Kikwete: Hatuwezi kuingilia masuala ya ndani ya nchi jirani

Malabo, Equatorial Guinea

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesisitiza kuwa kamwe Tanzania haitaingilia masuala ya ndani ya nchi yoyote jirani kwa sababu nchi hiyo haiwezi kuwa sehemu ya nguvu za kunyumbisha nchi nyingine.

Aidha, Rais Kikwete ameahidiwa kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi (UNHCR) litajaribu kuwashawishi wabia wa maendeleo duniani kuisaidia Tanzania katika kubeba mzigo mzito wa kutunza wakimbizi wa nchi za jirani za Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Kauli hiyo ya Mheshimiwa Rais na ahadi vilitolewa jioni ya jana, Alhamisi, Juni 30, 2011 wakati Rais Kikwete alipokutana na kufanya mazungumzo na Kamishna Mkuu wa UNHCR, Antonio Buterres mjini Malabo, Equatorial Guinea.

Viongozi hao wawili walikutana kwenye Ukumbi wa Kijiji cha Umoja wa Afrika (AU) cha Palace of Conferences mjini Malabo ambako viongozi hao wawili wanahudhuria Mkutano wa 17 wa Wakuu wa Umoja wa Afrika ulioanza jana na unamalizika leo, Ijumaa, Julai 01, 2011.

Katika mazungumzo hayo, viongozi hao wawili walijadili hali ilivyo katika eneo la Maziwa Makuu ambako hali ya kupungua kwa migogoro ya kisiasa na kijamii imepelekea kupungua kwa uzalishaji wa wakimbizi hata kama bado Tanzania inaendelea kuwa mwenyeji wa karibu wakimbizi 128,118 kutoka nchi za Burundi na DRC walioko katika kambi mbili za Mkoa wa Kigoma za Mtabila kwa ajili ya wakimbizi wa Burundi na Nyarugusu kwa ajili ya wakimbizi wa DRC.

“Nashukuru Mungu hakuna tena mazingira ya kuzalisha na kuingiza wakimbizi katika Tanzania. Ni muhimu hali ya utulivu huo ikaendelea na ndiyo maana kamwe Tanzania haitakuwa chanzo cha kuingili mambo ya ndani ya nchi nyingine katika eneo la Maziwa Makuu na hivyo kusababisha kuchafuka kwa hali ya kisiasa na kijamii katika nchi hizo.
“Tunayo mambo mengi sana na kazi kubwa ya kufanya kiasi cha kwamba hatuna hata muda wa kujiingiza katika mambo ya ndani ya nchi nyingine. Hatuna muda wa kuingilia mambo ya wengine. Tunapambana na umasikini, tunahangaika kuwatafutia wananchi wetu maisha bora. Hivyo, kamwe Tanzania haiwezi kuwa sehemu ya kuyumbisha nchi nyingine katika eneo la nchi zetu. Huu ni msimamo unaoongozwa na kanuni na msingi thabiti wa ujirani mwema,” Rais amemwambia Mheshimiwa Buterres.

Kiongozi huyo wa UNHCR ameilika Tanzania katika sherehe za kuadhimisha miaka 50 ya shirika hilo ambazo zitafanyika Desemba 8-9 mwaka huu. Rais Kikwete amekubali mwaliko huo ambako Tanzania inatakiwa kuwakilishwa kwenye ngazi ya mawaziri.

Imetolewa na:

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais,
Safarini,
Malabo, Equatorial Guinea.

01 Julai, 2011