Kikwete atuma rambirambi kifo cha Paul Chiwile

Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Marehemu Paul Chiwile

Na Mwandishi Maalumu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Ludovick Mwananzila kufuatia kifo cha ghafla cha Mkuu wa Wilaya ya Liwale, Marehemu Paul Chiwile kilichotokea usiku wa kuamkia leo tarehe 23 Machi, 2012 Mkoani Lindi alikokuwa amekwenda kikazi kutekeleza majukumu muhimu ya kitaifa.

Marehemu Paul Chiwile alikwenda Mjini Lindi kuhudhuria Kikao cha Kamati ya Sherehe za NaneNane, Kikao cha Siku ya UKIMWI Duniani ambayo mwaka huu kitaifa itafanyika mkoani Lindi, Kikao cha Maandalizi ya Maonyesho ya SIDO ambayo Kikanda yanafanyika Mkoani Lindi, na Kikao kuhusu Wiki ya Watu wenye Ulemavu wa Ngozi ambayo pia kitaifa inafanyika Mkoani humo.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa na habari za kifo cha ghafla cha Mheshimiwa Paul Chiwile ambaye enzi za uhai wake nilimfahamu kama kiongozi hodari, shupavu na msaidizi muhimu katika kusukuma gurudumu la maendeleo katika nchi yetu hususan katika Wilaya ya Liwale alikokuwa akiwatumikia wananchi”, amesema Rais Kikwete katika katika salamu zake.

Amesema kifo chake kimeacha simanzi na huzuni kubwa kwa wananchi wa Wilaya ya Liwale huku Taifa na hususan Wilaya ya Liwale ikiachwa na pengo kubwa la kiuongozi.

Kutokana na kifo cha Marehemu Chiwile, Rais Kikwete amemuomba Mkuu wa Mkuu wa Lindi kunfikishia salamu zake za rambirambi na pole nyingi kwa kwa familia ya Marehemu kwa kuondokewa na mpendwa wao na mhimili madhubuti wa familia.

Ameihakikishia familia hiyo kuwa yupo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo. Amesema anamuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema ailaze mahala pema peponi roho ya Marehemu Paul Chiwile, na awape wanafamilia moyo wa uvumilivu na ujasiri katika kipindi chote cha maombolezo.

Rais Kikwete vilevile ametoa pole nyingi kwa wananchi wa Wilaya ya Liwale kwa kumpoteza kiongozi muhimu aliyejitoa vilivyo kuwatumikia. Amewataka hali kadhalika wawe watulivu na wavumilivu licha ya kumpoteza kiongozi wao kwani kazi ya Mungu haina makosa.