;
Kama mjuavyo, katika siku ya leo, sambamba na sherehe za kumaliza Mbio za Mwenge wa Uhuru, ni siku ya kumbukumbu ya maisha ya Baba yetu wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyeaga dunia siku kama ya leo miaka kumi na sita iliyopita. Hivyo leo ni siku ya kusherehekea maisha yake na kujikumbusha mchango wake na urithi uliotuachia kama taifa na kama Watanzania. Hayati Baba wa Taifa alikuwa ni mwalimu wetu. Katika maisha yake ya uongozi hata baada ya uongozi ameendelea kuwa alama ya ushujaa, umoja wetu, uadilifu na uongozi uliotukuka. Jambo linalotia faraja ni kuwa, sote tunakubaliana kuwa Mwalimu Nyerere ndio kipimo cha uongozi bora katika nchi yetu.
Bahati nzuri, kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka huu inaadhimishwa siku 10 tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge, Wawakilishi na Madiwani nchini kwetu. Hivyo ni wakati muafaka sana kutafakari kwa wosia wake kuhusu uongozi na uchaguzi katika nchi yetu.
Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere ametuachia wosia muhimu kuhusu watu wanaofaa kuchaguliwa kuongoza nchi yetu katika hotuba zake na maandishi yake mbalimbali. Kimsingi alitutaka Watanzania tutambue kuwa hatima ya nchi yetu inategemea aina ya viongozi tulionao. Alisisitiza umuhimu wa kuwa na viongozi watakaojenga umoja wa taifa letu na uadilifu. Kwa ajili hiyo alituusia kuchagua viongozi watakaodumisha Muungano wetu na kuwawezesha Watanzania kuishi pamoja kidugu wakiwa na mshikamano na ushirikiano licha ya tofauti zao za dini, rangi, kabila au mahali watokako. Alisisitza sana uadilifu wa viongozi kwa ajili hiyo alituasa bila kumung’unya maneno kuwaogopa kama ukoma watu wanaotaka kwenda Ikulu kwa kutumia agenda za utanganyika na uzanzibari, udini, ukabila, ubaguzi wa rangi na kwa kutumia rushwa.
Ndugu zangu, Watanzania wenzangu;
Leo hii baada ya zaidi ya wiki sita za kampeni za uchaguzi na zinapoingia katika siku 10 za mwisho tumeshapata nafasi za kuwasikiliza watu wanaoomba kutuongoza na vyama vyao. Bila ya shaka tunawatambua nani ni nani? Naomba tuutumie Uchaguzi Mkuu huu kumuenzi Baba wa Taifa kwa vitendo kwa kuwakataa viongozi ambao wamekiuka wosia wake. Badala yake tuwachague viongozi watakaosaidia kuziba zile nyufa kuu nne za taifa letu alizozizungumzia kabla ya uchaguzi wa mwaka 1995. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa si tu tumemuenzi bali tumejinusuru sisi wenyewe na nchi yetu dhidi ya laana na majuto yanayoweza kutupata tukiupuuzia wosia wake. Wapo wagombea wanaodiriki kuomba kuchaguliwa kwa sababu ya kuwa dini fulani au madhehebu fulani. Wapo wapiga debe wa mgombea fulani waliothubutu kuomba watu wa kabila fulani kumpigania na kumpigia kura mgombea fulani ati kwamba wanamaslahi na mgombea huyo. Hatuchagui mgombea wa kunufaisha kabila bali Watanzania wote. Wapo wagombea ambao wameshindwa kukemea rushwa je tunawaelewaje? Wako tayari kupambana na rushwa? Hapana. Bila ya shaka wao ni sehemu ya tatizo. Bila ya shaka pia wao wanatumia rushwa kupata uongozi. Tarehe 25 Oktoba, 2015 tuwakatae.Watu wa aina hii ni balaa na janga. Tuliepushe taifa na watu wa aina hiyo.
Uchaguzi Mkuu
Ndugu wananchi;
Jukumu lililo mbele yetu sote tuliojiandikisha ni kujitokeza bila ya kukosa kupiga kura tarehe 25 Oktoba, 2015 tukiwa na vitambulisho vyetu vya mpiga kura mkononi. Bila ya hivyo hutapiga kura yako. Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha kutunza vitambulisho vyenu kwani bila kuwa navyo hutapiga kura. Nasikitishwa sana na taarifa kuwa wapo watu wanaouza vitambulisho vyao. Natamani habari hiyo iwe ni uvumi tu. Lakini kama ni kweli nawashangaa sana watu hao. Kwa nini ukubali kupoteza haki yako ya msingi ya kuchagua kiongozi wako umtakae? Nawashangaa zaidi wale wanaonunua. Hivi hiyo ndiyo maana ya kudumisha demokrasia huko? Naomba wajue kuwa wanatenda kosa la jinai. Vyombo vya dola vinawasaka watakapopatikana watafikishwa mbele vya vyombo vya sheria. Na hili litawahusu wote waliouza na kununua. Kipengele cha 2.3.1 (e) kinasema; “kila chama cha siasa kinachoshiriki katika uchaguzi kina wajibu wa kufuata na kutekeleza maamuzi na maelekezo ya Tume”.
Amani na Usalama wakati wa Uchaguzi Mkuu
Ndugu wananchi;
Napenda kuwakumbusha kuwa zoezi la uchaguzi linasimamiwa kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi ambazo zinaelekeza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) ndizo pekee zenye mamlaka ya kuendesha na kusimamia uchaguzi. Nawaomba ndugu zangu tuheshimu kauli na maelekezo ya tume hizo. Hivi karibuni baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani wametoa maelekezo kwa wafuasi wao kutaka wakishapiga kura wakae mita mia kulinda kura zao. Tume ya Uchaguzi imetoa tamko kwamba kufanya hivyo ni kinyume cha sheria. Wameeleza kwa usahihi kabisa kwamba wanaosimamia na kulinda kura za wagombea na vyama vyao kwa mujibu wa sheria ni mawakala wa wagombea na si mtu mwingine yeyote. Wao wapo ndani ya vyumba vya kupigia kura kwa ajili hiyo. Hivyo basi wafuasi wa vyama vya siasa msikubali kuchuuzwa na viongozi wenu kwa kuwaambia msiondoke vituoni kwa madai ya kulinda kura zenu. Kwanza mnazilindaje, kura zinazopigwa na kuhesabiwa ndani ya chumba cha kupigia kura.
Hapana shaka wenzetu wana dhamira mbaya na wanachotaka ni kuhamasisha uvunjifu wa sheria. Wana lao jambo lenye shari ndani yake. Hebu tujiulize, hivi ikiwa wapiga kura 22,751,292 wa bara na 503,193 wa Zanzibar watabaki kituoni kulinda kura za vyama vyao, je patatosha?
Narudia kusisitiza: Unailindaje kura yako ukiwa umbali wa mita mia moja wakati kura zinapigwa na kuhesabiwa ndani ya vituo vya kupigia kura? Mlinzi wa uhakika wa kura ni wakala wa Chama chake aliyeko ndani ya chumba cha Kupigia Kura. Tume imeshaelekeza kuwa aliyekwishapiga kura aondoke kituoni, naomba agizo hilo liheshimiwe. Anayekaidi hatavumiliwa, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake bila ya kusita. Msilazimishe Serikali kufanya yale ambayo yasiyopendeza. Lakini hapana budi na kwa maslahi ya taifa hatutoacha kutimiza wajibu wetu.
Ndugu Wananchi;
Hizo ni njama za kuleta vurugu na kutaka kuwazuia watu wengine kupiga kura. Nataka kuwahakikishia kuwa njama zao na nia yao ovu zimeshajulikana na katu hazitofanikiwa. Sisi kwa upande wetu wa vyombo vya ulinzi na usalama tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa agizo la Tume linatekelezwa kwa ukamilifu. Wale wanaotaka kufanya fujo watadhibitiwa ipasavyo bila ajizi wala kuonewa muhali. Upo usalama na ulinzi wa kutosha kuhakikisha kuwa kila mmoja mwenye sifa ya kupiga kura atapiga kura bila ya bughudha. Wale wenye nia ya kufanya fujo na kukaidi maelekezo halali wana hiyari ama ya kutiii sheria na taratibu au kukabiliana na mkono wa sheria kwa nguvu ile ile watakayoitumia wao. Kamwe hatutaruhusu, demokrasia kutekwa nyara. Kamwe hatutawapa nafasi ya kuivuruga nchi yetu. Wahalifu hawana kinga.
Mapambano dhidi ya UKIMWI
Ndugu Wananchi;
Ujumbe wa Mwenge umeendelea kusisitiza mapambano dhidi ya UKIMWI. Mwaka huu, kauli mbiu ni “Vijana wa leo na UKIMWI- Wazazi Tuwajibike”. Ni ujumbe unaokumbusha wajibu wa wazazi na walezi katika vita dhidi ya maambukizi mapya. Katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wangu, tumepata mafanikio ya kutia moyo katika vita dhidi ya UKIMWI.
Maambukizi ya VVU/UKIMWI yamepungua kutoka asilimia 7 mwaka 2007 hadi asilimia 5.1 mwaka 2012. Tumeongeza uwezo wetu wa kupima na kutambua virusi vya UKIMWI ambapo leo tuna vituo vya upimaji wa hiyari na ushauri nasaha (VCT) 2,929 ikilinganishwa na 96 mwaka 2005. Watu waliopima VVU/UKIWMI kuanzia 2005 mpaka sasa wamefikia 25,048,908. Hali kadhalika idadi ya wanaofaidika na huduma ya dawa za kufubaza (ARVs) nayo imeongezeka kutoka 16,167 mwaka 2005 hadi 1,904,000 mwaka 2015. Huduma ya kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto imeongezeka kutoka vituo 544 mwaka 2005 hadi 5,361 mwaka 2015.
Ndugu wananchi;
Mafanikio haya hayatupi sababu ya kubweteka maana maambukizi mapya bado yapo na yanaathiri zaidi vijana na hasa vijana wa kike. Inakadiriwa kuwa tunao wagonjwa wa UKIMWI milioni 1.4 nchini. Wito wa ujumbe huu wa mwaka huu ni kuwakumbusha wazazi na walezi wajibu wenu. Mnapaswa kuvunja ukimya na kuzungumza na vijana wenu kuhusu hatari inayonyemelea ujana wao, kuwaelemisha juu ya kujitunza na kuepuka mitego ya maisha inayoweza kuwaingiza katika tatizo hili. Huu ni wajibu ambao hamna mtu mwingine wa kumkasimisha, maana vijana wetu wanaishi katika kaya zenu.
Vita dhidi ya Malaria
Ndugu Wananchi;
Tuliendesha Mapambano dhidi ya malaria kwa nguvu kubwa na mafanikio ya kutia moyo katika miaka 10 ya uongozi wangu. Nafurahi kuwa kutokana na jitihada zetu tulizofanya na hatua tulizochukua zikiwemo usambazaji wa vyandarua vyenye dawa; kupulizia dawa ukoko majumbani na matumizi ya dawa mseto tumeweza kupunguza maambukizi ya malaria kutoka asilimia 18 mwaka 2007 hadi asilimia 10 mwaka 2012, na vifo vitokanavyo na malaria kutoka watu 41 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2004 hadi watu 12 kwa vizazi hai 100,000 mwaka 2014. Kwa upande wa Zanzibar, kutokana na jitihada kama hizo, haswa ila ya kupulizia mazalia ya mbu, wameweza kutokomeza malaria ambako sasa kiwango cha maambukizi ni asilimia 0.2.
Ndugu wananchi;
Jambo muhimu tulilofanya ambalo litatupa ushindi wa kudumu dhidi ya malaria ni kujengwa kwa Kiwanda cha Kutengeneza Madawa ya Viuadudu pale Kibaha. Kiwanda hiki kitazalisha madawa ya kupulizia kwenye mazalia ya mbu na hasa kuua viluviluvi vya mbu. Tutang’oa mzizi wa fitina wa malaria kwani hatimae mbu hawatakuwepo.
Vita Dhidi ya Dawa za Kulevya
Ndugu Wananchi;
Tunaendelea kupata mafanikio katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya. Haya ni mapambano makali ambayo hatuna budi kupambana kweli kweli mpaka tushinde. Dawa hizi za kulevya zinaathiri zaidi vijana wetu na kudhoofisha nguvu kazi muhimu ya taifa la leo na kesho. Aidha, ni kichocheo kikubwa cha vitendo vya uhalifu.
Ndugu wananchi;
Bahati nzuri, tofauti na ilivyokuwa huko nyuma, sasa walioathirika na dawa za kulevya wanaweza kupata matibabu na kupona. Nafurahishwa na kauli mbiu ya Mwenge mwaka huu isemayo, “Uteja wa Dawa za Kulevya Unazuilika na Kutibika; Chukua Hatua”. Inahamasisha watumiaji wa dawa za kulevya kuchukua hatua na kupata tiba. Hali kadhalika, inakumbusha wajibu wetu sote kuwasaidia wale walioathirika kwa kuhakikisha kuwa wanapata ushauri nasaha na tiba ambazo zinatolewa katika vituo vya serikali tena bila gharama yoyote.
Serikali imeendelea kutoa huduma katika vitengo vya afya ya akili vilivyopo Mirembe na Lutindi. Vitengo kama hivi vimeanzishwa pia katika hospitali Muhimbili, Mwananyamala na Temeke. Sasa tunajenga Kituo cha Matibabu cha kisasa cha Waathirika Madawa ya Kulevya hapa Itega, Dodoma ambacho kitakuwa kituo kikubwa kuliko vyote nchini. Kutokana na juhudi hizi, nchi yetu imekuwa nchi ya kwanza Kusini mwa jangwa la Sahara kuanzisha huduma hii kwenye mfumo wa afya ya jamii (public health).
Ndugu wananchi;
Upande wa pili wa mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya yaliendelea kwa nguvu. Huku nako tumepata mafanikio ya kutia moyo. Kati ya mwaka 2010 mpaka 2014 jumla ya kesi za dawa za kulevya 40,930 zilitolewa taarifa polisi. Kati yake kesi 22,167 zilifikishwa Mahakamani, kesi 18,763 zinaendelea kufanyiwa uchunguzi na kesi 1,082 zimekamilika. Kati ya mwaka 2005 na 2014 tumefanikiwa kukamata watuhumiwa 1,704 wa cocaine, wahutumiwa 2,149 wa heroine na watuhumiwa 5,462 wa mirungi. Mafanikio makubwa kuliko yote ni yale kukamatwa kwa kilo 211 za heroine mkoani Lindi mwaka 2012 kikiwa ni kiasi kikubwa zaidi kuwahi kukamatwa Barani Afrika.
Ndugu Wananchi;
Tumekwenda mbali zaidi kukabiliana na mtandao wa uuzaji na usafirishaji wa dawa za kulevya. Naweza kusema kuwa tumewadhibiti kwa kiasi kikubwa mtandao huu na sasa wamebanwa kweli kweli. Tumeongeza uwezo wetu wa kupambana na biashara ya madawa ya kulevya kwa kuipitia upya na kuibadili Sheria ya Kudhibiti Biashara ya Dawa za Kulevya ya mwaka 1995 na kutunga Sheria mpya ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Namba 5 ya mwaka 2015, iliyoanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015. Sheria hiyo pamoja na kuongeza makali ya adhabu ya makosa ya madawa ya kulevya, imeanzisha Mamlaka mpya yenye uwezo wa kupeleleza, kupekua na kukamata watuhumiwa wa dawa za kulevya. Awali, Tume kwa muundo wake, ilitegemea zaidi ushirikiano wa Polisi na mamlaka nyingine kutekeleza wajibu wake. Serikali itaendelea kuiwezesha Mamlaka hii kufanya kazi yake ipasavyo. Tunachoomba kutoka kwenu ni ushirikiano wenu. Vita hii tutashinda.
Mapambano Dhidi ya Rushwa
Ndugu Wananchi;
Tumeendelea na mapambano dhidi ya rushwa na mafanikio yameendelea kupatikana katika kipindi cha miaka 10. Hatua za kisera na kisheria tulizochukua ikiwemo kubadilisha Sheria iliyokuwapo ya Kupambana na Rushwa, kuongeza idadi ya makosa kutoka 4 hadi 24, kujenga uwezo wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa mafunzo, rasilimali watu na vitendea kazi kwa pamoja zimeongeza kasi ya kupambana na rushwa. Katika kipindi cha miaka 10, zimefunguliwa kesi 2,185 Mahakamani, watuhumiwa 611 wametiwa hatiani na fedha kiasi cha shilingi bilioni 93, 410,572, 117 kimeokolewa na kesi 658 zinaendelea Mahakamani.
Nafurahi kuwa nimejenga msingi mzuri wa vita dhidi ya rushwa. Sina mashaka kuwa katika awamu ijayo vita hii itashika kasi zaidi hasa ikiwa mgombea wa Chama changu atashinda kwani amezungumzia kupambana na rushwa na kuahidi kuunda Mahakama Maalum ya Rushwa. Sina mashaka kuwa, uchaguzi huu tutachagua wale wagombea wanaozungumza lugha ya kupambana na rushwa kwa maneno, nyuso zao na vitendo. Viongozi wasioionea rushwa haya. Hii ndio siri ya kuikabili rushwa. Inawezekana, timiza wajibu wako tarehe 25 Oktoba, 2015.
Wiki ya Vijana
Ndugu Wananchi;
Nimepata fursa ya kutembelea mabanda ya maonyesho ya shughuli za vijana katika viwanja vya barafu. Nimeguswa sana na ubunifu wao na ari yao ya kujikwamua kwa kujiajiri badala ya kungoja kuajiriwa. Mahitaji yao makubwa ni kuwezeshwa tu ili waweze kupanua shughuli zao na kuajiri vijana wenzao.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita tumejitahidi kutoa fursa kwa vijana na kuchochea maendeleo yao kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana. Mwaka 2005 Mfuko huu ulikuwa na kiasi cha shilingi milioni 100,000,000 mwaka 2005 na sasa bajeti yake imefikia shilingi bilioni 6,000,000,000 na umefaidisha vijana 10,241. Mwaka jana katika sherehe za Mwenge kule Tabora, nilizikumbusha Halmashauri zote za Wilaya na Miji kutekeleza kwa ukamilifu agizo la kutenga asilimia 10 ya mapato yao kwa mwaka kwa ajili ya shughuli za maendeleo ya Vijana na Wanawake. Nafurahi kuwa zimejitahidi kufanya hivyo na mwaka huu wa fedha zilitengwa kiasi cha shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya mfuko huo. Natambua kuwa mahitaji ya fedha yameongezeka sana kutokana na mwamko ulioko sasa. Nina imani serikali ijayo italipa jambo hili kipaumbele zaidi. Muhimu vijana msikilize wagombea na vyama vyao kwa makini kisha mfanye maamuzi sahihi.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Sherehe hizi za Mwenge ndizo zitakuwa sherehe za mwisho kwangu kushiriki nikiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Nafurahi kuwa katika kipindi chote cha uongozi wangu, Mwenge wa uhuru umeendelea kuwa na mafanikio na kuleta nuru zaidi, mshikamano zaidi matumaini zaidi na maendeleo zaidi kote ulikopita. Ninapoondoka rai yangu kwenu ni kuwa namna moja ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, ni kuudumisha Mwenge huu wa Uhuru ambao aliuasisi yeye mwenyewe.
Nitumie pia fursa hii kuwasisitiza tena kujitokeza kupiga kura ili kuchagua viongozi mnaowataka. Narudia kuwahakikishia kwa mara nyingine tena usalama katika kipindi chote cha uchaguzi. Kila mmoja na atimize wajibu wake wa kulinda amani ya nchi yetu katika kipindi hiki.
Nawatakia kila la kheri katika shughuli zenu za kila siku.
Mungu Ibariki Tanzania!
Mungu Ibariki Afrika!
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.