Kilango achachamaa bungeni, amshushua Ngeleja


*Asema hataki chai, anataka umeme

Dodoma
ILE siku iliokuwa ikisubiriwa kwa hamu na wabunge imewadia ambapo mbunge wa Same Mashariki, Anna Kilango (CCM), amekuwa wa kwanza, kumtupia makombora Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja mara baada ya waziri huyo kuwasilisha hotuba ya Makadirio ya Matumizi ya Fedha kwa mwaka 2011/2012 ya wizara yake.

Kilango akitoa mchango wake amegoma kuunga mkono hoja ya Ngeleja bungeni na kudai patachimbika iwapo hata mpa majibu ya kuridhisha kuhusu suala la kupeleka umeme jimboni kwake na kwamba hayuko tayari kuunga mkono hotuba yake.

“Kuhusu jimbo langu naomba nikwambie Waziri Ngeleja kwamba sitakuunga mkono, hapa patakuwa hapatoshi, kwanini mnawageuza wapiga kura wangu wateja wa tochi na mabetri wa nchi hii?
…Waziri ni mtu wa ajabu sana, aliniambia wataweka umeme jimboni kwangu…lakini jambo la kushangaza ni kwamba kwenye kitabu chake hakuna hata kijiji kimoja kilichoko kwenye mpango.
…Ameandika Same Mashariki lakini vijiji vilivyowekwa ni vya Same Magharibi kwa, Matayo ambaye ni rafiki yake na waziri mwenzake, hapa ananitumia mchanga kwenye macho yangu.
…Wananchi hawa nao ni binadamu, wapo kule tu kwasababu ya umasikini na shughuli za kilimo hivyo wamechoka kuwa wateja wa tochi na radio za betri wanataka umeme kama nyie mnavyotumia,” alisema Kilango.
Mbunge huyo akiendelea kuchangia alisema Ngeleja amejipendelea kwa kujiwekea vijiji tisa kwenye mpango wa kusambaza umeme wa grid vijijini. Alisema, Ngeleja amejipendelea kwa kujiwekea vijiji tisa, na kwamba pia kawampendelea na mawaziri wenzake Prof. Jumanne Maghembe (Mwanga) ambaye ni waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, na Naibu Waziri TAMISEMI, Agrey Mwanri (Siha), na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, Dk. David Mathayo (Same Magharibi).

Vijiji vilivyotajwa kwenye kitabu cha hotuba ya Ngeleja ambavyo vipo kwenye mradi huo ni Mhezi, Ijunyu, Kijom, Msindo, Mbakweni, Kizungo na Dido.
“Kila mara Ngeleja anataka kuninunulia chai, sihitaji chai yako, kwani uwezo wa kununua ninao ninachotaka ni umeme jimboni kwangu, naapa kwa jina la Mungu siungi mkono,” alisema.
Wakati Kilango anamwaga sumu hiyo, Ngeleja alikuwa akipigwa butwaa na kujifunika macho kwa kutumia mikono yake na kuinama chini ya kiti chake.
Kuhusu sekta ya madini, Kilango aliitaka serikali kuacha mara moja kupeleka mchanga wa madini nje ya nchi kwenda kusafishwa na kwamba jambo litasababisha taifa kuwa na mashimo tupu.
“Nyerere aliwahi kusema madini hayaozi, hivyo yaacheni tukipata uwezo wa kuyachimba ndiyo tuyachimbe. Siku hizi watoto wenu wanasoma sana hivyo kuwa na uwezo wa kufanya kazi hiyo,” alisema.
Kilango akichangia kuhusu mgawo wa umeme alisema tatizo hilo linaiaibisha nchi na linawaumiza watanzania na kuitaka Serikali kuchukua mradi mmoja mkubwa na kuufanyia kazi na siyo kuwa na mirorongo ya miradi.
“Naiomba serikali ichukue mawazo yetu, ichukue mradi mmoja mkubwa na kuufanyia kazi ili kumaliza tatizo la umeme nchini, kuwa na mrorongo wa miradi ndiyo imetufikisha hapa kwa serikali kupapasa papasa bila kufikia malengo,” alisema mbunge huyo.
Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keis (CCM), aliomba mwongozo na kueleza kuwa amechoka na tabia ya kudangwa kila mara na kwamba Ngeleja amedanganywa na Meneja wa Shirika la Umeme (TANESCO) Mkoa wa Rukwa kuhusu kukamilika kwa mchakato wa uwekaji nguzo jimboni mwake.
“Tumechoka kudanganywa, hatujaja bungeni kudanganywa katika vijiji ulivyovitaja kwamba mradi umatekelezeka ni uongo, hakuna hata nguzo moja iliyowekwa, meneja wa TANESCO mkoa amekudanganya,” alisema Keis.