Kikwete awakumbuka Prof Mushi na Mwakiteleko


Marehemu Danny Mwakiteleko

RAIS Jakaya Kikwete amemtumia salaam za rambirambi Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. Rwekaza Mukandala kufuatia kifo cha Mhadhiri Mwandamizi Prof. Samuel S. Mushi wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala.

Katika taarifa hiyo pia Kikwete amempa pole Ofisa Mtendaji Mkuu wa New Habari (2006) Limited, Hussein Mohamed Bashe kufuatia kifo cha Naibu Mhariri Mtendaji na Mhariri wa gazeti la Rai, marehemu Daniel Daimon Mwakiteleko kilichotokea alfajiri Julai 23, 2011 katika hospitali ya Muhimbili kitengo cha MOI, kufuatia ajali ya gari iliiyotokea Julai 19, 2011.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa jana jijini Dar es Salaam kutoka ikulu, ilieleza kuwa Prof. Mushi, alikuwa Profesa wa kwanza Mtanzania katika Idara hiyo. Kikwete amemwelezea Prof. Mushi kuwa Msomi, Mwalimu na Mwanataaluma Mahiri katika fani yake.
“Tumepoteza msomi mahiri na shupavu katika chuo chetu na nchi kwa ujumla, ametoa mchango mkubwa katika elimu, siasa na jamii ya Tanzania, ametuachia pengo kubwa na hatutamsahau milele,” alisema katika taarifa yake.
Rais ameomboleza na kumwomba Prof. Mukandala kumfikishia rambirambi zake za dhati kwa familia, ndugu, jamaa, wanazuoni na wanataaluma wote ambao wameguswa kwa kiasi kikubwa na kifo cha Prof. Mushi.

Akimzungumzia Mwanahabari nguli na mhariri wa kampuni ya New Habari, Kikwete alisema; “Tasnia ya Habari imeondokewa na mmoja wa vijana wake hodari na makini sana, ni pengo kubwa na litaonekana kwa muda mrefu”.

Rais amesema. “Dan amekuwa mmoja wa waandishi mahiri hapa nchini, nimemfahamu vyema kwa umakini na uandishi wake uliozingatia taaluma. Pokea rambirambi zangu za dhati na kwa masikitiko makubwa, na pia naomba unifikishie rambirambi zangu kwa mke wa marehemu, ndugu, jamaa na waandishi wote ambao Dan amekuwa mmoja wao kwa miaka mingi”.

Ameongeza, tumwombee Dan pumziko jema la milele na pia tuwaombee mke, watoto na familia ya marehemu nguvu na subira katika kipindi hiki kigumu. Pia nawaombea waandishi wenzake aliofanya nao kazi sehemu zote wamkumbuke mwenzao na kuiga yale yote mema aliyofanya katika taaluma yake na kuwa mfano bora siku zote. Amina.