Kikwete Kigeugeu

Na Saed Kubenea

-Anauma na kupuliza

-‘Auchuna’ kuhusu ufisadi

RAIS Jakaya Kikwete sasa ana sura mbili. Akiwa serikalini anauma. Akiwa kwenye chama chake anapuliza.

Wachunguzi wa masuala ya siasa nchini wanasema ameonyesha kuwa kigeugeu, hali ambayo inaweza kungharibu hadhi ndani na nje ya nchi.

Hayo yamedhihirika katika taarifa ya Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) iliyotolewa juzi Jumatatu mjini Dodoma na Katibu mwenezi, Nape Nnauye.

Nape aliwaambia waandishi wa habari kuwa CC imeagiza serikali “kutafuta njia za kushusha bei ya mafuta ya taa” ambayo yanatumiwa na wananchi wengi wa kipato cha chini.

Taarifa ya CC imesema chama hicho hakijaridhishwa na uamuzi wa serikali wa kupandisha bei ya mafuta ya taa nchini kwa kuwa nishati hiyo ndiyo kimbilio la wananchi wengi.

Serikali ya Rais Kikwete ndiyo iliweka bei ya mafuta ya taa ambayo wananchi wanasema ni kubwa na hailipiki; lakini ni chama cha Kikwete pia ambacho kinadai kuwa hakiridhishwi na upandishaji wa bei ya mafuta ya taa.

“Rais wetu ana sura mbili. Akiwa serikalini anashiriki vikao vya kupitisha bajeti ya serikali. Akiwa katika chama analalamikia kupanda kwa bei ya bidhaa. Hata wananchi watashindwa kumwelewa,” amesema John Mnyika, mbunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA-Ubungo).

Mjumbe mmoja wa CC aliyehudhuria kikao cha siku moja mjini Dodoma, amesema “…hata sisi tunashindwa kutetea hili. Ni kweli chama chetu  kinatakiwa kuisimamia serikali yake, lakini kwa kauli hii ya mheshimiwa, inaonyesha ama amechoka au anataka kukwepa wajibu wake.”

Haiwezekani CC ambayo Kikwete ni mwenyekiti, ilalamikie serikali ambayo pia Kikwete ni rais wake, ameeleza mjumbe huyo akiomba jina lake kutotajwa gazetini.

Kwa mujibu wa taarifa ya CC iliyotolewa na Nape, CC imesema haikuridhishwa na maelezo ya kupandishwa kwa bei ya mafuta ya taa na visingizo vya kuzuia uchakachuaji wa mafuta mengine.

Nape amesema CC imevitaka vyombo vya serikali vinavyohusika na usimamiaji wa ubora wa mafuta, kuhakikisha “vinatimiza wajibu wake kuzuia kabisa mtindo wa uchakachuaji wa mafuta nchini na si kupandisha bei ya mafuta ya taa kama suluhisho.”

Katika bajeti ya serikali iliyotangazwa Juni mwaka huu, serikali ilipandisha bei ya mafuta kutoka Sh. 900 kwa lita. Hivi sasa yanauzwa kati ya Sh. 2000 na 2100 kwa lita.

Kwenye baadhi ya vituo vya mafuta, bei hii ama ni sawa na ile ya dizeli na petrtoli na pengine ni zaidi ya bei ya mafuta hayo. Mafuta ya taa ndiyo yamekuwa nishati muhimu kwa kuwasha majumbani na hata kupikia mijini na vijijini.

Tayari wabunge, wakikariri kauli za wanaowawakilisha, wameonya serikali kuwa ongezeko la bei ya mafuta ya taa litajitokeza kwenye uharibifu wa mazingira ambapo miti mingi itakatwa kwa ajili ya mkaa ambao ni nishati mbadala.

Bei ya petroli na dizeli katika vituo mbalimbali inauzwa kati ya Sh. 2000 na Sh. 2100. Maelezo ya serikali wakati huo yalikuwa kwamba mafuta ya taa yanachanganywa kwenye dizeli na kwamba kupandisha bei ya mafuta ya taa kungesaidia kupunguza uchanganyaji ambao unaleta madhara kwa magari lakini pia kuwapatia wachakachuaji faida isiyo halali.

Haijafahamika na wala CCM haikufafanua jinsi ya kupunguza bei ya mafuta ambayo tayari iliishapitishwa na bunge katika bajeti kuu.

Wachunguzi wa mambo wanasema hata kama serikali itapunguza bei ya mafuta na hivyo kuingiza pengo katika mapato yake yaliyolengwa, bado thamani ya shilingi imeporomoka kwa asilimia tatu (3%) tangu kutangazwa kwa bei.

“Unajua bwana, huyu Kikwete amejiingiza katika mgogoro mwingine. Maana aliongoza kikao cha baraza la mawaziri na kupitisha uamuzi huu wa kupandisha bei ya mafuta ya taa. Lakini leo, anakuja kwenye chama na kulalamika, kana kwamba yeye siyo sehemu ya kile kilichoamuriwa na serikali,” amelalamika Mnyika.

“Hii bajeti kuu ya serikali iliyopitisha na bunge, iliwasilishwa na waziri wa fedha, Mustafa Mkullo ambaye ni mteule wa Rais Kikwete. Sasa katika mazingira hayo, Kikwete anawezaje kusema kwamba CCM inataka serikali ichukue hatua ya kushusha bei?” anahoji Mnyika.

Kuhusu tatizo la uhaba wa umeme, CC iliyokutana chini ya Rais Kikwete imeeleza masikitiko yake kwa kukosekana kwa nishati hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa na mtu mmojammoja.

Hapa chama kimeitaka serikali pia “kutumia muda iliyopewa wa kurekebisha bajeti ya wizara ya nishati na madini ili kuja na mpango wa dharura wa kunusuru hali hiyo na kisha kulimaliza kabisa tatizo la umeme nchini.”

Wakati hayo yakiendelea, taarifa kutoka ndani ya CC zinasema rais Kikwete alikwepa kabisa kuzungumzia suala la ufisadi ndani ya mkutano huo ambalo ni miongoni mwa tuhuma zilizomg’oa Rostam Aziz, mbunge wa Igunga aliyejiuzulu.

Wakijadili mrithi wa Rostam Igunga, wajumbe wamekubaliana kuwa wakienda Igunga, ni marufuku kuzungumzia “suala la ufisadi” kwa maelezo kwamba kufanya hivyo kutawakosesha ushindi.

Imeelezwa na mtoa taarifa wa gazeti hili kuwa hoja ya ufisadi iliyoambatana na msamiati wa kujivua gamba, iliibuliwa kikaoni na mwanasiasa mkongwe nchini, John Malecela.

“Alikuwa John Malecela, mjumbe wa CC aliyeibua hoja ya ‘magamba,’ lakini kabla hajafika mbali, mwenyekiti (Rais Kikwete), alionyesha kutoliwekea uzito suala hilo. Hakutaka maoni juu ya kulizima au kuliendeleza,” ameeleza mtoa taarifa akimnukuu mjumbe wa CC.

Alisema baada ya hoja hiyo kuzimwa, ndipo Kikwete akaelekeza mjadala katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa ubunge jimboni Igunga.

“Unajua mle ndani mlikuwa na John Malecela, Nape Nnauye na John Chiligati. Hawa ndio walioonekana kutaka kuibua hoja hii ya kujivua gamba. Lakini nakuambia Kikwete hakutaka suala hilo lijadiliwe, badala yake alielekeza chama kiangalie jinsi ya kupata ushindi katika jimbo la Igunga,” chanzo cha taarifa kimedokeza.

Haikuweza kufahamika mara moja ni kipi kilichosababisha Kikwete kutoonyesha kutaka kuzungumzwa kwa suala hilo.

Taarifa zinasema hata kauli ambazo Nape alitoa wakati akiongea na waandishi wa habari, zilikuwa zimeelekezwa na Kikwete mwenyewe.

“Wakati wa kufunga mkutano, Kikwete alieleza wenzake, hii ajenda (ya kujivua gamba) si wakati wake. Nawe Nape ukiulizwa na waandishi wa habari kuhusu agenda hiyo, jibu lake ni very simple (rahisi). Waeleze haya mambo ni ya NEC, yataishia kwenye NEC,” ameeleza mtoa taarifa.

Kauli ya mtoa taarifa inashabihiana na maelezo ya Nape kwa vyombo vya habari.

Katika taarifa yake Nape alisema, “…kuhusu suala la maadili ndani ya chama, chama kinaendelea kusimamia maadili, na kuwataka wale waliotakiwa kujipima na kuwajibika kutumia muda huo kujipima na kuwajibika kwa masilahi mapana ya chama.”

Alisema kikao cha NEC kitafanyika wakati wowote Septemba mwaka huu.

Bali taarifa za ndani ya kikao zinasema kuhusu ajenda ya uchaguzi mdogo wa Igunga, Kikwete alisikika akisema, “…Igunga ina mwenyewe, naye ni Rostam Aziz.”

Alisema, “Hamuwezi kumtukana Rostam na papohapo mkasema mnataka kushinda Igunga. Kama kuzungumza, basi zungumzeni na Rostam; ninyi wenyewe mtajua jinsi ya kumtafuta na kumpata.”

Haikuweza kueleweka iwapo Kikwete alikuwa na nia ya kupeleka ujumbe kwa Rostam kuwa anamhitaji ili waweze kutapa kiti cha Igunga au hayo ni masharti ya Rostam ili aweze kuwasaidia.

Mjumbe wa CC ambaye pia hakutaka jina lake litajwe gazetini ameliambia gazeti hili, “Unajua baada ya yaliyotokea Igunga, kila mtu anaogopa. Nadhani hatua ya huyu bwana imesaidia kurejesha adabu ndani ya chama.”

Baadhi ya wajumbe, taarifa zinasema, walipendekeza Nape na wenzake kutoshiriki kampeni za Igunga, jambo ambalo wajumbe wawili wamesema liliafikiwa na Kikwete kwa kile kilichoitwa, “kukiepusha chama na balaa la kushindwa uchaguzi.”

Uamuzi wa kampeni kufanywa na wabunge, viongozi wa mkoa na wilaya za mkoa wa Tabora ulikuja baada ya baadhi ya wajumbe wa CCM kuonya hatari ya chama kumtumia Nape, Chiligati na wenzao katika kampeni hizo.

“Haukuwa uamuzi uliokuja hivihivi tu. Baadhi yetu tulisema wazi kuwa hawa watu wakikanyaga Igunga tutashindwa uchaguzi,” ameeleza mjumbe huyo wa CC.

Mbali na Kikwete kukataa kusikiliza malalamiko dhidi ya Lowassa na wenzake, aligoma pia kusikiliza malalamiko yaliyowasilishwa dhidi ya waziri wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, ambaye alituhumiwa kutoa kauli zinazodaiwa kudhoofisha serikali.

Aliyeshambulia Sitta alikuwa Steven Wassira ambaye amenukuliwa akisema, “kuna watu wanatoka kwenye vikao halali, lakini wanakwenda nje kupinga serikali. Kama hawataki watoke,” alifoka Wassira.

Hata hivyo, Kikwete hakutaka kusikiliza hoja hiyo, badala yake alisema, “…Ndiyo, lakini nadhani si muhimu kwa sasa.”

Nje ya mkutano, Andrew Chenge, mmoja wa wanaotakiwa na CCM kuondoka ndani ya chama hicho kwa madai ya ufisadi, ameeleza MwanaHALISI, “…kwangu gamba limeishia kiunoni, kuliondoa hapa lilipo sharti uje na shoka.”

Chenge alikuwa akijibu swali la mwandishi wa gazeti hili lilitaka kufahamu ni lini ataondoka katika uongozi wa chama chake kutokana na kutuhumiwa ufisadi.

Chanzo: MwanaHalisi