Kikwete Awaonya Ludewa Juu ya Uuzaji Ardhi na Mashamba

 

lu8

Rais Jakaya Mrisho Kikwete akisalimiana na wananchi alipoowasili katika uwanja wa mikutano wa Ludewa ambako alihutubia mkutano wa hadhara.

LI6

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akionesha kilele cha Central Liganga hill ambacho ni mojawapo ya sehemu ambazo kampuni ya Sichuan Hongda ya China itachimba mashapu ya chuma na kuyafua katika  kiwanda kikubwa cha kufua chuma kitachoajiri watu 32, 000 katika eneo hilo lenye utajiri wa chuma la  Liganga wilaya ya Ludewa mkoani Njombe leo Oktoba 22, 2013. Kampuni hiyo

 

LI3

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na wawekezaji wa kampuni ya Sichuan Hongda ya China ambao ni wawekezaji katika eneo lenye utajiri wa chuma la  Liganga wilaya ya Ludewa mkoani Njombe leo Oktoba 22, 2013. Kampuni hiyo inatarajiwa kujenga kiwanda cha kufua chuma mapema mwakani kitachajiri watu 32,000 kitakapokamilika.

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete amewaonya wananchi wa Wilaya ya Ludewa wasiwe hodari ya kuuza ardhi na mashamba yao ambayo yatakuwa mali sana katika miaka michache ijayo kufuatia matunda makubwa ya uwekezaji wa Serikali katika miradi ya chuma, makaa ya mawe na madini mengi yanayopatikana kwenye Wilaya hiyo.

Badala yake, Rais Kikwete amewataka wananchi wa Wilaya hiyo kuchangamka mapema kuwekeza katika raslimali hizo kubwa zinazopatikana katika Wilaya hiyo ya Mkoa wa Njombe. Rais Kikwete ameyasema hayo, Oktoba 21, 2013, wakati alipoitembelea Wilaya huyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku saba katika Mkoa wa Njombe ambako tayari ametembelea Wilaya za Njombe, Makete na Wanging’gombe.

Rais Kikwete amewaambia wananchi wa Ludewa katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Ludewa: “Msiwe hodari wa kuuza mashamba na ardhi yetu na nyie mkabakia kama vibarua kwenye maeneo yenu,” amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Msipochangamka mapema na kuanza kuangalia namna ya kunufaika na raslimali za hapa, mtageuka manokoa wa watu wengine kwenye ardhi yenu wenyewe. Baada ya muda mfupi raslimali hizi zikianza kuonekana vizuri zaidi wajanja watakuwa wengi hapa na wanaojua pesa watafurika hapa kwenu. Hivyo, jiandaeni mapema.”

Mbali na madini mengi na ya kila aina ambayo yamethibitika kuwemo katika Wilaya ya Ludewa, Wilaya hiyo pia ina raslimali mbili kubwa za makaa ya mawe katika eneo la Mchuchuma na miamba ya chuma katika eneo la Liganga, maeneo yanayotenganishwa na umbali wa kilomita 45 tu.

Inakadiriwa kuwa miradi yote mikubwa na yenye thamani ya mabilioni ya dola za Marekani itaweza kuajiri maelfu ya watu moja kwa moja ama ama wategemezi wa waajiriwa wa moja kwa moja. Rais Kikwete amesema kuwa kulingana na takwimu za kitaalamu, eneo la makaa ya mawe la Mchuchuma lina kiasi cha tani milioni 370 na eneo la milima ya chuma ya Liganga lina kiasi cha tani milioni 200, madini ambayo yatachimbwa kwa miaka inayokadiriwa kufikia 70 tokea siku uchimbaji ukianza.

Ili kuweza kuanza uchimbaji wa madini hayo, kiasi cha dola za Marekani bilioni 1.3 zitawekezwa katika mradi wa Mchuchuma na kiasi cha dola bilioni 1.7 zitawekezwa katika mradi wa Liganga. Rais Kikwete amesema kuwa ili kujiandaa na Watanzania kunufaika na miradi hiyo mikubwa, Serikali yake imeamua kujenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) kikubwa katika eneo la Shauri Moyo, Kata ya Lugarawa, kitakachotoa mafunzo maalum yanayohusiana na utaalam wa makaa ya mawe, chuma na madini.

Tayari Serikali imetoa Sh. bilioni nne kwa ajili ya ujenzi huo kwenye eneo la ekari 78.2 ambalo limetolewa na Serikali tayari kwa ujenzi kuanza Machi, mwakani, 2013. Rais Kikwete pia ameutaka uongozi wa Wilaya ya Ludewa na Mkoa wa Njombe kuanza maandalizi ya kuyapanga vizuri maeneo ya Liganga na Mchuchuma kwa ajili ya uwekezaji huo mkubwa. “Anzeni kupanga namna maeneo hayo yatakavyokuwa ili tuwe na miji mizuri na ya kuvutia katika maeneo hayo.”