RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Septemba 2, 2014, ameungana na viongozi wengine wa Afrika na wajumbe kutoka nchi mbalimbali duniani kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (AU) kujadili hatari na athari za ugaidi katika Bara la Afrika na namna ya kukabiliana nao.
Katika Mkutano huo kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Kenyatta – Kenyatta International Convention Centre (KICC) mjini Nairobi, Kenya umefanyika chini ya uenyekiti wa Mwenyekiri wa sasa wa Baraza hilo, Mheshimiwa Idrisa Deby, Rais wa Chad.
Nchi zote 15 wanachama wa Baraza hilo zimewakilishwa katika Mkutano huo wa siku moja na miongoni mwa Marais ambao walihudhuria mbali na Rais Kikwete na Rais Deby ni Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Mheshimiwa Goodluck Jonathan, Rais wa Nigeria, Rais wa Somalia, na mwenyeji wa Mkutano huo, Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, Rais wa Kenya.
Rais Kikwete ambaye aliwasili mjini Nairobi usiku wa jana, Jumatatu, Septemba Mosi, 2014, baada ya kukatisha kwa muda ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Dodoma, alitarajiwa kuhutubia Mkutano huo baadaye jioni ya leo.
Kikao cha ufunguzi cha mapema asubuhi, wajumbe walisikia hotuba kutoka kwa viongozi wanne wakianza na Rais Deby ambaye alitoa hotuba ya ufunguzi akifuatiwa na Rais Jonathan ambaye alizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) Mohamed Abdulaziz, Rais wa Mauritania ambaye hakuweza kuhudhuria Mkutano huo.
Rais Jonathan ambaye nchi yake imeathirika mno kutokana na ugaidi wa Kikundi cha Boko Haram amesema kuwa ugaidi unashamiri katika Afrika kwa sababu ya kuongezwa nguvu na uhalifu mwingine wa kimataifa kama vile biashara ya dawa za kulevya, ujangili, biashara ya binadamu, biashara ya fedha haramu.
Amesema kuwa dunia na Afrika inahitaji mbinu nyingine za kukabiliana na ugaidi kwa sababu ya uhalifu huo kusaidiwa na uhalifu wa aina nyingine na ambazo unavuka mipaka ya nchi mbali kwa urahisi zaidi.
Naye Rais Kenyatta ambaye pia nchi yake imeathiriwa mno na ugaidi wa Kikundi cha El Shaabab, amesema kuwa Bara zima la Afrika linakabiliwa na ugaidi zikiwa nchi za eneo la Sahel za Chad, Mali na Libya, eneo la Afrika Mashariki ambalo linasumbuliwa na ugaidi wa El Shaabab na eneo la nchi za Nigeria na Cameroun, ambazo zinasumbuliwa na Boko Haram na eneo la Afrika ya Kati ambazo zinasumbuliwa na ugaidi wa Lord’s Army.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika, Balozi Erasto Mwencha amesema kuwa uteuzi wa Jiji la Nairobi kuandaa Mkutano huo ni mwafaka kabisa kutokana na madhara ambayo Jiji hilo na nchi ya Kenya kwa jumla imekuwa inapitia kwa sababu ya mashambulizi ya ugaidi.
“Kwa pamoja tumekuja hapa kuelezea mshikamano wetu na ukaribu wetu kwa Kenya, wananchi wake na Serikali yake kutokana na mashambulzi ambayo yamekuwa yanaikumba nchi hii,” amesema Balozi Mwencha. Mkutano huo pia umesikiliza Ripoti ya Mwenyekiti wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika kuhusu aina, athari, hatari ya ugaidi na namna nchi hizo zinaweza, kwa pamoja, kukabiliana na kushinda balaa hilo.