Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete amesema chama hicho kitaendelea kujenga taswira nzuri kwa jamii kwa kuwavua viongozi wa chama hicho wenye kashfa mbalimbali na tuhuma ambazo pia zinakichafua chama hicho.
Kikwete ametoa kauli hiyo alipokuwa akihutubia wanachama wa CCM na wafuasi wake katika maadhimisho ya miaka 35 ya kuzaliwa kwa chama hicho mjini Mwanza. Amesema hatua ya kuwaondoa uongozi viongozi wachafu itasaidia kukisafisha chama na kuongeza mvuto kwa wananchi ambao ndiyo mtaji wa chama.
Rais Kikwete amesema CCM itaendelea kufanya mabadiliko ili kiujumla ikiwa ni pamoja na kwenda na wakati na matakwa ya wanachama wake. “Mtaji mkubwa wa CCM ni kuungwa mkono na wananchi…hatuna budi kuwasikiliza wananchi nini wanataka, chama chetu kijitahidi kujenga taswira nzuri kwa wananchi,” alisema Kikwete katika hatuba yake.
Akifafanua juu ya uamuzi wa NEC ya CCM kutaka viongozi wenye tuhuma kujivua gamba, mwenyekiti huyo wa Chama Cha Mapinduzi amesema Mkutano Mkuu wa mwisho wa chama umeamuru viongozi hao waanze kuvuliwa uongozi ngazi za wilaya kama wamegoma kujivua wenyewe.
Amesema CCM lazima ibadiliko kutokana na kuwa na mtanzamo tofauti kwa jamii kutokana na tuhuma na uchafu wa kipuuzi kwa baadhi ya viongozi wake, na kama haitokuwa tayari kufanya mabadiliko itakuwa inakiua chama hicho. “lazima tubadilike, tusipo kubali kubadilika tunakiua chama, NEC ya CCM imekubaliana kwamba kuwa na viongozi wasafi na hodari ni mtaji mkubwa wa chama,” amesema Rais Kikwete.
Alisema taswira ya CCM imechafuka kwa jamii kutokana na kuwa na viongozi wanaonyooshewa vidole jambo ambalo lazima liangaliwe kwa kina na wanaokitakia uhai na mema chama hicho. Kuwa na viongozi wachafu ni sawa na kukiweka chama hicho mashakani, hivyo viongozi wenye tuhuma hawafai kuendelea na nafasi zao. Ameongeza kuwa kiongozi ni kioo cha jamii hivyo anapopoteza sifa ya kuwa kiongozi lazima avuliwe madaraka yake.
Hata hivyo amesema vitendo vya baadhi ya wanachama wa CCM kujenga tabia za kununua nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama zimechafua pia taswira ya chama, hivyo kuitaka Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa kujipanga kukabiliana na wana-CCM wenye tabia hizo katika uchaguzi wa chama hicho mwaka huu.
Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Rais Kikwete, Katibu Mkuu wa CCM taifa, Wilson Mukama alisema licha ya CCM kujivunia mafanikio ya kuwaunganisha Watanzania wote kwa kipindi chote cha uhai wake na kushika hatamu haina budi kujipanga na kutathmini utendaji wake, ikiwa ni pamoja na kufanya mabadiliko yanayokwenda na hali ya kisiasa ya sasa.
Mukama alisema licha ya ushindani mkubwa wa vyama vya upinzani kwa kukishambulia chama hicho bado ni imara na viongozi wake hawana msongo wa mawazo. Sherehe hizo zilipambwa na shughuli mbalimbali pamoja na gwaride maalumu ya vijana wa CCM ambao walitoa heshima kwa Mwenyekiti wao wa Taifa kiukakamavu. Katika maadhimisho hayo CCM ilipokea wanachama wapya 1,847 ambao wanatoka maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza, na kukabidhiwa kadi na Rais Kikwete.
CCM ilizaliwa Februari 5, 1977 na kila ifikapo tarehe hiyo chama huadhimisha kuzaliwa kwa chama hicho.