HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHE. DKT. JAKAYA MRISHO KIKWETE KWENYE UFUNGUZI WA KITUO CHA UPASUAJI WA MOYO NA MAFUNZO CHA HOSPITALI YA TAIFA MUHIMBILI,
TAREHE 27 APRILI, 2014
Mwakilishi wa Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Mhe. Chen Changzhi,
Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Mhe. Dkt. Seif S. Rashid (Mb),
Katibu Mkuu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Bw. Charles Pallangyo,
Mhe. Balozi wa Serikali ya Watu wa China,
Waheshimiwa Mabalozi waliopo hapa,
Mwenyekiti na Wajumbe wa Bodi ya Wadhamini, Hospitali ya Taifa Muhimbili,
Viongozi Wenzangu;
Wafanyakazi wa Hospitali ya Muhimbili;
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana,
Shukrani
Nakushukuru Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii kwa kunialika kuja kushiriki nanyi katika ufunguzi wa kituo hiki muhimu cha upasuaji wa moyo na mafunzo. Nafurahi kuwa Mheshimiwa Chen Changzhi, Naibu Spika wa Bunge la China amejumuika nasi katika hafla hii. Alikuja hapa kwa sherehe za miaka 50 ya Muungano akimwakilisha Rais wa China. Tukaona tutumie fursa hiyo pia tuzindue kituo hiki muhimu kilichojengwa kwa msaada wa Serikali ya China kugharamia sehemu kubwa ya gharama. Kituo hiki kimegharimu shilingi bilioni 26.6 kati ya hizo China imetoa shilingi bilioni 16.6 na Tanzania imetoa shilingi bilioni 10.
Kituo tunachokizindua leo ni kituo cha kisasa kabisa, chenye vifaa vya hali ya juu, vinavyotumia teknolojia ya kisasa katika uchunguzi na tiba ya magonjwa ya moyo. Kupatikana kwa kituo hiki, Tanzania inapiga hatua nyingine muhimu katika kuendeleza huduma ya afya nchini. Ni ukweli usiofichika kwamba maradhi ya moyo duniani yanaongezeka. Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa kwa mwaka takribani watu milioni 12 wanakufa duniani kwa maradhi haya. Hapa nchini inasemekana wagonjwa wa maradhi haya wamekuwa wanaongezeka kwa asilimia 26 kwa mwaka. Maradhi haya yameanza kuwa tatizo kubwa hapa kwetu, hivyo hatuna budi kuchukua hatua thabiti kukabiliana nayo.
Kwa sababu ya kukosa uwezo wetu wa ndani, haswa kwa wagonjwa wanaohitaji upasuaji kuwekewa wa moyo, pacemakers au stents, tumelazimika kuwapeleka nje ya nchi kwa matibabu. Ni gharama kubwa, hivyo hatuwezi kuwapeleka watu wengi wanaohitaji tiba hiyo. Matokeo yake ni wagonjwa wengi kuishi kwa mateso na hata kupoteza maisha.
Kwa nia ya kutaka kuokoa maisha ya Watanzania waliopata maradhi ya moyo, ndipo tulipowaomba ndugu zetu wa China. Wakati ule Rais wa China, Mheshimiwa Hu Jintao alitukubalia. Jimbo la Shandong ambalo ndilo limekuwa linatoa madaktari wengi kutoka China, lilikabilidhiwa jukumu la ujenzi wa kituo hiki. Kama nilivyosema, kwa ushirikiiano wa pamoja wa nchi zetu, kituo kimekamilika na kimekwishaanza kutoa huduma.
Tunapofanya uzinduzi wa kituo hiki leo, ni fursa nzuri kuwashukuru marafiki zetu wa China. Tunawashukuru kwa msaada mkubwa waliotupatia na tunawashukuru kwa heshima ya Mjumbe mzito kwenye sherehe hii. Tunashukuru pia kwamba mgeni huyu pia amekuja kumwakilisha Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping na watu wa China katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya Muungano.
Mheshimiwa Waziri;
Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na
Mkuu wa Taasisi Hii;
Kituo kimekamilika sasa kazi kwetu. Tunaomba muhakikishe kuwa kituo hiki kinatimiza majukumu yake kama ilivyokusudiwa. Kwa ajili hiyo, naomba mfanye yafuatayo:
1. Hakikisheni vifaa na mahitaji ya upasuaji yanapatikana wakati wote. Itakuwa haina maana kujenga jengo zuri kama hili na kufundisha mabingwa wa upasuaji wa moyo kisha wasifanye kazi waliyosomea kufanya.
2. MSD ielekezwe kuhakikisha kuwa vifaa na mahitaji hayo yanapatikana wakati wote.
3. Wizara, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Mkuu wa Kituo hiki hakikisheni kuwa mnatoa kipaumbele cha kwanza kwa shughuli za upasuaji katika kituo hiki. Hii ina maana ya mgao wa fedha na mipango ya kazi ya kituo.
4. Waziri na Mkurugenzi Mkuu anzeni kufikiria utaratibu bora wa uandeshaji wa kituo hiki. Angalieni uwezekano wa kufanya kituo hiki kuwa taasisi inayojiendesha chini ya Hospitali ya Taifa, Muhimbili. Nazungumzia mfumo unaokaribia kufanana na Taasisi ya Mifupa. Hii itaihakikishia kituo hiki ustawi na uhai endelevu.
5. Jiepusheni na kishawishi cha kugeuza wodi za taasisi hii kuwa ni wodi za wagonjwa ambao ni watu mashuhuri na wenye uwezo. Ninachoshauri, tengenezeni mpango wa kujenga jengo kama hili kwa watu hao. Nachelea tusije kujikuta, wamejaa watu wengine, wagonjwa wa moyo wakakosa nafasi.
6. Naomba uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, uongozi wa kituo na wafanyakazi kukitunza kituo hiki kwa kiwango cha juu ili kidumu na kilifae taifa letu na watu wake kwa miaka mingi ijayo. Hakikisheni kunafanyika matengenezo kwa wakati. Msifanye ajizi kwani ukarabati husababishwa na kuchelewa kufanya matengenezo. Ukifanya matengenezo kwa wakati huhitaji ukarabati. “Rehabilitation is deferred maintenance”.
Hitimisho
Ndugu Wananchi;
Nimalize kwa kutoa tena shukrani zangu za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China, Rais mstaafu Mheshimiwa Hu Jintao na Rais Xi Jinping, Serikali ya Jimbo la Shandong na Kampuni ya Uhusiano wa Kiuchumi na Kiufundi ya Kimataifa ya Shandong kwa mchango wao uliowezesha ujenzi wa Kituo hiki. Wananchi wa Tanzania wanathamini na kuienzi zawadi hii kutoka kwa wananchi wa China kwa ajili yetu. Serikali ya Tanzania itahakikisha kwamba Kituo hiki kinaendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa kama inavyotarajiwa.
Baada ya kusema haya sasa naomba kutamka kuwa Kituo cha Upasuaji, Tiba na Mafunzo ya Moyo kimefunguliwa rasmi.
Ahsanteni kwa kunisikiliza!