Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa mwanasiasa anayeamua kupigana kwa sababu ya upinzani ama ushabiki wa kisiasa basi huyo siasa zimemshinda na ni vyema atafute shughuli nyingine ya kufanya.
Aidha, Rais Kikwete amewataka Wakuu wote wa Wilaya nchini ambako kuna dalili za upungufu ama tayari kuna ukosefu wa chakula wawasilishe haraka taarifa za upungufu huo Serikalini ili hatua zichukuliwe kuwafikishia wananchi chakula mapema.
Rais Kikwete ameyasema hayo leo, Ijumaa, Novemba 29, 2013, wakati alipohutubia mkutano mkubwa wa hadhara mjini Meatu katika siku ya tatu ya ziara yake ya siku tano katika Mkoa wa Simiyu ambako leo ametembelea wilaya za Bariadi, Itilima na Meatu.
Amesema kuwa tofauti ya vyama siyo sababu ya kutosha ya kugombanisha na kupiganisha watu kwa sababu mwanasiasa ambaye anaamua kupigana na mpinzani wake kwa sababu ya ushabiki wa upinzani ana matatizo kwenye akili yake.
“Kuwapo kwa tofauti ya vyama siyo sababu ya kugombana na ikitokea ukaona mwanasiasa anapigana na mwenzake kwa sababu ya tofauti za siasa basi ujue huyo ana matatizo kwenye akili yake. Mwanasiasa anayepigana kwa sababu ya tofauti za siasa basi huyo siasa zimemshinda, aende akalime muhogo,” amesema Rais Kikwete.
Rais Kikwete alikuwa anajibu malalamiko ya Mbunge wa Meatu, ambaye alikuwa amedai kuwa washabiki wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao alidai walikuwa wamewapiga washabiki wa chama chake cha CHADEMA walikuwa wanalindwa na wanasiasa wa CCM hata kama amekiri kuwa wako mahakamani.
Baada ya kusikia malalamiko hayo, Rais Kikwete amesema: “Ukiona mwanasiasa anapigana kwa sababu ya ushabiki wa siasa ujue kuwa amefilisika. Huyu siasa imemshinda, aende kulima muhogo. Ugomvi ama lugha za damu itamwagika na nchi haitatawalika hazina nafasi katika siasa. Ushindani wetu siyo wa ngumi bali wa nguvu ya hoja kwenye majukwaa.”
Amesisitiza Rais Kikwete: “Mwanasiasa anayeanzisha ugomvi, awe wa CCM ama wa CHADEMA, huyu siasa zimemshinda. Akafanye shughuli nyingine. Kubwa ni kwamba mtu wa namna hiyo anastahili kukamatwa na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.”
Kuhusu malalamiko ya wananchi kuhusu uhaba na ukosefu wa chakula ambayo Rais Kikwete ameelezwa njiani wakati anasafiri kutoka Wilaya ya Bariadi kwenda Wilaya ya Meatu kupitia Wilaya ya Itilima, Rais amesema:
“Nyinyi viongozi hamjanieleza jambo hili lakini wananchi wamelalamika sana njia nzima. “Wanasema wanakabiliwa na upungufu na uhaba wa chakula kwa sababu ya ukame. Nawataka viongozi wa Wilaya hii yenye historia ya ukame na wilaya nyingine nchini kuandaa haraka taarifa za hali ya chakula na kuziwakilisha Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kufanyiwa kazi.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Viongozi changamkieni kuleta taarifa. Lakini nataka jifunzeni kuacha kulima mahindi – maeneo yenye mvua kidogo mahindi hayastawi mnapoteza jasho lenu bure. Limeni mtama unastahili ukame vizuri zaidi.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.